Namungo yalenga historia mpya Ligi Kuu ya NBC

PAMOJA na kukiri ugumu wa ligi, Namungo imesema kati ya mechi 12 ilizobakiza inasaka japo pointi 18 ili kujihakikishia usalama, huku ikihitaji kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).

Hadi sasa Namungo imecheza mechi 18 na kuwa nafasi ya tisa kwa pointi 22 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara. Timu hiyo imebakiza mechi 12 kumaliza msimu huu, ambapo kwa sasa inajiandaa na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya TRA United, utakaopigwa Aprili 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi.

Msimu wa 2019-2020, Namungo ilicheza fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba na kulala kwa mabao 2-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nahodha wa Namungo, Jacob Masawe alisema hawajawa na matokeo mazuri sana licha ya jitihada zao uwanjani, lakini wanayo malengo yao kuhakikisha wanabaki salama.

Alisema katika mechi 12 zilizobaki, wanapambana wavune pointi 18 ambazo zitawafanya kufikisha 40, ambapo kwa kufanya hivyo wataweza kujihakikishia nafasi nzuri na kuondoa presha za mwisho wa ligi.

“Si kwamba kuna tatizo lolote bali ni ushindani wa timu pinzani na ugumu wa ligi kwa ujumla, tunajitahidi kupambana lakini matokeo si mazuri sana kama tulivyotarajia, hesabu zetu kama tutakosa ushindi michezo yote iliyobaki basi tukusanye japo pointi 18,” alisema.

Nyota huyo mwenye historia ya kuwa nahodha timu anazocheza, ameongeza kuwa kwa sasa wanafikiria mchezo ujao wa Kombe la FA dhidi ya TRA United kuhakikisha wanashinda na kufuzu robo fainali.

Alisema ndoto zao ni kufanya vizuri kwenye michuano hiyo na kufikia rekodi waliyowahi kuiweka ya kucheza fainali na ikiwezekana kubeba taji kwa mara ya kwanza kutokana na hamasa waliyonayo hivi sasa.

“Tunajua ni mchezo mgumu kwakuwa wapinzani nao wanaonesha ushindani kwenye ligi, lakini Namungo hatujafika hatua hii kwa bahati mbaya, tunahitaji historia mpya ya kutwaa ubingwa msimu huu,” alisema mkongwe huyo.