HAKUNA ZUIO LA KUANZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA LNG – DKT. MWIGULU

Serikali yatenga sh. bilioni 280 kama dhamana kwa uwekezaji kwa vijana

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema hakuna zuio la kisheria wala la kikanuni linalosababisha kutokuanza utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) wenye thamani shilingi trilioni 100 bali Serikali inaendelea na majadiliano na wawekezaji ili kuhakikisha inalinda maslahi ya Taifa.

“Kinachofanyika ni masuala ya majadiliano na kwa kutambua ukubwa wa mradi huo na nchi yetu haijawahi kuingia kwenye uwekezaji mkubwa kama huo na ili kuweza kuitendea haki nchi yetu na rasilimali zake tukaona ni vema Serikali ikawa makini katika kila kipengele ili kuweza kulinda maslahi mapana ya nchi.”

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Aprili 9, 2026 wakati akijibu swali la Arif Premji, Mbunge wa Mtwara Vijijini katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua ni zuio lipi la kisheria au la kisera linalosababisha kutokutekelezwa kwa mradi huo ambao ni kipaumbele cha Taifa ulioanza mwaka 2014.

Waziri Mkuu amesema majadiliano yanaendelea na yako kwenye hatua nzuri na ni vipengele vichache vinaendelea kukamilishwa ili kuweza kuanza utekelezaji, ambavyo ni pamoja na uwepo wa asilimia tatu ama zaidi ya gesi inayozalishwa itumike nchini kwani awali ilikuwa iende nje baada ya kufanyika uwekezaji. “Nchi iliona lazima kuwe na gesi itakayotumika nchini.”

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kipengele kingine ni ulazima wa uwepo wa ushiriki wa makampuni ya wazawa katika utekelezaji wa mradi huo ili kujenga uchumi ulio imara. “Mara zote Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akielekeza ili tujenge uchumi ulio imara lazima tuyajengee uwezo makampuni ya wazawa”.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imefungua dirisha  la kutoa dhamana kwa vijana wanaokosa dhamana litakaloanza mwaka huu ambapo tayari kupitia Benku Kuu ya Tanzania (BoT) imetenga shilingi bilioni 280.

Pia, amesema yamefunguliwa madirisha ambayo vijana wanaweza kupata fursa likiwemo dirisha la kuwaunganisha katika masuala ya viwanda, masoko na taasisi za kifedha jambo ambalo lilikuwa likiwakwamisha vijana wengi.

Amesema Serikali inaendelea utaratibu wa kuandaa mazingira bora yatakayowawezesha vijana kupata vijana ajira ndani ya sekta ya umma na kwa wingi katika sekta binafsi na tayari imeshapitisha sheria ya uwekezaji ambapo wanaweza kunufaika na vivutio wanavyovipata wawekezaji wakubwa ikiwemo kupata ardhi, mapunguzo kwenye kodi, ushuru pamoja na tozo mbalimbali.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Timida Fyandomo aliyetaka kujua mkakati wa Serikali katika kuwawezesha vijana kuwekeza kwa kuwaunganisha na wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kuweza kukuza wigo wa ajira.