Chakwera awasili Tanzania, atumwa na Jumuiya ya Madola

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Malawi, Lazarus Chakwera amewasili nchini kwa ziara ya kikazi usiku wa kuamkia leo Alhamisi Aprili 9, 2026, ikiwa ni takriban miezi sita imepita tangu ilipotangazwa angewasili kama kiongozi wa ujumbe wa Jumuiya ya Madola.

Novemba mwaka jana, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Botchwey, alimteua Chakwera kuwa mjumbe maalumu wa jumuiya hiyo, na ilitangazwa angefanya ziara ya siku nne nchini kuanzia Novemba 18 hadi 21, lakini hakuonekana kama ilivyotarajiwa.

Katika ziara hiyo ya awali, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Jumuiya ya Madola, angefanya majadiliano na wadau mbalimbali kuhusu masuala yanayohusiana na uchaguzi na mustakabali wa maendeleo ya nchi.

Ilielezwa angekutana na viongozi wa Serikali, wanasiasa, mashirika ya kiraia, viongozi wa dini, mila, na wadau wa kitaifa na kimataifa ili kuanzisha mjadala jumuishi kuhusu maridhiano, haki za kisiasa na kuimarisha demokrasia.

Ziara hiyo ya awali ilitangazwa wiki chache baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka jana, siku ambayo kuliibuka maandamano yaliyozaa vurugu, zilizosababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali za umma na binafsi.

Rais wa Zamani wa Malawi, Lazarus Chakwera na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Ayorkor Botchwey, amewasili nchiniAprili 8, 2026 kwa ziara ya kikazi. Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe.

Hata hivyo, haikuwahi kuwekwa wazi ni nini kilikwamisha ziara hiyo ya siku nne ya Chakwera. Hata Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati huo aliwahi kuiambia Mwananchi kuwa hakuwa na taarifa za ziara ya kiongozi huyo nchini.

Lakini, Chakwera anakuja mwezi mmoja baada ya Tanzania kupokea ujumbe mwingine wa jumuiya ya kimataifa. Ilimpokea mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Parfait Onanga-Anyanga, aliyefanya ziara nchini kuanzia Machi 8 hadi 12.

Katika ziara hiyo, Onanga-Anyanga alizungumza na viongozi wa vyama vya ACT Wazalendo, Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na asasi za kiraia kuhusu yaliyotokea Oktoba 29.

Hata hivyo, Chadema baadaye ilimwandikia barua Katibu Mkuu wa UN, António Guterres, ikimweleza wasiwasi wake kuhusu mjumbe huyo, kwa kile ilichodai kuwa anaweza kuwa na mgongano wa maslahi, kwani aliwahi kufanya kazi na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro.

Taarifa ya kuwasili kwa Chakwera nchini imetolewa usiku wa kuamkia leo Alhamisi, na amepokewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, ziara ya Chakwera inatarajiwa kujumuisha mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Tanzania, ambapo masuala ya kuimarisha demokrasia na haki za binadamu yatajadiliwa.

Rais wa Zamani wa Malawi, Lazarus Chakwera na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Ayorkor Botchwey, amewasili nchini Aprili 8, 2026 kwa ziara ya kikazi. Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe.

Aidha, anatarajiwa kukutana na wadau mbalimbali, wakiwemo wawakilishi wa asasi za kiraia, sekta binafsi na vyama vya siasa, ili kujenga msingi wa mshikamano na hatua za maridhiano.

Ziara hiyo inatazamwa kama sehemu ya jitihada za Jumuiya ya Madola katika kuimarisha uhusiano na nchi wanachama wa Afrika Mashariki, huku ikilenga kuongeza ushirikiano katika maeneo ya utawala bora.