Tabora. Watu wawili mkoani Tabora inadaiwa wamejinyonga hadi kufa, akiwemo mkazi wa Igembensabo, Kata ya Uyui, Ngalawa Idd (50). Ngalawa amekutwa amejinyonga kwenye mti karibu na shambalake.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumanne, Aprili 7, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amedai chanzo cha tukio hilo ni marehemu kushindwa kuhimili deni la ng’ombe alilokuwa akidaiwa na watu.
“Mtu huyo alikuwa akiwekezewa ng’ombe kwenye zizi lake ili awafuge, lakini kumbe hakuwa akiwafuga na baada ya kuanza kudaiwa akaamua kujinyonga,” amesema.
Amesema marehemu Ngalawa enzi za uhai wake alikuwa akiwekezewa ng’ombe ili kuwafuga kwenye zizi, lakini hakuwa akifanya hivyo. Baada ya kuanza kudaiwa mifugo hiyo ambayo haikuwa ya mtu mmoja, ndipo akajinyonga.
Aidha, Kamanda Abwao amesema mwili umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete, huku akitoa wito kwa wananchi kuwa waaminifu wanapopewa mali za watu ili kujiepusha na misongo ya mawazo isiyo ya lazima.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao akizungumzia matukio ya watu wawili kujinyonga .
“Tuache kujipa mawazo ya lazima. Kama unaona huwezi kukaa na mali ya mtu, ni afadhali kukataa ili usijiumize mwenyewe maisha yako pale utakapoingiwa tamaa, hata ya kuuza pengine,” amesema.
Katika tukio jingine, Shabani Luhende (25), mkazi wa Mtaa wa Kizigo mkoani humo, amekutwa amejinyonga ndani ya chumba kimoja wapo katika nyumba aliyokuwa akiishi na babu yake.
Kamanda Abwao amedai mbinu aliyotumia kijana huyo ni kufunga kamba kwenye kenchi ndani ya chumba hicho na kujining’iniza, na kusababisha kifo chake.
“Tunaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kuchukua uamuzi wa kujiua, kwa sababu si rahisi mtu kuamua kufa,” amesema.
Amesema sababu za kuchukua uamuzi huo bado hazifahamika, ila uchunguzi unaendelea ili kuzibaini.
Mwili wa Luhende umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete kwa ajili ya uchunguzi zaidi na utakabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi.
