Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema uamuzi wake wa kumteua Profesa Palamagamba Kabudi, kumrithi hayati William Lukuvi, umetokana na umri, uzoefu na maarifa ya mwanasiasa huyo.
Hata hivyo, amesema ataendelea kumtumia Profesa Kabudi katika majukumu ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, huku akiendelea na wadhifa wake wa sasa wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.
Profesa Kabudi, aliteuliwa Aprili 2, mwaka huu, kumrithi Lukuvi aliyefariki dunia Machi 25, mwaka huu. Pamoja na Profesa Kabudi, wengine walioteuliwa siku hiyo ni Dk Festo Dugange, kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Pia, Reuben Kwagilwa, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, huku aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Dk James Andilile uteuzi wake ukitenguliwa.
Wengine ni Balozi Said Othman Yakub aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Balozi Ali Mwadini kuwa Katibu wa Rais, Angela Kizigha na Dk Everline Munisi, waliteuliwa kuwa wabunge.
Rais Samia ameeleza hayo leo, Jumatano Aprili 8, 2026 wakati akiwaapisha wateule hao, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Amesema jamii yoyote isiyo na mtu mzima haitaenda vizuri, hivyo ililazimika atafutwe mtu wa namna hiyo, mwenye maarifa, mzoefu, anayeijua nchi, historia na awamu zote ndiyo apewe nafasi hiyo.
“Kwa hiyo tumeona mtu mzima wetu hapa ni Kabudi. Pole nakuapisha kwa mara ya tatu ndani ya kipindi kifupi. Nilikuapisha ukiwa Waziri wa Habari, ukiwa Waziri ofisi kwangu, nakushukuru sana kwa kazi uliyoifanya,” amesema.
Ameeleza Kabudi akiwa katika ofisi yake, amefanya kazi nzuri ya kuizungumzia vema nchi hadi hatua iliyofikia sasa na kwamba ataendelea kumtumia kwa kazi hizo, huku akitumika katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Sikumwona mtu mwingine aliyesoma na mwenye umahiri kama wewe kwenye ofisi hiyo. Kwa uwezo ulionao sina shaka jukumu utalimudu. Tunaanza na utekelezaji wa dira inataka uratibu ndani ya Serikali baina ya sekta zetu,” amesema.
Katika uratibu huo, amesema Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka ndiye alikuwa mratibu mkuu ambaye ni kijana kama wengine, hivyo Profesa Kabudi ni sahihi kwa kuwa mtu mzima.
Amesema pia inahitajika sauti yenye ukomavu na uzamivu wa mambo, hivyo Profesa Kabudi ana sifa zote hizo, ndiyo maana ameteuliwa.
“Pole sana kwa kazi nzito, lakini ndiyo hivyo, kwenye fungu ndiko kunakoongezwa. Hongera sana,” amesema.
Kwa upande wa naibu mawaziri, amesema wamewabadili aliyekuwa Tamisemi amepelekwa mazingira na aliyekuwa mazingira amepelekwa Tamisemi.
Sababu ya uamuzi wake huo, amesema ni namna alivyomwona Kwagilwa akiwa mchakarikaji alipokuwa Tamisemi, huku Ndugange akimfananisha na Padri kwa upole wake.
“Yeye mwache akasimamie afya sijui elimu naye siyo mgeni Tamisemi, ameshafanya kazi nzuri. Zile hekaheka zako (Kwagilwa) twende tukasimamie mazingira ya Tanzania,” amesema.
Kwa upande wa Mdemu, amesema uzoefu wake ni mkubwa hivyo anakosa zaidi ya kumwelezea zaidi ya kuondoa shaka na uwezo wake.
