Dodoma. Tanzania kama yalivyo mataifa mengine, inakabiliwa na jukumu la kusaka mbinu za kuokoa fedha ili kulinda uchumi wake dhidi ya misukosuko inayotokana na vita vya Mashariki ya Kati, vilivyosababisha kupanda kwa bei ya mafuta.
Wanazuoni wa masuala ya uchumi, wameonya bila nidhamu ya haraka ya matumizi ya fedha za umma, gharama za mafuta zinazoendelea kupanda zitasababisha kupanda kwa bei za bidhaa na huduma nchini.
Wanazuoni hao wanatoa ushauri hao kipindi ambacho wabunge leo, Jumatano Aprili 8, 2026 wanaendelea na mjadala wa makadirio ya bajeti ya Sh12.5 trilioni ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Mjadala huo utahitimishwa Aprili 15, 2026.
Wanasema Serikali inapaswa kuchukuliwa hatua za haraka za kutathmini upya vipaumbele vya matumizi.
Awali, wakichangia makadirio ya mapato na matumizi hayo Aprili 2, mwaka huu, baadhi ya wabunge waliishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza matumizi na kuacha kuendesha mambo kama hakuna changamoto, kama ilivyoelezwa na Mbunge wa Buchosa (CCM), Erick Shigongo.
“Ombi langu mimi, sitamani kuona tunaingia kwenye hali ngumu ya uchumi kama Taifa, natamani kuona tunaendesha maisha yetu kama Serikali katika kujibana kutokana na hali tulionayo,” alisema.
Mbunge wa Nyasa (CCM), John Nchimbi alisema eneo la matumizi ya magari ya Serikali linatumia fedha nyingi, akisema ni wakati muafaka liangaliwe upya.
“Iangaliwe aina ya magari yanayotumika na kazi anazozifanya mtumishi. Utakuta mtumishi yeye ni mkurugenzi, tena hapahapa Dodoma na kazi zake hazimlazimu kutoka nje ya mkoa lakini anatumia gari la Sh480 milioni.
“Kwa nini anatumia gari la gharama hiyo wakati haendi mbali? Serikali inatumia magari aina ya V8 zaidi ya 400, wakati kuna wengine hawakupaswa kuyatumia hayo,” alisema.
Nchimbi, alisema hata hao wanaotumia V8 hivi sasa, kuna tatizo la mafuta, lakini madereva wa magari wanayawasha kuanzia asubuhi hadi jioni yakiwasubiri viongozi.
“Unajiuliza hawa wanajua kama haya mafuta yananunuliwa kwa dola? Lakini ni gharama ya Serikali, mtu anangurumisha gari kuanzia asubuhi hadi mchana akimsubiri bosi wake ili lisipate joto,” alisema.
Aidha, Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT Wazalendo), Ado Shaibu, aliitaka Serikali kueleza kwa uwazi maandalizi yake kukabiliana na hali hiyo.
Katika swali lake hilo, alionyesha hofu ya usumbufu katika minyororo ya usambazaji duniani inayoweza kuathiri mifumo ya usafiri, bima na masoko ya bidhaa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alijibu yote hayo, akiwahakikishia wabunge Serikali iko tayari kuepuka matumizi yasiyo ya lazima huku ikiendelea kufanya tathmini za mara kwa mara kulinda uchumi.
Baadaye Aprili 4, mwaka huu alipoulizwa na Mwananchi
kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabili hatari tarajiwa kutokana na mijadala inayoendelea na wadau wa usafiri, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema wanafanyia kazi jambo hilo kwa umuhimu mkubwa.
“Wataalamu wanachakata namna bora ya kufanya na wakati wowote Serikali itatoa mwelekeo tutakaochukua. Tunawaomba wananchi wavumilie muda mfupi ujao watajulishwa,” alisema.
Mapendekezo ya wachambuzi
Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Dk Nasibu Mramba, amesema udhibiti wa matumizi katika taasisi zote za Serikali haukwepeki kwa sasa.
Amesema miradi inayoweza kusubiri iahirishwe hadi hali ya kimataifa itakapokuwa nafuu, huku fedha zikielekezwa katika huduma muhimu za kijamii.
Pia, ameshauri matumizi yanayogharimu fedha nyingi, kama sherehe za kitaifa ikiwamo Siku ya Muungano, Mei Mosi na Sikukuu ya Uhuru, ziahirishwe kwa muda ili kuokoa fedha kwa mahitaji ya dharura.
Mhadhiri mwingine kutoka CBE, Dk Benedict Mwakabungu, amependekeza Serikali ipunguze matumizi ya kawaida, hususan ununuzi wa magari ya kifahari na ya gharama kubwa.
“Kuhusu hatua za muda mrefu, napendekeza kutokana na kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa duniani, sasa ni wakati wa kuacha kutegemea mafuta pekee na badala yake kutumia fursa ya gesi,” ameshauri.
Mtaalamu wa sheria na masuala ya kimataifa, Dk Lutengano Mwinuka, amependekeza kuboreshwa kwa ufanisi wa kiutendaji serikalini.
“Nashauri Serikali ipunguze safari zisizo za lazima ndani ya nchi zinazotumia mafuta mengi, ipitie upya sera za kodi kwa bidhaa muhimu kama mafuta, na iongeze uwezo wa hifadhi ya mafuta ya Taifa kufikia akiba ya miezi sita hadi 12 ili kukabiliana na mishtuko ya baadaye,” amesema.
Athari za kupanda kwa bei ya mafuta tayari zinaanza kuonekana. Watoa huduma za usafiri kote nchini wameonya uwezekano wa kuongeza nauli wakieleza gharama za uendeshaji kuwa kubwa kupita kiasi.
Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imechukua msimamo mkali kwa kutishia kufuta leseni za watoa huduma watakaoongeza nauli bila kibali.
Licha ya katazo hilo la Latra, baadhi ya wananchi maeneo mbalimbali wamekutana bei mpya za usafiri kwenye daladala, bajaji na bodaboda.
Matarajio kikao cha Latra leo
Baada ya hali hiyo, Latra imeitisha kikao cha wadau leo Jumatano, Aprili 8, 2026 jijini Dar es Salaam kupokea maoni yao kuhusu hatua za kuchukuliwa endapo gharama za mafuta zitaendelea kuongezeka.
Kikao hicho kitaendeshwa ana kwa ana na mtandaoni ili kutoa fursa wa walioko nje ya Dar es Salaam kushiriki.
Kwa mujibu wa taarifa ya Latra, mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Karimjee kuanzia saa tatu asubuhi, huku ikiwaalika wadau wote wa masuala ya usafiri kushiriki kikao hicho.
Wakati hayo yakijiri, Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), jana Jumanne, kiliitisha kikao cha kamati ya utendaji kujadili mapendekezo ya nauli watakayowasilisha leo mbele ya wadau wa usafiri katika kikao cha Latra.
“Ni kweli tumeitisha kikao cha kamati ya utendaji kitafanyika leo Jumanne mchana (jana), ajenda ni moja kuhusu nauli tutakazozipendekeza baada ya mafuta kupanda. Tutakuwa na wahasibu wetu watakaochakata viwango tutakavyopendekezwa kisha kesho tutawasilisha kwenye mkutano,“ amesema Mustapha Mwalongo ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji Taboa.
Hata hivyo, Mwalongo ambaye ni msemaji wa Taboa, hakuwa tayari kuzungumzia viwango vipya vya nauli watakavyovipendekeza, akisema ni mapema hadi pale watakapomaliza kikao cha kamati ya utendaji wa chama hicho.
