Chadema yaanzisha kampeni kushinikiza kuachiwa Lissu

Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maedeleo (Chadema), Tundu Lissu, akitimiza mwaka mmoja akiwa mahabusu, chama chake kimetangaza kuanzisha kampeni maalumu kupitia mitandao ya kijamii pamoja na kubandika matangazo katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, kikishinikiza aachiwe huru.

Chama hicho kimesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha umma wa ndani na kimataifa kuungana katika kudai haki ya kiongozi huyo, kikisisitiza kuwa endapo Serikali haitachukua hatua, kitaitisha maandamano ya amani kushinikiza kutekelezwa kwa takwa hilo.

Msimamo huo wa Chadema umeungwa mkono na Katibu Mkuu wa Chama cha ODM cha Kenya, Edwin Sifuna, aliyesema kuwa chama chake kitaungana nao kwa kutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kushinikiza kuachiwa kwa Lissu.

Kauli hizo zimetolewa leo, Aprili 9, 2026, kupitia mjadala wa mtandaoni ulioandaliwa na Chadema, ukiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutiwa mbaroni kwa kiongozi huyo.

Katika mjadala huo, viongozi na wanachama wa chama hicho wamesisitiza umuhimu wa kulinda misingi ya haki, demokrasia na utawala wa sheria, wakieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuhamasisha mjadala mpana kuhusu haki za kisiasa nchini.

Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, katika mji wa Mbinga, mkoani Ruvuma, alipokuwa akihamasisha kampeni ya chama chake yenye kaulimbiu ya “No Reforms, No Election” (hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi).

Akifungua mjadala wa mtandaoani wa kampeni hiyo, leo, Aprili 9, 2026, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, ametangaza kuanza kwa kampeni hiyo, akisema ni hatua ya kuonesha msisitizo wa chama katika kudai kuachiwa huru kwa Lissu bila masharti yoyote.

“Hatutaendelea kukaa kimya na kulia, tutaitisha maandamano makubwa nchi nzima ili utawala usikie na kumuachia Lissu. Hatutakaa kimya tena kuwataka wao kwa huru, wao waone ni lini, kwa furaha yao, watamuachia Lissu,” amesema.

Heche amesema kampeni hiyo kupitia mitandao ya kijamii itakuwa kubwa na yenye lengo la kuongeza uelewa kwa Watanzania kuhusu suala hilo.

Ameongeza kuwa viongozi wa chama hicho watakutana na baadaye kutoa tamko rasmi litakalobainisha hatua na muda wa kuanza kwa harakati za kushinikiza kuachiwa kwa Lissu.

“Kwa niaba ya chama chetu, hatutapiga magoti na hatutakubali kulamba viatu vya wadhalimu. Tunataka haki itendeke na ionekane inatendeka,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha ODM cha Kenya, Edwin Sifuna, amesema muungano wa vyama vya siasa 30, ambao Lissu ni miongoni mwa viongozi wake, umekuwa ukitoa matamko mbalimbali ukiitaka Serikali ya Tanzania kumuachia huru kiongozi huyo au kuharakisha mchakato wa kesi yake.

Sifuna amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mdau anayejali misingi ya demokrasia kuonesha wasiwasi pale kunapojitokeza dalili za kudorora kwake, akifananisha hali ya ukandamizaji wa demokrasia na namna ugonjwa wa Uviko-19 ulivyokuwa ukisambaa kwa kasi duniani.

“Hata sisi kwenye mitandao yetu tutaungana na Chadema kushinikiza aachiwe huyo kiongozi, ni haki ya kila Mtanzania kupigania haki ya Lissu,” amesema Sifuna, ambaye ni Seneta wa Nairobi.

Kwa upande wake, mwanaharakati Maria Sarungi ameeleza namna Lissu anavyosimamia haki nchini.

“Tangu awali, Lissu amekuwa akinivutia kwa sababu alikuwa ni mtu anayependa ukweli hadi sasa. Uwanaharakati wake umetokana na kupenda haki na ukweli na imefikia hatua ambayo huwezi kumshauri asiseme ukweli,” amesema.

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala, amekumbusha kuwa wakati Lissu akikamatwa na kuwekwa lupango, chama chake kilikuwa huru, lakini sasa nacho kimefungiwa kwa namna zote.

Pamoja na hayo, amesema Chadema kimeendelea kuimarika na kuwa chama kikuu cha upinzani kwa kuendelea kuvutia watu zaidi na ndicho chama imara kilichopo.

Amesema Lissu amekaa mwaka mzima gerezani na gharama watakayolipa wao ni kutokubali kununuliwa.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Amani Golugwa, amemtaja Lissu kama ishara ya udhabiti, ujasiri na kujitolea kwa mapambano ya demokrasia.

“Kukamatwa kwake hakukuwa mwisho wa sauti yake bali ulikuwa mwamko wa mwanzo wa kudai haki, uhuru na utu kwa kila Mtanzania, hasa sauti yake kubwa juu ya nchi hii ya kuhitaji mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi ili kuwepo kwa uchaguzi huru na haki,” amesema.

Pia, mbunge wa Bunge la Ulaya na Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, David McAllister, kupitia taarifa ya pamoja aliyoitoa na wabunge wenzake, wameeleza kusikitishwa na kinachoendelea dhidi ya Lissu nchini, wakitaka kuachiwa huru kwa kiongozi huyo.

“Mwaka mmoja uliopita, Lissu alifungwa na tangu wakati huo ameendelea kuwekwa katika kifungo cha upweke bila fursa ya dhamana. Tunatoa wito wa kuachiliwa huru mara moja na bila masharti kwa Tundu Lissu, pamoja na kuondolewa kwa marufuku ya kisiasa dhidi ya Chadema,” imeeleza taarifa hiyo.