LATRA Yafafanua Vigezo Vinavyozingatiwa Katika Upangaji wa Nauli Nchini

Bakari Mahundu
April 9, 2026
0 Comments

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesema kuwa upangaji wa nauli hauzingatii bei ya mafuta pekee, bali huzingatia vigezo mbalimbali vinavyoathiri gharama za uendeshaji wa huduma za usafiri wa umma.

Mamlaka hiyo imeeleza kuwa vigezo hivyo ni pamoja na bei ya vyombo vya moto kwa wakati husika, gharama za vipuri, mishahara ya wafanyakazi pamoja na rejesho la uwekezaji kwa watoa huduma.

Aidha, imesema mchanganyiko wa vigezo hivyo husaidia kupata nauli halisi inayoakisi hali ya soko na kuhakikisha uendelevu wa sekta ya usafiri wa umma.

LATRA imeongeza kuwa mabadiliko ya bei ya mafuta ni sehemu tu ya mambo yanayochangia mapitio ya nauli na si kigezo pekee cha ongezeko au punguzo la nauli.

Akizungumza katika mkutano wa wadau, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Dkt. Habibu Suluo, amesema kanuni za tozo za mwaka 2020 zinaelekeza utaratibu wa mapitio ya nauli.

Amesema mtoa huduma anaweza kuwasilisha mapendekezo ya mapitio ya nauli au mamlaka kuanzisha mchakato huo pale inapobidi, ili kuhakikisha nauli zinaakisi gharama halisi za uendeshaji.

Kauli hiyo imetolewa katika mkutano wa wadau wa usafiri wa umma uliofanyika Aprili 8, 2026 katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Awali, akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, Bw. Andrew Magombana aliwataka wadau kuwasilisha maoni yao wakieleza namna mabadiliko ya bei ya mafuta yanavyoathiri shughuli zao za biashara.