……….
Na: Dk. Reubeni Lumbagala
Nakumbuka mwalimu wangu wa somo la Uraia (Civics) alipokuwa akitufundisha mada (topic) ya “Haki za “Binadamu” (Human Rights) tulipokuwa Kidato cha Kwanza, alituambia mengi kuhusu haki za binadamu.
Miongoni mwa mikazo yake, alituambia hivi: Haki ya kuishi (Right to life) ndiyo haki kubwa kuliko zote maana mtu anapokuwa hai ndipo anakuwa na uwezo wa kupata haki nyingine zote. Nilimwelewa vizuri sana.
Kimsingi, uhai ni muhimu katika maisha ya mwanadamu, ndiyo maana inapotokea mtu ameugua, na akawa hana uwezo wa kumudu gharama za matibabu yake, basi familia, ndugu, jamaa na marafiki hushikamana kwa kuchangishana fedha kunusuru uhai wa ndugu yao huyo.
Watoto ni kundi ambalo lipo hatarini kukabiliwa na magonjwa mbalimbali. Ni kutokana na msingi huo, serikali inajitahidi sana kutoa chanjo za magonjwa mbalimbali ili kuimarisha na kujenga afya zao ili kuwa na kinga ya kutosha ya kuweza kupambana na magonjwa.
Taasisi ya Doris Mollel (DMF) ni wadau muhimu hapa nchini katika suala la afya ya mama na watoto. Ni taasisi inayopambana sana kuhakikisha maisha ya mama na watoto yanakuwa salama dhidi ya vifo hasa vitokanavyo na uzazi.
Taasisi hii chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji wake, Doris Mollel, imejikita katika kusaidia vifaa vya kuweza kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya muhula (njiti) katika vituo vya afya na hospitali mbalimbali nchini.
Bi. Mollel alipata msukumo wa kuanzisha taasisi hii kwani yeye ni miongoni mwa watoto waliozaliwa kabla ya muhula na alizaliwa mama yake alipokuwa na ujauzito wenye wiki 27 huku akizaliwa na uzito wa gramu 900 tu. Kupona kwake kumempa msukumo wa kutetea maisha ya wanawake na watoto ili wawe salama katika suala zima la uzazi kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya afya.
Kupitia taasisi hii, vituo vya afya na hospitali nyingi zimepata msaada wa vifaa, jambo linalosaidia kuokoa maisha ya maelfu ya wanawake na watoto. Hata mtoto anapozaliwa na uzito pungufu, anapata wasaa wa kuwekewa kwenye wodi maalum ya uangalizi wa watoto njiti (NICU).
Aidha, kutokana na vifaa vilivyopo humo na unyonyeshaji unaoendelea kutoka kwa mama yake, uzito wa mtoto huongezeka. Na pale wataalamu wanapojiridhisha juu ya kuimarika kwa afya ya mtoto, mtoto huyo hutolewa katika wodi hiyo na kuendelea na maisha mengine ya kunyonya kutoka kwa mama yake.
Mwezi Machi, 2026, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetambua kazi kubwa na nyingi zinazofanywa na DMF, na hivyo kumpa tuzo ya heshima Doris Mollel kama njia ya kutambua mchango wake katika kuboresha na kukuza afya mama na mtoto nchini Tanzania.
Tuzo hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus katika Makao Makuu ya WHO, Geneva, Uswisi. Binafsi, nampongeza Bi. Mollel kwa tuzo hiyo kwani jitihada zake za kupigania afya ya mama na watoto zimezaa matunda, na maisha ya wengi yameokolewa kupitia juhudi zake.
Harakati za Bi.Mollel zinaongozwa na kauli yake isemayo “Nikiacha kupigana, watoto njiti watafariki”. Hakika, tuzo hii ni heshima kwa Bi.Mollel na Tanzania kwa ujumla.
Maoni; 0620 800 462.