Aliyeshtakiwa kwa mauaji ya mwanafunzi aachiwa

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, imemwachia huru Elia Daniel, aliyekuwa ameshtakiwa kwa mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Ayatsea, Suzana Ginyabasi.

Hukumu hiyo iliyomwachia huru mshtakiwa huyo ilitolewa Aprili 8, 2026 na Jaji Devotha Kamuzora na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Mahakama baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili ilibaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka yoyote.

Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani kwa shtaka moja la mauaji, kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, kosa alilodaiwa kutenda Aprili 29,2025, katika Kijiji cha Gidamara ndani ya Wilaya ya Babati katika Mkoa wa Manyara.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 10 na vielelezo 16.

Ilidaiwa siku ya tukio mwanafunzi huyo aliondoka nyumbani kwao asubuhi kwenda shuleni, lakini hakuwahi kurejea.

Shahidi wa nane, ambaye ni baba wa marehemu, Samweli Ginyabasi, alidai kuanza kumtafuta na akaarifiwa kwamba alionekana mara ya mwisho katika eneo la shule na baadaye alionekana akiondoka hata hivyo, hakuna mtu aliyejua alipo.

Alidai jambo hilo liliripotiwa awali kwa mamlaka za serikali za mitaa na baadaye katika Kituo cha Polisi cha Galapo.

Kwa mujibu wa shahidi huyo na shahidi wa sita, Mkapa Ginyabasi, Mei Mosi, 2025, taarifa ilitolewa, ambapo jamii ilikusanyika na kuanza msako na mwili wa mwanafunzi huyo ulidaiwa kukutwa kwenye shamba.

Baada ya mwili huo kupatikana, polisi waliarifiwa na shahidi wa pili Koplo Asha akifuatana na Sajenti Elias, walienda hadi eneo la tukio wakiwamo hapo,  waliarifiwa kwamba mshtakiwa   alikuwa amekamatwa na wanakijiji kwa tuhuma za kuhusishwa na kosa hilo.

Walienda kwenye ofisi za kijiji na baadaye wakampeleka mshtakiwa Kituo cha Polisi cha Galapo.

Shahidi wa saba alidai mwili wa marehemu ulikuwa umevalia sare ya shule,  shati jeupe na sketi ya bluu ambapo katika eneo la karibu na mwili huo mita 12 kulikutwa nguo ya ndani ya kiume.

Baada ya vielelezo kukusanywa vilikabidhiwa na kupelekwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA).

Shahidi wa kwanza, Dk Christopher Malagashimba, daktari, aliyeufanyia uchunguzi mwili huo alidai kuwa   ulikuwa na damu ikitoka puani na masikioni, pamoja na michubuko sehemu kadhaa na kuwa aliona uhamaji usio wa kawaida wa shingo, jambo lililoashiria uwezekano wa kunyongwa.

 Zaidi ya hayo, aliona majeraha yakienea kutoka ukeni hadi kwenye sehemu ya haja kubwa jambo linaloashiria unyanyasaji wa kingono na kuhitimisha kuwa chanzo cha kifo kilikuwa upungufu wa oksijeni kwenye ubongo unaosababishwa na kunyongwa, kutokwa na damu nyingi kutokana na majeraha aliyopata.

Shahidi wa tisa, Dk Joshua Dawson wa Hospitali ya Mrara, alishuhudia kwamba aliombwa kutoa sampuli ya damu kutoka kwa mshtakiwa kwa madhumuni ya kwenda kufanya vipimo vya sampuli za vinasaba (DNA) ambapo alivikabidhi kwa shahidi wa saba, ofisa Polisi kisha vikapelekwa GCLA, Kanda ya Arusha.

Vielelezo hivyo vilidaiwa kukabidhiwa kwa shahidi wa tano, aliyedai kuwa GCLA Kanda ya Arusha haifanyi uchambuzi wa DNA, hivyo alivisafirisha hadi GCLA, Dar es Salaam, kwa ajili ya uchambuzi huo. Katika maabara ya Dar es Salaam, alikabidhi vielelezo hivyo kwa shahidi wa tatu, Boniface Emanuel.

Shahidi wa tatu alikiri kupokea, kwa madhumuni ya upimaji wa DNA, vielelezo ambavyo ni vazi jeusi la ndani linaloripotiwa kuvaliwa na marehemu, vazi la kubana lenye rangi ya kaki, ambalo pia lilidaiwa kuvaliwa na marehemu, vazi la kubana lenye rangi nyingi lililopatikana kutoka eneo la uhalifu, majimaji ya ukeni yaliyokusanywa kutoka kwa marehemu, sampuli ya damu iliyochukuliwa kutoka kwa mshtakiwa na nguo ya ndani.

Matokeo ya uchunguzi wa DNA yaliwasilishwa mahakamani yakionyesha kuwa kulikuwa na ulinganifu kati ya sampuli ya damu ya mshtakiwa na DNA iliyopatikana kwenye mwili wa marehemu pamoja na baadhi ya vielelezo vilivyokusanywa eneo la tukio.

Mshtakiwa alikana kusababisha kifo cha marehemu, isipokuwa kwa kukubali kwamba sampuli ya damu ilichukuliwa kutoka kwake, alikataa kwamba nguo ya ndani ya kiume iliyopatikana katika eneo la uhalifu ilikuwa yake.

Alishuhudia kwamba, wakati huo, alikuwa akiishi katika eneo tofauti ambapo alikuwa akichunga ng’ombe na kuwa alishtakiwa kwa kosa la uongo.

Wakili wa Jamhuri alidai ingawa kulikuwa na tofauti ndogo katika ushahidi wa PW9 kuhusu ni nani hasa aliyetoa sampuli ya damu kutoka kwa mshtakiwa, haikuwa na ubishi kwamba sampuli ya damu ilichukuliwa kutoka kwake.

Hata hivyo, pamoja na ushahidi huo, mahakama ilibaini kuwepo kwa dosari kubwa katika namna ushahidi huo ulivyokusanywa na kushughulikiwa, hali iliyozua mashaka juu ya uhalali wake kisheria.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Kamuzora alieleza kuwa sheria ya Udhibiti wa DNA ya Binadamu inaweka masharti maalumu kuhusu ukusanyaji na usimamizi wa sampuli za DNA, ikiwa ni pamoja na nani anaruhusiwa kukusanya sampuli hizo.

Mahakama ilibaini kuwa kulikuwa na mkanganyiko mkubwa katika ushahidi wa upande wa mashtaka kuhusu nani hasa alichukua sampuli ya damu ya mshtakiwa.

Ingawa daktari mmoja alidai kuwa ndiye aliyekusanya sampuli hiyo, alikuja kubadilisha kauli yake baadaye na kusema kuwa alisimamia tu hatua hiyo iliyofanywa  na mtu mwingine ambaye hakuthibitishwa kuwa alikuwa na sifa za kisheria kufanya kazi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Mahakama ilieleza kuwa uhalali wa sampuli hiyo haukuweza kuthibitishwa ipasavyo, na hivyo kuathiri uaminifu wa matokeo yote ya uchunguzi wa DNA yaliyotegemea sampuli hiyo.

Jaji Kamuzora amesema hata kama ushahidi wa DNA ungechukuliwa kuwa halali, bado ulikuwa na mapungufu, kwani baadhi ya vielelezo muhimu kama nguo ya ndani ya kiume iliyodaiwa kuwa ya mshtakiwa havikuonyesha ulinganifu wowote wa DNA na mshtakiwa.

Amesema  kuwa katika sheria za jinai, ushahidi wa kitaalamu kama DNA haupaswi kutegemewa peke yake bila kuwepo ushahidi mwingine wa ziada unaounga mkono madai ya mashtaka na kuwa katika kesi hiyo, hakukuwa na shahidi yeyote aliyeshuhudia tukio hilo wala ushahidi wa moja kwa moja unaomhusisha mshtakiwa na mauaji hayo.

Zaidi ya hayo, haikuwekwa wazi ni kwa namna gani mshtakiwa alihusishwa na tukio hilo hadi kukamatwa kwake na wananchi.

Mahakama pia ilizingatia utetezi wa mshtakiwa, ambaye alidai kuwa alikamatwa bila sababu za msingi na kuhusishwa na tukio hilo kutokana na migogoro binafsi aliyokuwa nayo na mwajiri wake katika kazi ya uchungaji.

Kwa mujibu wa mshtakiwa, siku ya tukio alikuwa katika eneo tofauti akichunga mifugo, na alikamatwa baadaye baada ya kuitwa na mwajiri wake na kupelekwa katika ofisi za kijiji, kabla ya kukabidhiwa kwa polisi.

Mahakama ilibaini kuwa maelezo hayo hayakupingwa na upande wa mashtaka, hali iliyoongeza mashaka juu ya uhusika wake katika tukio hilo na kwa kuzingatia mapungufu hayo yote, Jaji Kamuzora alihitimisha kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka ya msingi, kama inavyotakiwa na sheria.

“Ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha kesi yao bila kuacha shaka yoyote. Katika kesi hii, ushahidi uliowasilishwa haukidhi kiwango hicho,” alieleza katika hukumu yake.

Kutokana na hitimisho hilo, Mahakama iliamuru mshtakiwa aachiliwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.