Wabunge wataja mambo saba kupunguza makali ya bei ya mafuta

Dodoma. Wabunge wametoa ya moyoni kuhusu suala la mafuta wakitaja mambo saba ambayo yanaweza kupunguza makali hayo ili kutoa nafuu ya maisha kwa wananchi.

Miongoni mwa mambo hayo ni kuuza akiba ya dhahabu ili kuongeza ruzuku kwenye mafuta, kuongeza uzalishaji wa gesi na kupunguza gharama, kuondoa baadhi ya tozo kwenye mafuta, kushughulika na madalali wa mafuta na kujenga maghala ya kuhifadhia mafuta.

Nyingine ni ushauri kwa Waziri Mkuu ili akate posho za vikao na kuzuia visivyo vya lazima, lakini wakataka aliyesema kuna akiba ya mafuta miezi mitatu akasababisha taharuki kwa wananchi ajitokeze hadharani kutoa ufafanuzi.

Kauli za wabunge zimetolewa leo Jumatano Aprili 8, 2026 wakati wakichangia kwenye hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na wizara zilizo chini yake kwa ajili ya mapato na matumizi ya mwaka 2026/27.

Kauli za wabunge ni mwendelezo wa mkakati kwa watunga sheria hao kutaka Serikali itoe kauli ya matumaini kwa wananchi kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta kulikosababishwa na vita inayoendelea Mashariki ya Kati.

Spika wa Bunge, Mussa Zungu aliagiza Kamati ya Nishati kukutana haraka na Wizara ya Nishati ili watoe kauli yenye mwelekeo wa ukweli kuhusu suala la mafuta.

Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu amesema mahali Taifa lilipofikia ni lazima Waziri Mkuu akubali kupunguza vikao vya lazima na kukata posho ili kiasi kitakachookolewa kielekezwe kwenye ruzuku ya mafuta.

Kingu amesema huu ni wakati wa Serikali kwenda mbele zaidi kwa hatua 100 ili iweze kupunguza dhahama kwa wananchi ambao ndiyo wenye maumivu kutokana na kupanda kwa mafuta.

“Wenzetu TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania) wamekwenda mbele zaidi na kuja na matumaini kuwa tutapata ahueni kuanzia Mei hadi Juni, nawapongeza sana, sasa Waziri Mkuu pokea ushauri huu kwamba umefika wakati lazima tujenge maghala yetu yatakayosaidia wakati wa dhiki hata tuwauzie wengine.”

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kata matumizi lakini ondoa hata baadhi ya kodi, ukifanya hivyo utachukua pointi tano za nchi na Taifa litatabasamu, lakini umefika wakati turuhusu kampuni nyingine kushindana kwenye biashara ya mafuta siyo hao wanne waliopo sasa,” amesema Kingu.

Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Jonas Mbunda ameitaka Serikali kuwekeza zaidi kwenye uzalishaji wa gesi na kupunguza gharama ili watu wengi waone umuhimu wa kutumia gesi hata katika vyombo vya usafiri.

Mbunge wa Ukonga (ACT-Wazalendo), Bakari Shingo ameitaka Serikali kuweka mkazo ili bei ilipofikia isiongezeke kwani  ikipanda zaidi itapelekea maumivu kwa wananchi.

“Lakini, naishauri Serikali ipunguze kodi kwenye baadhi ya  tozo za mafuta kwani suala la mafuta linaongeza mfumuko wa bei bila sababu za msingi, tutumie nafasi hii kuongeza posho kwa watumishi wetu ili waendane na hali ilivyo sasa,” amesema Singo.

Kwa upande wake Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM), Ezra Chiwelesa ameihoji Serikali kwa nini aliyetoa taharuki kwa wananchi asijitokeze hadharani kueleza hali ikoje kuhusu mafuta.

Chiwelesa amesema si jambo jema kwa watu wasiojua kuzungumza kwenye mambo magumu kuachwa waseme kwani inazua maswali mengi.

“Ndiyo maana Rais alianzisha Wizara ya Mahusiano, fanyeni utaratibu wa kuona nani anaweza kuzungumza kipi na wakati upi, sasa kwenye hili kwa nini hakuachiwa Waziri wa Nishati au Naibu Waziri ndiyo waseme,” amehoji Chiwelesa.

Mbunge huyo amesema kuwa kuna mtumishi alitoka hadharani akasema Tanzania inayo akiba ya mafuta kwa zaidi ya miezi mitatu mbele, lakini ghafla hali ikabadilika hivyo akaomba mtu huyo ambaye hakumtaja kwa jina arudi hadharani kusema ni wapi alikuwa amekosea.

Katika mchango wake Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola yeye amemtaka Waziri Mkuu kuwasha moto ili awachome aliowaita ni madalali wa mafuta kwani haiwezekani wakawepo na wawe wanatazamwa.

Lugola ameanza kwa kumpa sifa Dk Mwigulu Nchemba kwamba alipoteuliwa kushika wadhifa huo, hotuba yake iliwavutia na yeye (Lugola) akajua chuma kimeingia.

“Lakini, Waziri Mkuu kasi uliyokuja nayo siyo hii uliyonayo, shambulia kabisa tupo pamoja na wewe, hawa madalali wa mafuta choma kabisa wateketee,” amesema Lugola.

Naye Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe amesema hakuna namna kwa hali ilivyo ni lazima Serikali ikubali kuuza akiba ya dhahabu iliyopo ili fedha zitakazopatikana zikasaidie kupunguza makali ya mafuta.

Mafuwe amesema kimfaacho mtu chake, hivyo dhahabu iliyopo kwenye akiba ni mali ya Watanzania wakati wanaoteseka na bei ya mafuta ni Watanzania hivyo umefika wakati kutumia rasilimali zake kuwasaidia wananchi.

Mafuwe pia aliunga mkono suala la kuwa na hifadhi ya kutosha ya mafuta ili yanapokuja majanga isaidie kuwapa ahueni wananchi lakini kuuza hata kwa majirani.

Wabunge wataendelea kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu ambayo inatarajia kuhitimishwa mapema wiki ijayo.