Bagamoyo. Serikali imezindua rasmi mafunzo ya siku tano kwa maofisa uvuvi na wakaguzi wa mazao ya uvuvi wapatao 25 kutoka ukanda wa Bahari ya Hindi, katika juhudi za kuimarisha sekta ya uvuvi ili ichangie zaidi katika uchumi wa Taifa.
Mafunzo hayo, yanayoendelea mkoani Pwani, yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (Feta).
Akifungua mafunzo hayo leo, Aprili 8, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Mohammed Shekhe amesema Serikali inakusudia kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa (GDP) kutoka asilimia nane ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
Profesa Shekhe amebainisha kuwa Tanzania inasafirisha nje takribani tani 60,000 za mazao ya uvuvi kila mwaka, hali inayoiingizia nchi zaidi ya Sh500 bilioni tangu mwaka 2021.
“Sekta ya uvuvi ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi wetu. Ni wajibu wenu maafisa kuhakikisha mnasimamia ubora wa mazao na kuzingatia viwango vya kimataifa ili kuongeza ushindani wa bidhaa zetu,” amesema.
Amewataka washiriki kutumia elimu watakayopata kikamilifu na kuitekeleza kwa vitendo katika maeneo yao ya kazi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Feta, Dk Semvua Msigani, amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea maafisa hao uwezo wa kusimamia sheria, kanuni na viwango vinavyotakiwa katika sekta ya uvuvi.
“Tumelenga kuhakikisha washiriki wanakuwa na uelewa wa kina wa kanuni na sheria za nchi ili mazao yanayosafirishwa nje yakidhi viwango vinavyokubalika kimataifa,” amesema Dk Msigani, akibainisha kuwa uelewa huu utapunguza changamoto za kukataliwa kwa mazao katika masoko ya nje na kuongeza mapato ya taifa.
Kaimu Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Christian Nzowa, amesema mafunzo haya ni mwanzo wa programu pana itakayohusisha maafisa uvuvi kutoka kanda nyingine nchini.
“Haya ni mafunzo ya awali kwa ukanda wa Bahari ya Hindi, lakini mpango ni kuyapanua na kuwafikia pia maafisa wa ukanda wa Ziwa Tanganyika na maeneo mengine nchini,” amesema, akisisitiza umuhimu wake katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kuongeza thamani ya mazao.
Maofisa uvuvi wanachukua jukumu muhimu katika kulinda rasilimali za bahari na maji na kuhakikisha zinatumika kwa njia endelevu, sambamba na kusimamia ubora wa mazao, jambo linalochangia kuimarisha biashara ya nje na kuongeza mapato ya fedha za kigeni.
Sekta ya uvuvi inaendelea kuwa chanzo kikuu cha ajira, lishe na kipato kwa maelfu ya Watanzania, huku Serikali ikijenga mikakati ya kuongeza uzalishaji na usafirishaji wa mazao ya mifugo na uvuvi ili kukuza uchumi wa viwanda.
Kupitia mafunzo haya, Tanzania inalenga kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kusimamia kikamilifu sekta ya uvuvi na kuhakikisha mchango wake katika maendeleo ya taifa unakua kwa kiwango cha juu, ikihakikisha sekta hii inabaki nguzo muhimu ya uchumi, biashara ya nje na ustawi wa wananchi.