Straika KMC akataa unyonge | Mwanaspoti

WAKATI KMC hali ikiendelea kuwa tete kwenye Ligi Kuu Bara, straika wa timu hiyo, Adam Uledi amesema iwapo atashindwa kuipigania timu kubaki basi kazi kubwa itakuwa ni kujipagania mwenyewe kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.

Alisema kwa matokeo yalivyo hivi sasa, hataki kurudia historia iliyojitokeza kipindi akikipiga KenGold aliyoipandisha na kushuka nayo msimu uliopita, kabla ya kuibukia Transit Camp baadaye kutua KMC.

Nyota huyo alijiunga na KMC dirisha dogo la usajili Januari 2026 akitokea Transit Camp akiwa kinara wa mabao Ligi ya Championship alipofunga 11 ambapo kwa sasa amefunga bao moja akiwa na wana Kinondoni wanaoburuza mkia wa Ligi Kuu Bara kwa pointi nane.

Akizungumza na Mwanaspoti, Uledi amekiri hali kutokuwa nzuri akieleza kuwa bado hawajakata tamaa kwani ligi haijaisha na lolote linaweza kutokea kwa sababu wachezaji wanaendelea kupambana.

Alisema licha ya kiwango bora alichonacho, hesabu kubwa ni kuipambania timu kubaki Ligi Kuu na iwapo mipango itagoma hana budi kujipigania kuendeleza ubora wake ili abaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.

“Mambo ni mawili, kuipaginia timu kwanza ikigoma ni kujipigania mwenyewe ili kubaki na kiwango changu kitakachonibakisha Ligi Kuu, kiujumla matokeo si mazuri ila hatujakata tamaa, mechi bado zipo na tunaweza kufanya lolote,” alisema mshambuliaji huyo.

Aliongeza kuwa kupungua kwa kasi ya mabao tofauti na ilivyokuwa Championship ni kutokana na mabadiliko ya mazingira aliyopo kwani Ligi Kuu ushindani ni mkali na kwamba anaamini atarejesha makali kwani anapata nafasi ya kucheza.