Mafuta bado pasua kichwa, Serikali na Bunge wakutana bungeni

Dodoma. Sakata la kupanda kwa mafuta limeendelea kugonga vichwa vya wadau mbalimbali ndani na nje ya Bunge licha ya tumaini linaloanza kuonekana.

Kwa kauli za mtaani, mjadala wa mafuta kwa sasa ndiyo mpango mzima kwani baadhi ya nchi kunaelezwa hakuna mafuta na vyombo vya usafiri vimesimama, huku wengine wakianza kufanyia kazi majumbani.

Bei ya mafuta imepanda nchini na duniani kwa ujumla, baada ya kuzuka kwa vita Mashariki ya Kati, vinavyohusisha mataifa ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, vilivyoathiri mnyororo wa ugavi wa nishati hiyo.

Kutokana na vita hivyo, Iran ilifunga mlango wa Bahari wa Hormuz, unaotumika kupitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yanayosafirishwa kwenye mataifa mbalimbali duniani.

Licha ya yote hayo, kuna matumaini ya kushuka kwa bei ya nishati hiyo baada ya ahadi ya kufunguliwa kwa mlango wa Hormuz, kunakosababishwa na makubaliano ya kusitishwa mapigano kwa wiki mbili.

Jana Jumatano, Aprili 8, 2026, Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, alitangaza mkakati wa kubana matumizi akianzia misafara yake.

Mjadala huu wa mafuta unaingia siku ya tisa tangu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei mpya za mafuta kuanzia Aprili 1, 2026.

Aprili 1, 2026, Spika wa Bunge, Mussa Zungu aliagiza Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kukutana na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi kupata taarifa ya nini kimetokea.

Spika Zungu alitoa maagizo hayo dakika chache kupita tangu Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kusema Serikali itaketi ili kuangalia uwezekano wa kuleta unafuu kwa Watanzania.

Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka 2026/27, Dk Mwigulu alisema: “Tumeona bei zimeshaanza kupanda, tutakaa ndani ya Serikali kuhakikisha tunakabiliana nalo vipi suala hili ili wananchi waendelee kupata mafuta kwa bei nzuri na kudhibiti kupanda kwa gharama za maisha.”

Jana Jumatano, Aprili 8, 2026, Kamati ya Nishati na Madini chini ya Uenyekiti wa Subira Mgalu ilikutana na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa rasmi ya Serikali kuhusu hali ya upatikanaji na bei za bidhaa za mafuta nchini.

Kikao hicho, kilihudhuriwa pia na Watendaji kutoka Wizara ya Fedha wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wake, Ndugu Elijah Mwandumbya.

Asububi ya leo Alhamisi, Aprili 9, 2026 baada ya maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Spika Zungu aliliambia Bunge kuwa anakabidhi kiti kwa Mwenyekiti Najma Giga kwani yeye anakwenda kwenye kikao.

“Waheshimiwa wabunge, naomba nimuachie kiti Mwenyekiti Najma Giga kwani mimi nakwenda kwenye kikao muda huu,” amesema Zungu.

Baada ya kuondoka kwenye kiti, Zungu alikwenda moja kwa moja eneo la Ofisi ndogo ya Spika iliyopo ndani ya ukumbi wa Bunge.

Wengine walioingia ndani ya ukumbi huo ni Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, Katibu wa Bunge, Baraka Leonard, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati, Subira Mgalu na watu wachache walionekana kwenda huko.

Kikao hicho kilidumu kwa muda wa dakika 50 ndipo viongozi hao wakatoka akianza Subira Mgalu kisha Spika Zungu, Katibu wa Bunge na Waziri Ndejembi walitoka pamoja na hawakuingia ndani ya ukumbi wa Bunge.

Mwananchi limemtafuta Mgalu kujua kikao cha jana na kile cha mapema leo asubuhi nini kinaendelea ambapo amejibu kuwa, “Taarifa tumeiwasilisha kwa Spika, tunasubiri aipangie ratiba.”

Hata hivyo, Mgalu ambaye ni Mbunge wa Bagamoyo (CCM) aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini amesema vikao hivyo bado vinaendelea kikiwemo kitakachofanyika mchana wa leo.