Dar es Salaam. Vijana sita wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni, kujibu shtaka moja la kutoa taarifa za uongo kuwa wameibiwa sehemu zao za siri (uume) wakati wakijua ni uongo.
Washtakiwa hao ni Price Pius (26) mkazi wa Tabata; Juma Abeid(26) na Nurdin Nondwa (23) wote ni fundi gari na wakazi wa Tabata.
Wengine ni dereva, Yusuph Rashid (36) mkazi Bunju; mfanyabiashara Sita Issa (24) mkazi wa Mabino, pamoja na Mandieta Zongera(25) mfanyabiashara na mkazi wa Manzese.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutoa taarifa za uongo, kinyume na kifungu 122 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi, Aprili 9, 2026 na kusomewa kesi zao kwa mahakimu wawili tofauti.
Katika kesi ya kwanza hadi ya tatu inayomkabili mshtakiwa Pius, Abeid, Nondwa na Rashidi, wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Salome Mdese.
Kesi ya nne na ya tano inayomkabili mshtakiwa Issa na Zongela, wao wamesomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Olivia Towilo.
Akiwasomea mashtaka yao, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Abeid Swaiba, amedai mbele ya Hakimu Salome Mdesa, kuwa mshtakiwa Pius anadaiwa kutenda kosa lake Aprili 7, 2026 eneo la Victoria, Kindononi B.
Mshtakiwa Sita Issa(kushoto) na Prince Pius( mwenye kanzu) wakijificha nyuso zao, baada ya kusomewa mashtaka ya kutoa taarifa za uongo kuhusiana na sehemu zao za siri kutoweka.
Inadaiwa siku hiyo, saa 10:00 jioni, kwa makusudi mshtakiwa alitoa taarifa za uongo kwa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Omary Hamad, kuwa ameibiwa sehemu zake za siri (uume) wakati akijua kuwa sio kweli.
Shtaka la pili, linamkabili Abeid na Nondwa ambapo wanadaiwa kutenda kosa lao Aprili 5, 2026 eneo la Mburahati Kituo cha Polisi.
Washtakiwa hao wanadaiwa siku hiyo, saa 7:15 mchana wakiwa kituoni hapo, kwa makusudi walitoa taarifa za uongo kwa Mkaguzi wa Polisi Ismail Adam, kuwa wameibiwa sehemu zao za siri wakati wakijua ni uongo.
Swaibu alidai katika shtaka la tatu, mshtakiwa Rashid yeye anadaiwa kutenda kosa lake Aprili 5, 2026 eneo la Magomeni Kituo cha Polisi.
Inadaiwa siku hiyo saa 11:00 jioni akiwa katika kituo hicho, kwa makusudi alitoa taarifa za uongo kwa Stafu Sajenti mwenye namba WP 4580 Kawale, kuwa ameibiwa sehemu zake za siri, wakati akijua ni uongo.
Shtaka la nne, limesomwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bahati Manyama, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Olivia Towilo.
Manyama alidai mshtakiwa Issa anadaiwa kutenda kosa lake, Aprili 5, 2026 katika kituo cha Polisi Magomeni, ambapo alitoa taarifa za uongo kwa askari polisi Stafu Sajenti mwenye namba WP 4580 Kawale, kuwa ameibiwa sehemu zake za siri, wakati akijua ni uongo.
Manyama aliendelea kuieleza mahakama hiyo, mshtakiwa Zongera anadaiwa Aprili 5, 2026 katika Kituo cha Polisi Mburahati, kwa makusudi alitoa taarifa za uongo kwa Mkaguzi wa Polisi, Frank Nkusa kuwa sehemu zake za siri hazipo, wakati akijua ni uongo.
Baadhi ya washtakiwa wakiwa katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni, Dar es Salaam baada ya kusomewa mashtaka ya kutoa taarifa za uongo kuhusiana na sehemu zao za siri kutoweka.
Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao walikana kutenda.
Hakimu Mdesa na Towilo walitoa masharti matano ya dhamana dhidi ya washtakiwa hao ambayo ni; kila mshtakiwa anatakiwa awe na mdhamini moja atakayesaini fungu la dhamana la Sh1 milioni.
Pili, mdhamini huyo anatakiwa awe mkazi wa Jiji la Dar es Salaam na awe na barua kutoka serikali za mitaa pamoja kitambulisho cha Nida.
Hata hivyo, washtakiwa hao wamefanikiwa kutimiza masharti ya dhamana.
Mshtakiwa Pius, Abeid, Nondwa na Rashid kesi zao zimeahirishwa hadi Aprili 15, 2026 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi.
Wakati mshtakiwa Issa, kesi yake imeahirishwa hadi Mei 4, 2026 na mshtakiwa Zongea kesi yake imeahirishwa hadi Mei 5, 2026 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi.
