Dodoma. Serikali imewapa kipimo watumishi wa umma kwamba hawatapandishwa vyeo kwa kigezo cha kukaa muda mrefu ofisini, bali watapewa vyeo kwa kupimwa kwa matokeo.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Aprili 9, 2026 na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba wakati akijibu swali la Mbunge wa Monduli (CCM), Isack Capriano ambaye amehoji ni mkakati upi wa Serikali kuwa na timu ya kufuatilia ahadi na maagizo ya Serikali yanayotolewa kwenye ziara za viongozi.
Mbunge huyo katika swali lake kwa Waziri Mkuu amesema baadhi ya maeneo ambayo viongozi hupita kwenye ziara, akiwemo Dk Mwigulu mwenyewe, kero za wananchi hupatiwa ufumbuzi papo hapo lakini nyingine hutolewa maagizo ambayo bila kuwa na ufuatiliaji huenda zikabaki hivyo.
Waziri Mkuu amesema vitengo vya tathmini na ufuatiliaji vimeboreshwa na Serikali imekuwa na mfumo mzuri wa kufanya tathmini na mrejesho.
“Tunaanzisha mpango mzuri wa kuwa na jedwali litakalosaidia kupata tathmini ya maelekezo na namna yalivyotekelezwa. Je, kiongozi wa ngazi ya chini ya kijiji alipokea hoja ngapi na alisaidiaje wananchi kuwafikia viongozi? Siyo mtumishi kupandishwa cheo kwa kukaa ofisini muda mrefu,” amesema Dk Mwigulu.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza Halmashauri zote nchini kutenga mapato ya ndani kwa ajili ya kuwalipa walimu wa kujitolea, kwani jukumu la kuajiri walimu siyo la wazazi.
Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea (Chaumma), Agnesta Kaiza ambaye amehoji kuhusu utitiri wa michango mashuleni.
Kaiza ameuliza mkakati upi uliowekwa na Serikali kukomesha michango holela ambayo amesema imekuwa ni sawa na kausha damu.
Waziri Mkuu amekiri uwepo wa utitiri wa michango mashuleni ambayo mingi inachangishwa bila utaratibu na hivyo kuwaumiza wazazi.
Dk Mwigulu amesema michango hiyo inaondoa na kufifisha kauli ya Serikali ya elimu bila malipo ambayo inamtaka mtoto asome kuanzia awali hadi kidato cha nne bure.
“Nchi yetu haijataka watoto au wazazi walipe walimu wanaojitolea. Kazi ya kuajiri walimu ni ya Serikali, ndiyo maana tumekuwa na waraka maalumu wa kuelekeza aina ya michango,” amesema Dk Mwigulu.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema mchango uliokubalika ni unaohusu chakula cha wanafunzi shuleni huku akisifia baadhi ya juhudi za walimu katika kuwasaidia watoto kuzifikia ndoto zao.
