Muya apewa mkono wa kwaheri Coastal Union

Coastal Union imetangaza kuachana na Kocha wake Mkuu, Mohammed Muya kuanzia leo Jumatano, Aprili 8, 2026.

Taarifa ya Coastal Union leo, imesema kuwa pande hizo mbili zimefikia maridhiano katika kufikia uamuzi huo.

“Uongozi wa Klabu ya Coastal Union umefikia makubaliano ya pande zote ya Kusitisha Kandarasi na Kocha Mkuu Mohammed Muya.

“Klabu inamshukuru Mwalimu Mohammed Muya kwa mchango wake uliotukuka kwa kipindi chote alichoiongoza Timu yetu.

“Uongozi wa Coastal Union utaujulisha umma juu ya Muundo na Uongozi Mpya wa benchi la Ufundi muda mchache ujao,” imesema taarifa ya Coastal Union.

Japo sababu za kufikia makubaliano ya kuachana hazijawekwa hadharani, matokeo yasiyoridhisha ya Coastal Union chini ya Muya yanaonekana kuushawishi uongozi wa timu hiyo kusitisha mkataba wa kocha huyo wa zamani wa Dodoma Jiji na Fountain Gate.

Kocha huyo katika mechi 15 alizoiongoza Coastal Union msimu huu, imepata ushindi mara mbili tu huku ikitoka sare katika michezo saba na imepoteza mechi tisa.

Coastal Union inashika nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa imekusanya pointi 16 katika michezo 18.