…..
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali imesema imepiga hatua kubwa katika kuimarisha usawa wa kijinsia na elimu jumuishi kupitia utekelezaji wa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Uwalimu (Teachers Education Support Program TESP), uliolenga kuhakikisha haki na fursa sawa zinapatikana kwa wote katika vyuo vya ualimu nchini.
Akizungumza leo Aprili 9, 2026 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema mradi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuondoa vikwazo vya kijinsia katika elimu ya ualimu kwa kuhakikisha wanafunzi na watumishi wanapata fursa sawa katika mafunzo, ajira na nafasi za uongozi.
Amesema kupitia TESP, vyuo vya ualimu vimewezeshwa kuweka mazingira rafiki yanayozingatia mahitaji ya makundi yote, hususan wanawake na watu wenye mahitaji maalum, hatua inayochochea ushiriki wao kikamilifu katika sekta ya elimu.
“Mradi huu umehakikisha kuwa hakuna anayebaguliwa kwa misingi ya jinsia. Kila mwanafunzi na mtumishi anapata haki sawa ya kushiriki katika mafunzo na kupewa nafasi za uongozi,” alisema Prof. Nombo.
Alifafanua kuwa pamoja na kuboresha miundombinu katika vyuo 34 vya ualimu, TESP umezingatia pia matumizi ya teknolojia ya kisasa, upatikanaji wa vifaa vya kidigitali na mifumo ya maktaba, ambayo yote yamechangia kupanua fursa za kujifunza kwa usawa.
Kwa mujibu wa Prof. Nombo, mradi huo pia uliwajengea uwezo walimu katika masuala ya uongozi jumuishi, hatua inayosaidia kuondoa mianya ya ubaguzi na kuongeza uwiano wa kijinsia katika nafasi za maamuzi.
Aidha, amesema majengo mapya yaliyojengwa kupitia mradi huo yamezingatia mahitaji ya makundi yote, ikiwa ni pamoja na mazingira rafiki kwa wanawake na watu wenye ulemavu, sambamba na kuzingatia mabadiliko ya tabianchi.
Kuhusu uendelevu, Prof. Nombo alisisitiza kuwa licha ya mradi kufikia mwisho wake kimkataba, serikali imejipanga kuhakikisha mafanikio ya usawa wa kijinsia yanaendelezwa katika vyuo vyote vya ualimu.
“Hatutaruhusu mafanikio haya kupotea. Wizara kwa kushirikiana na wakuu wa vyuo tutaendelea kusimamia sera na mifumo inayolinda usawa na haki kwa wote,” alieleza.
Katika hatua nyingine, alibainisha kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewekeza takribani shilingi bilioni 140 katika mradi huo, huku washirika wa maendeleo kutoka Global Affairs Canada wakichangia bilioni 92, uwekezaji unaolenga si tu kuboresha elimu bali pia kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwa sehemu ya msingi wa maendeleo ya sekta hiyo.
Amesema mchango huo umeiwezesha Tanzania kuweka misingi imara ya elimu jumuishi, ambapo wanawake na wanaume wanapata nafasi sawa za kujifunza, kufundisha na kuongoza.
“TESP umeacha alama ya kudumu katika kujenga mfumo wa elimu unaozingatia usawa wa kijinsia. Huu ni mwanzo wa safari ya kuhakikisha elimu inakuwa jumuishi zaidi nchini,” alihitimisha Prof. Nombo.






