Rais Kagame atoa ujumbe akitahadharisha maisha ya chuki

Kigali. Rwanda imeanza rasmi maadhimisho ya miaka 32 tangu kutokea kwa mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi ya Aprili 7, 1994, tukio lililosababisha vifo vya zaidi ya watu milioni moja ndani ya kipindi cha siku 100.

Maadhimisho hayo yameanza leo huku wananchi wa taifa hilo wakiongozwa na Rais wao, Paul Kagame, wakiingia katika kipindi cha siku 100 za kumbukizi, kinacholenga kuenzi waliopoteza maisha na kutoa nafasi ya kutafakari historia hiyo chungu.

Mauaji hayo yanatajwa kuwa miongoni mwa matukio mabaya zaidi katika historia ya binadamu, yakichochewa na utawala wa wakati huo ulioeneza kwa muda mrefu propaganda, ubaguzi na chuki dhidi ya Watutsi.

Katika kipindi hicho cha siku 100, zaidi ya Watutsi milioni moja waliuawa kikatili kutokana na mpango ulioratibiwa kwa umakini mkubwa.

Wachambuzi wa mambo nchini Rwanda wanansema mauaji hayo hayakutokea kwa bahati mbaya, bali yalikuwa matokeo ya maandalizi ya muda mrefu yaliyohusisha kusambazwa kwa itikadi za chuki ndani ya jamii.

Wanamgambo wa Interahamwe walipewa mafunzo na silaha, huku jamii ikihamasishwa kushiriki katika vitendo hivyo vya kinyama. Matokeo yake, hata majirani, ndugu na marafiki waligeuka na kuwa maadui, wakishiriki katika mauaji dhidi ya watu waliowafahamu kwa karibu.

Akizungumza leo Jumatatu Aprili 7, 2026, katika viunga vya Kigali Genocide Memorial,   wakati wa uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya Kwibuka 32 na kuwasha mwanga wa matumaini (mshumaa wa kumbukizi), Rais wa Rwanda, Paul Kagame amesema tukio hilo linawakumbusha Wanyarwanda na dunia kwa ujumla umuhimu wa kulinda utu wa binadamu na kusimama imara dhidi ya chuki.

Rais Kagame amesema kumbukizi ya mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi si tukio la kuadhimisha historia pekee, bali ni wajibu wa kizazi cha sasa na kijacho kuhakikisha kuwa maovu hayo hayajirudii tena katika radhi nchi yao.

“Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 hayakutokea ghafla, bali yalitokana na itikadi ya chuki iliyojengwa kwa muda mrefu, jambo linalopaswa kuwa funzo si kwa Wanyarwanda tu, bali jamii zote duniani,” amesema Rais huyo.

Amesema kukumbuka ni zaidi ya wajibu na ni ahadi ya pamoja ya kuhakikisha kuwa yaliyotokea hayajirudii tena.

Rais huyo amesema licha ya maumivu makubwa yaliyosababishwa na mauaji hayo, Rwanda imeweza kusimama tena na kujenga taifa lenye umoja, mshikamano na dira ya maendeleo.

Aidha, ameonya kuhusu kuendelea kuwepo kwa dalili za itikadi za chuki katika baadhi ya maeneo, akihimiza juhudi za pamoja za kitaifa na kimataifa katika kupambana na upotoshaji wa historia na kauli za uchochezi, hususan kupitia majukwaa ya kidijitali.

Ametoa wito kwa vijana kuchukua nafasi ya mbele katika kulinda ukweli wa historia, kuendeleza amani na kupinga vitendo vyote vinavyoweza kuhatarisha mshikamano wa Wanyarwanda walionao hivi sasa.

Maadhimisho ya Kwibuka 32 yataendelea kwa siku 100, yakilenga kuwaenzi waliopoteza maisha, kuimarisha mshikamano na kuendeleza safari ya uponyaji na ujenzi wa taifa la Rwanda.

Hata hivyo, Mwananchi imezungumza na mtaalamu wa historia  nchini humo, Alex Habyelimana amesema hakuna tukio la mauaji ya kimbari linalotokea ghafla, bali hujengwa taratibu kupitia misingi ya ubaguzi, chuki na propaganda zinazodhoofisha utu wa binadamu kwa muda mrefu.

Ametoa rai kwa Wanyarwanda kuchukua hatua ya kudhibiti hali hiyo punde wakiibaini ili kuepusha kujirudia tena,

“Tunamshukuru Mungu sasa hivi nchi imetulia na sidhani kama kuna mtu anatamani kuona hali hiyo ikijitokeza tena, ndiyo maana sasa hivi kila Mnyarwanda amekuwa mlinzi wa amani ya nchi yake kama anavyosisitiza Rais Kagame,” amesema Habyelimana.

Amesema baada ya janga hilo, ndiyo maana  Rwanda ilianza safari ya uponyaji, maridhiano na ujenzi upya wa taifa.

Amesema ikiwa imetimia miaka 32 sasa, nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika kuimarisha umoja wa kitaifa, amani na maendeleo.

Hata hivyo, tahadhari inaendelea kutolewa kuhusu kuibuka kwa dalili za itikadi hizo hatarishi, hususan katika baadhi ya jamii za diaspora na katika ukanda wa Maziwa Makuu, ambapo mitandao ya kijamii imekuwa chombo cha kusambaza ujumbe wa chuki na upotoshaji.

Katika maadhimisho ya mwaka huu ya Kwibuka 32, wananchi wanahimizwa kuchukua jukumu la kupinga itikadi hizo na kulinda ukweli wa historia.

Naye Jesca Ndyeshime anasema vijana wanapaswa kutumia majukwaa ya kidijitali vizuri ili kupambana na taarifa potofu na kuendeleza mshikamano.

Wakati huo huo, jijini Dar es Salaam, Tanzania, hafla ya kumbukumbu  imefanyika eneo la Mlimani City ikiwakutanisha viongozi wa serikali, wananchi wa Rwanda wanaoishi nchini humo, wanadiplomasia na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.

Washiriki wa hafla hiyo wametoa heshima kwa waliopoteza maisha na kuonesha mshikamano kwa manusura, huku wakisisitiza kuwa kukumbuka si wajibu wa kihistoria pekee, bali ni dhamira ya kuhakikisha kuwa matukio kama hayo hayajirudii tena.

Wanyarwanda hao wameitumia hafla hiyo kuthibitisha wajibu wa pamoja wa kulinda utu wa binadamu, kuimarisha amani na kupinga chuki katika jamii, kwa lengo la kuendelea kuijenga nchi yao iwe ya haki, usawa na mshikamano wa kweli.

Mbali ya kuwasha mwanga wa matumaini asubuhi, jioni, Rais Kagame ameongoza pia wananchi wake katika matembezi ya mshikamano ya umbali wa kilomita moja yaliyoanzia katika viunga vya Remera jijini Kigali na kuishia katika Uwanja wa BK Arena ambako wananchi waliwasha pia mishumaa ikiwa ni Ishara ya kuwakumbuka waliofariki dunia katika mauaji hayo ya kutisha.