DAKIKA 626 alizocheza kiungo wa Yanga, Allan Okello katika Ligi Kuu Bara akihusika na mabao matatu kufuatia kufunga mawili na asisti moja, imemfanya kocha wa timu hiyo, Pedro Goncalves kusema kijana huyo kutoka Uganda anapambana kufanya kazi nzuri.
Pedro alibainisha kwamba, kiungo mshambuliaji huyo anayetumia zaidi mguu wa kushoto, namba zake zimeendelea kuwapunguzia presha Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli.
Moja kati ya sajili ambazo zimeingia dirisha dogo la Januari 2026 ndani ya Yanga na kuonekana kufanya vizuri mbali na Laurindo Depu, ni Mganda huyo aliyetokea Vipers ya nchini kwao.
Unaweza kusema alitua Yanga na kismati kwani tangu asajiliwe amekaa benchi kwenye mechi moja pekee ya ligi dhidi ya Simba iliyochezwa Machi 1 mwaka huu. Mpaka sasa, Okello amecheza mechi tisa za ligi kwa dakika 626.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro alisema, siyo siri uwepo wa Okello unaongeza nguvu kubwa hasa eneo la mbele la kikosi hicho.
Alisema kazi nzuri ambayo ameanza kuifanya ya kutengeneza nafasi ndicho kitu cha muhimu zaidi kwani anatoa uwepesi kwa washambuliaji kufunga mabao kirahisi zaidi.
“Hatua ya Okello kuanza kutengeneza asisti na kuendelea kufunga itazidi kuimarisha kiwango chake yeye mwenyewe kama mchezaji, ukiachilia mbali timu.
“Ubora wake ni chachu kwenye kikosi chetu na unapunguza presha iliyokuwa kwa Pacome na Maxi ambao awali walikuwa wana kazi ya kutengeneza nafasi.
“Okello akiendelea kuwa na ubunifu mkubwa wa kutengeneza nafasi anaweza kuwa moja ya viungo hatari siyo ndani ya Yanga pekee, hata Ligi Kuu,” alisema.
Katika kikosi cha Yanga, Maxi ambaye tangu msimu uanze hajakosa mechi hata moja ya ligi, amefunga mabao mawili na asisti tatu, huku Pacome aliyepata majeraha yaliyomfanya akae nje na kukosa mechi tano mfululizo, ana rekodi ya kucheza mechi 13 kati ya 18 ambazo timu hiyo imecheza, huku akiwa na mabao manne na asisti mbili.
Kati ya viungo hao wote, Pacome ndiye namba zake zipo juu, huku Mivory Coast huyo na Maxi wote wakiitumikia Yanga kwa misimu mitatu mfululizo.
Yanga bado iko kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa imecheza mechi 17, ikishinda 12 na sare tano ikifikisha pointi 41 ikiwa kwenye mapambano ya kutetea taji la ligi hiyo ililochukua misimu minne mfululizo na mara 31 kwa jumla.