Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametangaza kupunguza msururu wa magari katika misafara yake, ikiwa ni hatua ya awali za kupunguza matumizi ya mafuta kutokana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo duniani.
Katika utekelezaji wa hilo, mkuu huyo wa nchi amesema, badala ya wakuu mbalimbali wa idara wanaoongozana naye kutumia magari yao, kwa sasa wote watapanda kwenye basi moja na kuacha magari yao.
Uamuzi huo unakuja wakati Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alipoeleza mpango wa Serikali kufanya kila linalowezekana kubana matumizi ya mafuta kutokana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo.
Bei ya mafuta imepanda nchini na duniani kutokana na vita Mashariki ya Kati vinavyohusisha mataifa ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, vilivyokwaza mnyororo wa ugavi wa nishati hiyo.
Kutokana na vita hiyo, Iran iliufunga mlango wa Bahari wa Hormuz, unaotumika kupitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa duniani.
Hata hivyo, tayari kumekuwa na ahadi ya kufunguliwa kwa mlango huo baada ya makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano kwa wiki kadhaa.
Rais Samia ametoa kauli hiyo Ikulu jijini Dodoma leo, Jumatano Aprili 8, 2026, alipohutubia baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateuwa wiki iliyopita.
Amesema anatambua ndani ya Serikali kuna matumizi makubwa ya mafuta, kwani magari na safari ni nyingi, akiwataka maofisa waanze kupunguza matumizi ya nishati hiyo.
Amesema hilo linaanzia kwenye ofisi yake, badala ya kuongozana na maofisa wakiwa na magari yao, sasa wote watapanda kwenye basi moja kumfuata.
“Msafara utakuwa gari yangu, escort yangu ya polisi na gari ya akiba nyuma. Waliobakia wote nawaingiza kwenye basi ili tupunguze matumizi ya mafuta,” amesema.
Amewataka watumishi wengine hata kwenye ofisi zao wahakikishe wanapunguza matumizi ya nishati hiyo.
Katika hotuba yake, amesema kinachoendelea Mashariki ya Kati ndicho kilicholeta athari kwa ulimwengu wote, na wiki iliyopita alitumiwa kuhusu bei za mafuta katika mataifa mbalimbali duniani.
“Kuna nchi ambazo zimeshawapa watu wao ruhusa ya kufanya kazi nyumbani ili kusiwe na safari za magari kwenda ofisini na kurudi. Kuna nchi zimepunguza matumizi ya mafuta na wana upungufu wa mafuta.
“Leo tumeamka na neno la faraja, kwamba angalau pale Harmon’s, ukiongea nao vizuri, vile vimeli vinapitapita, inatupa matumaini kwamba meli itapita. Na ile kuruhusu tu mali za Japan na Ufaransa kidogo nimeona bei ya mafuta imeshuka kidogo,” amesema.
Amesema hiyo inatoa matumaini, lakini pia haijulikani wataamkaje, namna wanavyoamka ndiyo itakayochochea bei ya nishati hiyo.
Kwa kuwa upandaji wa bei ya mafuta unaambatana na kupanda kwa bei za bidhaa, Rais amewataka wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa walizonunua kabla ya msukosuko huo ziko na bei stahiki.
“Isitumike fursa ya kupanda kwa mafuta na kuweka bei za bidhaa kubwa kuliko zinavyopaswa kuwa. Wananchi, kuna bidhaa ambazo zinaingia kipindi hiki ambazo zimekumbana na msukosuko huu zitapanda bei,” amesema
Ameeleza hayo hayakusababishwa na Serikali bali ni athari za mazingira ya ulimwengu, huku akidokeza bei ya mafuta nchini ni ndogo ukilinganisha na mataifa mengine.
“Wananchi muwe watulivu na wastahimilivu, sisi kama viongozi wan chi mbalimbali tunajitahidi kuzungumza na wenzetu ili vita hivi vimalizike na mambo yarudi kuwa kawaida,” amesema.
Amesema iwapo hali itaendelea kuwa tulivu kama ilivyotangazwa leo, huenda hata Tanzania bei ya mafuta ikashuka kwa tangazo la mwezi ujao, ukilinganisha na iliyopo sasa.
