Mwanamke mwajiriwa sekta binafsi, alianza kukatwa fedha kutoka kwenye mshahara wake ili kuchangia bima. Baada ya miaka mitatu ya makato, alipata maumivu ya kifua. Alikwenda hospitali, daktari baada ya kumsikiliza, alimwandikia kipimo cha ufanyaji kazi wa moyo, ambacho kitaalamu huitwa Electrocardiogram (ECG).
Hata hivyo, mwanamke huyo aliambiwa atoe fedha taslimu Sh30,000 ili apimwe ECG, maana bima yake haikuwa ikiwezesha kipimo hicho. Hakuwa na kiasi hicho cha fedha. Alilazimika kurejea nyumbani bila kupimwa. Kila mwezi hukatwa Sh100,000 kwa ajili ya bima. Jumla ni Sh1.2 milioni kwa mwaka. Miaka mitatu ni Sh3.6 milioni.
Mtu huyu ambaye miaka mitatu alikatwa jumla ya Sh3.6 milioni bila kuugua, anajisikiajia anapoambiwa pamoja na michango yake yote hiyo, bado hawezi kuhudumiwa kipimo kinachogharimu Sh30,000? Hili ndilo eneo mahsusi linalohitaji tafakuri. Je, mwananchi huyo hajafanyiwa ujambazi wa fedha zake kweli?
Bima ni ulinzi. Mwanachama huupata ulinzi huo kwa kulipia ada. Kila mwezi kampuni ya bima inachukua fedha za mteja kwa ahadi kwamba akiumwa itahakikisha anapata huduma za afya. Siku akiumwa, anaambiwa huduma fulani hatapata kwa sababu kampuni ya bima ambayo huchukua fedha zake haiwezeshi.
Limekuwa tatizo kubwa kwa wenye bima za afya. Mteja anaambiwa dawa fulani haiwezeshwi na bima yake, kwa hiyo anapaswa kuilipia. Mbaya zaidi, dawa ambazo bima inakataa ndizo ambazo madaktari wanazipendekeza. Hii ina maana gani? Kampuni zinachukua fedha, lakini wakati wa kutoa huduma vikwazo vinakuwa vingi.
Maofisa wa kampuni ya bima watakuja na ahadi za pepo kwa wafanyakazi endapo wataugua. Mgonjwa akiwa kwenye chumba cha daktari, ndiyo anakutana na vikwazo. Kipimo fulani hataweza kufanyiwa, maana hakiwezeshwi. Dawa hii ni bora lakini bima yake haitagharamia. Wenye akiba hutoa fedha, wasio na chochote ambao ndiyo wengi, huishia kujibana kwenye huduma zinazowezeshwa na bima, matokeo yake hawaponi.
Yupo mtu alikwenda hospitali akiwa na dalili za bawasiri. Daktari akagundua kuwa dawa ya suppository haipo kwenye bima yake. Daktari alimwambia suppositories zingekuwa bora kwa matibabu yake. Hakuwa na fedha, ikabidi apokee dawa iliyokuwepo, ambayo daktari alisema haikuwa na uwezo mzuri. Matokeo yake, alitumia dawa yote ikaisha bila kupata nafuu. Anaendelea kuumwa.
Aliporudi kutazama kumbukumbu zake, ugonjwa huo aliwahi kuupata na alitumia dawa alizonunua duka la dawa kwa fedha taslimu Sh18,000. Dawa hiyo ilikuwa suppository. Unajiuliza, mtu anakatwa karibu Sh1.5 milioni kwa mwaka, inakuwaje anakataliwa dawa inayogharimu chini ya Sh20,000? Hatuoni kama kuna ujambazi wa fedha za watu unaotekelezwa kwa njia halali?
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) ni taasisi ya serikali yenye jukumu la kudhibiti, kusimamia, na kuendeleza sekta ya bima nchini. Tira ilianzishwa kupitia Sheria ya Bima namba 10 ya mwaka 2009. Maumivu haya ya wananchi ambao ni wateja wa bima, yalipaswa kufanyiwa kazi na Tira. Mamlaka ya serikali inaruhusu vipi Mtanzania akatwe fedha za bima na asinufaike ipasavyo na fedha zake?
Kitu kimoja ni uhakika; bima imekuwa biashara kama kununua na kuuza, yaani trading. Kampuni za bima zinatafuta faida kupitia mteja hadi mteja. Bima ilimaanishwa huduma na faida haiwi kwa mtu na mtu, bali kwa uwiano wa wateja. Wanachangia wengi, wachache wanapata matatizo yenye kuhitaji bima ifanye kazi. Uwiano baina ya wengi wanaochangia dhidi ya wachache ambao huhitaji fidia ya bima, ndipo kampuni hunufaika.
Kitendo cha kumbana mgonjwa asipewe dawa bora, asipate kipimo kinachostahili, ni mchezo wa kuanza kuipigia hesabu pesa ya kila mwanachama. Kila ada ya mwanachama lazima iwe na faida kwa kampuni ya bima. Hiyo ni trading. Tira lazima walione hilo. Bunge lilitunga Sheria ya Bima na kuhakikisha mamlaka hiyo inaanzishwa kwa lengo la kuhakikisha kampuni za bima hazijipangii na kuendesha mambo yao zinavyotaka. Sharti masilahi ya wateja ambao ni wananchi yazingatiwe.
Inafahamika kuwa upo udanganyifu mkubwa ambao hufanywa dhidi ya kampuni za bima. Ni mnyororo wa uhalifu unaoungwa baina ya wateja na wafanyakazi. Hii siyo Tanzania tu, bali ulimwenguni kote. Ukosefu wa uadilifu ni janga. Wateja na wafanyakazi wanashirikiana kuhujumu kampuni za bima. Watu wanaharibu mali zao na kulipwa fidia kubwa na bima.
Kipo kisa kilitokea London, UK. Mtu mwenye asili ya Afrika Mashariki alijitengenezea ajali, halafu akajifanya amejeruhiwa vibaya. Kampuni ya bima ilimhudumia kwa muda mfupi, halafu ikazungumza naye ili impe fidia ya jumla aendelee kujitibu mwenyewe. Baada ya makubaliano, yule mtu alilipwa pauni za UK 50,000. Ni tukio la mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Michezo ya kuchoma moto magari, nyumba na mali nyingine ipo. Ukosefu wa uadilifu ni janga. Wakati huohuo jiulize kuhusu mtu ambaye analipa bima ndogo (third-party insurance), ambayo ni lazima. Akipata ajali bado anatumia fedha zake kumlipa aliyemsababishia ajali. Tena, askari wa usalama barabarani wanasimamia makubaliano, mwenye makosa analipa, kisha, askari naye anaomba na kupokea kamisheni.
Wengine wanaharibiwa magari yao na wanalazimika kutengeneza wenyewe. Sababu ni usumbufu. Watu wanaona kufuatilia fidia bima ni mateso. Kwa nini? Jinsi ilivyo haraka kupokea pesa kwa nini uharaka huohuo usiwepo wakati wa kuwafidia wateja? Matokeo yake, third-party insurance imekuwa ikichukuliwa na watu kama malipo ya lazima ili kutogombana na askari wa usalama barabarani, lakini haziwasaidii kitu wanaolipa.
Unamgonga mtu na gari, anajeruhiwa, unatakiwa kumtibu, wakati hiyo ni kazi ya bima. Askari wa usalama barabarani wanaodai bima kila uchwao utadhani wao ni maofisa wa bima, hawawasaidii watu kutambua nini haki yao. Yupo rafiki yangu ameweka mgomo wa kukata bima, baada ya kuona hazimsaidii. Alikata bima kubwa (comprehensive insurance), gari yake ikapata ajali. Alisota kupata fidia mpaka akasusa. Amefanya mgomo.
Profesa wa bima, Solomon Huebner, ambaye alifundisha Shule ya Biashara, Chuo Kikuu cha Pennsylvania, Marekani, alipata kusema ili bima iwe halali inatakiwa pande zote watu wawe na elimu ya kutosha na waadilifu. Hapa Tanzania bima zinalazimishwa ila elimu haitolewi. Uadilifu hakuna. Wananchi wanaibiwa. Inakuwa sawa na ujambazi uliohalalishwa.
