‘Pray for KMC’ mechi 18, pointi 8 yajichimbia mkiani NBC PL

JAHAZI la Klabu ya KMC kubakia Ligi Kuu Bara, linaendelea kuzama siku baada ya siku, kufuatia kikosi hicho kuchapwa bao 1-0, dhidi ya Singida Black Stars, katika mechi kali na ya kuvutia iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Airtel, mjini, Singida.

Katika mechi hiyo, bao pekee la wenyeji, Singida, lilifungwa na winga nyota wa timu hiyo, Mgambia Lamine Jarjou, dakika ya 70, baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa KMC walioshindwa kuuokoa mpira, uliokuwa unaelea kwenye eneo la kikosi hicho.

Timu hizo zimekutana ikiwa ni siku chache zimepita tangu zivunje mabenchi ya ufundi kutokana na mwenendo usioridhisha, ambapo Singida iliachana na Mkenya David Ouma, huku kwa upande wa KMC FC, ikiachana na Kocha, Abdallah Mohamed ‘Baresi’.

Uamuzi wa Singida wa kuvunja benchi la ufundi ulifikiwa ikiwa ni muda mfupi tu tangu timu hiyo ichapwe mabao 2-0, dhidi ya TRA United, Aprili 5, 2026, katika mechi ya Ligi Kuu, iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri, Abeid, jijini, Arusha.

Ouma aliyetangazwa rasmi kushika wadhifa huo, Januari 5, 2026, akichukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyejiunga na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, aliondolewa na aliyekuwa meneja mkuu wa kikosi hicho, Othmen Najjar, raia wa Tunisia.

Kwa upande wa uongozi wa KMC ulifikia makubaliano ya kuachana na ‘Baresi’, kwa makubaliano ya amani ya pande zote mbili, huku kocha huyo akidumu kwa siku 94, sawa na miezi mitatu na siku nne, tangu alipotambulishwa rasmi, Desemba 30, 2025.

Baresi aliyejiunga na KMC FC, Desemba 30, 2025, akichukua nafasi ya Mbrazil Marcio Maximo, aliyeondoka, Desemba 6, 2025, alifikia makubaliano ya kuondoka ndani ya kikosi hicho, kutokana na mwenendo usioridhisha kwa msimu huu wa 2025-2026.

Uamuzi wa kuachana na Baresi, ulifikiwa Aprili 3, 2026, ikiwa ni muda mfupi tu tangu kocha huyo achapwe mabao 3-2, dhidi ya Mbeya City, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara.

Kwa matokeo ya leo, yanaifanya Singida kupata ushindi wa kwanza, baada ya kuchapwa mechi mbili mfululizo, ambapo kwa sasa kikosi hicho kinashika nafasi ya tano na pointi 28, kikishinda mechi nane, sare nne na kupoteza sita kati ya 18.

Kwa upande wa KMC, inafikisha mechi tano mfululizo za Ligi Kuu bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Mashujaa bao 1-0, Februari 3, 2026, ikiendelea kuburuza mkiani mwa msimamo mwa nafasi ya 16, baada ya kukusanya pointi zake nane.

Katika mechi 18, ilizocheza KMC katika Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, timu hiyo imeshinda miwili tu, ikitoka sare pia miwili na kupoteza 14, ikifunga mabao saba na kuruhusu 29, ikiendelea kushika nafasi ya 16 na pointi nane hadi sasa.