KATIKA misimu mitano ya Ligi Kuu Bara, wachezaji wa kimataifa ‘maproo’ wameonekana kutawala kuwa vinara wa asisti, huku mzawa Feisal Salum ‘Fei Toto’ akikataa unyonge.
Katika misimu hiyo kuanzia 2020-2021, jina la kiungo wa Simba, Clatous Chama raia wa Zambia, limeibuka mara mbili huku akiwa na rekodi ya asisti nyingi ambazo ni 15 msimu wa 2020-2021 na 14 msimu wa 2022-2023.
Katika msimu wa 2021-2022, Pape Ousmane Sakho aliyekuwa Simba na sasa Raja Club Athletic ya Morocco, alimaliza kinara wa asisti akiwa nazo sita, huku Kipre Junior raia wa Ivory Coast akiwa Azam msimu wa 2023-2024 akamaliza kinara na asisti tisa. Kipre kwa sasa ni nyota wa MC Algiers ya Algeria.
Msimu uliopita 2024-2025, Fei Toto akiwa Azam, akawa kinara wa asisti akifikisha 13, huku pia msimu huu 2025-2026 pia ni kinara akipiga asisti tano sawa na Mkongomani, Elie Mpanzu wa Simba.
Nahodha wa zamani wa Simba, Mussa Hassan Mgosi, alisema kinachoonekana hapo ni muendelezo wa viwango vya wachezaji, lakini pia inategemeana na mahitaji ya timu kwa mchezaji, akimtolea mfano Fei Toto msimu wa 2023-2024 alipomaliza nafasi ya pili kwa kufunga mabao 19, nyuma ya aliyekuwa nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki aliyekuwa na mabao 21.
“Msimu huo (2023-2024) Fei Toto alimaliza na asisti saba, unaweza ukaona timu ilikuwa inamtegemea zaidi kufunga japokuwa aliwatengenezea wengine mabao, lakini ninachokiona ni muendelezo wa viwango, ingawa wakati mwingine kocha anaweza akambadilisha mchezaji akacheza nafasi tofauti,” alisema.
Nyota wa zamani wa Singida United na Yanga, Kipanya Malapa, alisema: “Ukiondoa Fei Toto ambaye amekuwa katika kiwango kizuri katika misimu mingi, ila wanachokifanya wageni wanapambana kwani wanajua kilichowaleta Tanzania ni kazi, ukiona kuna mgeni hajitumi basi anakuwa hajajitambua.”
Aliongeza: “Lakini ukiangalia nafasi za hao wanaoongoza kwa asisti ni eneo lao, ingawa wanafunga lakini kazi yao kubwa ni kuwatengenezea wengine nafasi ya kufunga.”
Kocha wa zamani wa Stand United, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema: “Kuna wakati mchezaji anaweza akabadilishwa majukumu, lakini asilimia kubwa viungo wanatengeneza mabao.”