Dar es Salaam. Kuendelea kuwepo kwa mashimo katika barabara mbalimbali za mitaa ya Jiji la Dar es Salaam kumechangia kujaa kwa maji hata pale mvua zinaponyesha kidogo.
Hayo yamesemwa na baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam walipozungumza na Mwananchi kuhusu uwepo wa athari za mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali.
Tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha kwa mvua kubwa siku tatu mfululizo zinazoweza kusababisha mafuriko katika baadhi ya mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumanne Aprili 7, 2026, na TMA, mvua hizo zilizoanza jana Jumatano zitanyesha hadi Ijumaa na sitahusisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani pamoja na Jiji la Dar es Salaam, sambamba na visiwa vya Unguja na Pemba.
Mkazi wa Msasani bonde la Mpunga akipita kwenye maji machafu yalitokana na mvua iliyonyesha jijini Dar es Salaam Aprili 8, 2026. Picha na Michael Matemanga
Aidha imeonya mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.
Kutokana na hali hiyo, wananchi hususan wanaoishi maeneo ya Pwani na visiwani, wametakiwa kuwa waangalifu zaidi kutokana na uwezekano wa ongezeko la kiwango cha mvua.
Mwananchi leo Jumatano Aprili 8, 2028, imezunguka katika maeneo mbalimbali kuangalia hali ilivyo ambapo ambayo siku zote huonekana kuwa korofi, ikiwemo Msasani Bwawani, Mwananyamala kwa Msisiri na Tegeta Basihaya, imekuta hali ni shwari.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameeleza huenda kwa kuwa mvua hiyo kwa siku ya leo haijanyesha kubwa, huku wakisema kama itanyesha mfululizo kama ilivyotangazwa huenda hali ikabadilika kwa kuwa udongo wa Dar es Salaam una tabia ya kushiba maji haraka.
“Kiukweli mpaka sasa hivi (ilikuwa saa 8 mchana) hatuwezi kusema tumeshaziona athari, ndio maana unaona tunaendelea na shughuli zetu, maana huku hali ikiwa mbaya hata ndani hamtoki,” amesema Winfrida Kisanga, mkazi wa Msasani Bwawani.
Kwa upande wake, Angel Lameck, Mkazi wa Tegeta Basihaya, amesema kinachowatesa kwa sasa ni mashimo yaliyoko kwenye barabara ambapo mvua zikinyesha yanajaa maji na kugeuka mabwawa jambo linalowapa taabu kupita si tu waenda kwa miguu bali na vyombo vya moto.
“Nadhani ifike mahali hata kama wameshindwa kututengenezea barabara basi watujazie vifusi vinavyotoka kwenye barabara wanazozibomoa na kuzitengeneza upya,”amesema Angle.
Naye Saleh Mwamasanga, Mkazi wa Msasani Bwawani amesema tangu kumetengenezwa mitaro mikubwa katika maeneo hayo kuna ahueni hali iliyopunguza wasiwasi mvua zikinyesha.
Mwamasanga pia hakuwa mbali na Angel ambapo ameeleza kwa sasa barabara za mtaani ndio shida kwani mvua kidogo tu ikinyesha kunakuwa na madumbwi yanayosababisha adha kwa watumiaji wa barabara husika.
Maji ya mvua yaliyojaa njiani na kuwa kero kwa watumiaji katika mtaa wa Basihaya jijini Dar es Salaam, Aprili 8, 2026,. Picha na Michael Matemanga
Shani Allen mkazi wa Mwananyamala Msisiri amesema ukiacha barabara, lakini pia kuna baadhi ya watu wamejenga na kuziba mifumo ya maji ambapo mvua zikiwa nyingi yanakosa pa kutokea.
Shani ameomba mamlaka zinazohusika na kusimamia mazingira, ziwe zinafanya kaguzi hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua kuwabaini watu hao na kuwachukulia hatua.
“Sisi wananchi kupambana na watu hawa wanaoziba mikondo ya kupitisha maji mvua zinaponyesha hatuwamudu kwani wengine ni watu wenye hela lakini zikifika mamlaka naamini kuna jambo litafanyika,” amesema.
Jack Mwesiga, mkazi wa Chanika Zingiziwa, amesema kuna haja barabara zinapotengenezwa hata kama ni kwa kuzikwangua, kuwekwe mitaro pembeni itakayowezesha kupitisha maji mvua zikinyesha.
Mwesiga amesema hatua hiyo pia itasaidia Serikali kuokoa hela za mara kwa mara kufanya matengenezo.
Kelen Clemence, mkazi wa Gongo la Mboto, amesema kumekuwa na taabu ya usafiri kutokana na hali hiyo, na kueleza kwamba amechelewa kufika ofisini kutokana na hilo.
Hata hivyo, wakati mvua ikiwa neema kwa baadhi ya watu, kuna wanaoteseka kwa uwepo wao wakiwemo waendesha bodaboda.
Samson Semiono mwendesha bodaboda maeneo ya Ubungo, amesema mvua hizo zimefanya biashara kwao kuwa ngumu, kwani ni abiria wachache wanaokubali kupanda pikipiki huku wanaloana.
Mwendesha bodaboda mwingine, Emmanuel Joachim amesema katika kipindi hiki, faida wanayopata kwenye usafiri huo wanagawana na fundi kutokana na kuzitengeneza mara kwa mara kunakochangiwa na kuingia maji.
“Ni kutokana na hali hii, hata sehemu ambayo ulikuwa uende kwa Sh1,000 inabidi utoze Sh1,500 ili kufidia haya, kwa kuwa safari moja kupeleka abiria, nyingine kwa fundi,” amesema Joachim.
