JKCI yaanzisha maabara ya kisasa inayotumia AI na roboti

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha maabara ya kisasa yenye teknolojia ya Akili Unde (AI) na mfumo wa kiroboti wa kuchakata sampuli, ambayo ni kubwa zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki na Jangwa la Sahara.

Maabara hiyo mpya imetajwa kuwezesha uchambuzi wa vipimo kwa usahihi, kupunguza makosa ya kibinadamu na kugundua magonjwa hata katika hatua za awali.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Aprili 9, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa mwaka 2025/2026.

Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Afya, kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na haraka.

Baadhi ya waandishi wa habari wakiuliza maswali wakati wa mkutano wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, JKCI uliofanyika Aprili 9, 2026, kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

“Maabara hii ina mfumo wa kisasa unaoweza kuchambua sampuli kwa usahihi mkubwa, kupunguza nafasi ya makosa ya kibinadamu, na kugundua magonjwa hata katika hatua zake za awali,” amesema.

Amesema maabara mpya imeongeza ufanisi kwa kupunguza muda wa kusubiri matokeo ya vipimo kutoka saa tatu hadi saa moja pekee. Aidha, inawezesha uchakataji wa idadi kubwa ya sampuli kwa muda mfupi, jambo linalosaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali.

“Robotic Lab ya JKCI inafanya taasisi hii kuwa kituo cha ubora cha uchunguzi wa maabara ya magonjwa mbalimbali, hasa ya moyo. JKCI imekuwa kitovu cha ubora kwa ukanda mzima wa SADC na Afrika Mashariki, ikichochea utafiti na maendeleo ya matibabu,” amesema.

Aidha, amesema maabara hiyo hutumika kama darasa hai kwa wataalamu wa afya wa ndani, kuwapatia maarifa mapya na ushauri wa kitaalamu katika uchunguzi wa kisayansi.

Hii ni hatua kubwa inayothibitisha kuwa Serikali inajitahidi kuboresha huduma za afya nchini, kuhakikisha wagonjwa wanapata matokeo ya haraka na sahihi, na kuchangia maendeleo ya matibabu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika matumizi ya teknolojia kwenye utoaji huduma, Dk Kisenge amesema wameendelea kuboresha matibabu kwa kutumia teknolojia za kisasa, ikiwemo mfumo wa uangalizi wa wagonjwa unaotumia akili bandia unaojulikana kama Dozee.

Teknolojia hiyo, iliyoanzishwa mwaka 2024 kwa mara ya kwanza Afrika, inamwezesha daktari kufuatilia hali ya mgonjwa akiwa hata nje ya hospitali. Kupitia kifaa maalumu kinachowekwa chini ya godoro, madaktari hupata taarifa muhimu kama mapigo ya moyo, upumuaji na presha ya mgonjwa kwa wakati halisi.

“Wagonjwa zaidi ya 100 tayari wamenufaika na huduma hii, huku ikitarajiwa kuongeza ufanisi wa wataalamu wachache waliopo kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi nchini,” amesema.

Mbali na hilo, taasisi hiyo ilizindua mfumo wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao mwaka 2025, ambao hadi sasa umetumiwa na wagonjwa zaidi ya 71,000, hatua iliyopunguza muda wa kusubiri huduma hospitalini.

Aidha, mfumo wa usajili wa ndugu wa wagonjwa waliolazwa umeanzishwa ili kurahisisha utaratibu wa utembeleaji na kuimarisha usalama wodini.

“JKCI sasa inalenga kuimarisha huduma za tiba mtandao ili kupanua zaidi upatikanaji wa huduma za moyo nchini,” amesema.

Aidha amesema JKCI imeendelea kuweka historia katika huduma za matibabu ya moyo kwa kufanya zaidi ya upasuaji 800 wa kufungua kifua kwa mwaka pamoja na kuanza kufanya upasuaji mgumu ambao haujawahi kufanyika katika baadhi ya nchi za Afrika.

Dk Kisenge, amesema taasisi hiyo sasa inafanya taratibu tata za matibabu (complex procedures) ikiwemo Tavi, pamoja na upasuaji wa watoto kama Ozaki na Truncus, ambao kwa Afrika nzima ulifanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania kupitia JKCI.

Amesema mafanikio hayo yamepunguza ulazima wa Watanzania kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu ya moyo, na hivyo kuokoa gharama kubwa huku yakiiweka Tanzania katika ramani ya utalii wa matibabu barani Afrika.

Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Dodoma wakifuatilia mkutano wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, JKCI uliofanyika Aprili 9, 2026, kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

“Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, JKCI imepanua huduma zake kwa kufungua matawi sita katika maeneo ya Tazara, Kawe, Oysterbay, Kariakoo, Chato na Arusha, hatua iliyosaidia kuongeza idadi ya wagonjwa kutoka wastani wa 400 kwa siku mwaka 2022 hadi zaidi ya 1,100 mwaka 2025,” amesema Dk Kisenge.

Aidha, amesema kupitia ufadhili wa Serikali, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, zaidi ya watoto 300 wamefanyiwa upasuaji wa moyo bila malipo, huku zaidi ya watoto 30 wakifanyiwa upasuaji mkubwa wa kufungua kifua.

Dk Kisenge amesema taasisi hiyo imeanza mchakato wa upandikizaji wa moyo, ikilenga kuanza huduma hiyo ifikapo mwaka 2030 na kuendelea kuvutia wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali na sasa inalenga kufungua tawi nje ya nchi, hatua itakayoimarisha zaidi nafasi ya Tanzania kama kitovu cha utalii wa matibabu Afrika.