Mbeya. Safari ya matumaini mapya kwa kijana Mpoki Abraham (32), mwenye ulemavu wa viungo, imegeuka kuwa chanzo cha furaha, tabasamu na matumaini mapya, si kwake tu bali pia na kwa familia yake.
Abraham, mkazi wa Mtaa wa Bombambili, Kata ya Mwakibete, jijini Mbeya, aliyezaliwa na ulemavu wa kudumu unaomfanya akose mikono na miguu, amekuwa akiendesha maisha yake kwa kujivuta kwa kutumia makalio kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Hali hiyo, ilimfanya aishi maisha ya unyonge, upweke na kukosa kujiamini, licha ya jitihada zake za kujishughulisha na ujasiriamali mdogo wa kuuza bidhaa za mahitaji ya nyumbani karibu na anapoishi.
Alilazimika kukaa zaidi nyumbani au kibandani, akitegemea msaada wa wanafamilia, hasa mama yake, ili afike maeneo mbalimbali au kutekeleza mahitaji yake ya msingi.
Licha ya changamoto hizo, hakukata tamaa, bali aliendelea kupambana kadiri ya uwezo wake.
Mabadiliko makubwa katika maisha yake yalianza Machi 25, 2026, baada ya kuibuliwa kupitia kampeni ya “Bendera ya Upendo” inayoendeshwa na Taasisi ya Tulia Trust. Kupitia kampeni hiyo, inayolenga kuwafikia watu wenye mahitaji maalumu katika jamii, Abraham alitambuliwa kama mmoja wa wahitaji waliostahili kusaidiwa.
Hatua hiyo ilizaa matunda Aprili 8, 2026, alipokabidhiwa kiti mwendo (wheelchair), msaada ambao umeleta mageuzi makubwa katika maisha yake.
Sambamba na hilo, alikabidhiwa fedha taslimu Sh500,000 kwa ajili ya kuimarisha mtaji wa biashara yake ndogo anayoiendesha.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Abraham anasema,”nilikuwa naumia sana kuona nimekuwa mtu wa kukaa sehemu moja, wakati mwingine nikisaidiwa na ndugu zangu, hasa mama yangu. Ilikuwa ni hali ngumu sana kwangu kisaikolojia na kimwili.”
Anasema kupata kiti mwendo kumefungua ukurasa mpya wa maisha yake, akieleza kuwa sasa ana uhuru wa kusogea kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila kutegemea msaada mkubwa kama ilivyokuwa awali.
“Hii ni historia mpya kwangu. Kwa miaka mingi nilitamani kuwa kama wengine, kuweza kutoka nyumbani na kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Sasa naona ndoto hiyo inaanza kutimia,” anaeleza kwa furaha.
Abraham anasema msaada huo utamwezesha kupanua wigo wa biashara yake, kwani ataweza kufuatilia bidhaa mwenyewe sokoni na kuongeza ufanisi katika shughuli zake za ujasiriamali.
“Nitaweza kwenda kuchukua bidhaa mwenyewe, kukutana na wateja na hata kufikiria kupanua biashara yangu. Hii itanisaidia kujikwamua kiuchumi na kupunguza utegemezi kwa familia,” anaeleza.
Pamoja na mafanikio hayo, Abraham anaweka wazi ndoto yake ya muda mrefu ya kuwa mfanyabiashara mkubwa. Hata hivyo, anaeleza kuwa changamoto ya mtaji bado ni kikwazo kinachohitaji kuangaliwa zaidi.
“Nina ndoto ya kuwa mfanyabiashara mkubwa siku zijazo. Naomba wadau waendelee kunisaidia ili niongeza mtaji wangu. Natamani kufikia hatua ambayo nami nitasaidia wengine wenye mahitaji kama mimi,” anasema.
Kwa upande wa familia, furaha ilikuwa dhahiri. Ndugu yake, Penance Reuben (21), anasema msaada huo umekuwa ni faraja kubwa kwao, kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakibeba jukumu la kumsaidia Abraham katika shughuli zake za kila siku.
“Tumekuwa tukijitahidi kumsaidia kwa kila hali. Kupatikana kwa kiti mwendo kutapunguza mzigo mkubwa tuliokuwa nao, na pia kutampa uhuru zaidi wa kufanya mambo yake binafsi,” anasema Penance.
Anaogeza kuwa sasa Abraham ataweza kujitegemea zaidi katika biashara yake, ikiwemo kupanga na kuuza bidhaa, jambo ambalo awali lilitegemea msaada wa familia.
Kwa upande wa Taasisi ya Tulia Trust, Mratibu wa kampeni ya “Bendera ya Upendo,” Daudi Mwangosi, anasema Abraham ni miongoni mwa walengwa waliobainika wakati wa mbio hizo za hisani zinazolenga kusaidia watu wenye mahitaji maalumu.
Anasema kupitia kampeni hiyo, wamelibaini watu wengi wenye changamoto mbalimbali, wakiwemo wanaohitaji viti mwendo na wengine wanaohitaji huduma za matibabu.
“Kampeni hii imetuwezesha kufika kwa watu wengi wenye mahitaji. Wapo wanaohitaji vifaa saidizi kama viti mwendo, na wengine wanahitaji matibabu. Tunapanga kuwafikia hatua kwa hatua kulingana na mahitaji yao,” anasema Mwangosi.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bombambili, Said George, anasema mwanzo haikuwa rahisi kwa Abraham kukubali msaada huo kutokana na uzoefu mbaya wa watu waliowahi kumlaghai hapo awali.
“Awali alikuwa na hofu kutokana na baadhi ya watu kumlaghai, lakini tulijitahidi kumshawishi na hatimaye akakubali kupokea msaada huu. Ni jambo la faraja kuona sasa anapata msaada stahiki,” anasema George.
Anaongeza kuwa ujio wa kampeni hiyo katika eneo lao umekuwa na manufaa makubwa, na kuwataka wadau wengine kujitokeza kusaidia watu wenye mahitaji maalumu katika jamii.