Mbeya. Familia ya Ordinary Sanga iliyopo jijini Mbeya, imeiomba Serikali kuingilia kati mgogoro wa mirathi unaoendelea kufuatia mali za urithi zilizoachwa kudaiwa kumilikiwa na mtu mmoja huku nyingine zikielezwa kuuzwa kinyemela.
Inadaiwa kuwa Sanga alifariki tangu Aprili 1997 huku akiacha watoto saba aliozaa kwa wake watano, ambapo aliacha mali zaidi ya 40 zinazohamishika ambapo zimeonekana kutosimamiwa vema kama alivyoelekeza kwenye wosia wake.
Akizungumza na Mwananchi, Josepha Sanga ambaye ni mke wa kwanza kwa marehemu, amesema anasikitishwa na kitendo cha mke mwenza, Juliana Luvanda ambaye amejimilikisha mali na kuziacha familia nyingine zikitaabika.
Josepha Sanga mke wa kwanza na mjane wa marehemu Ordinary Sanga.
Amesema licha ya vyombo vyote vya kisheria kutoa maelekezo ya mali zote kuwekwa wazi ili kila mwenye haki apate jasho la mpendwa wao, lakini imekuwa tofauti na hali ambayo inaleta mgogoro mkubwa.
“Serikali tunaiomba iingilie kati mgogoro huu na haki iweze kutendeka, haiwezekani mali nilizochuma na mume wangu atokee mtu mwishoni aje kujimilikisha, mahakama zilishaelekeza lakini yeye kafoji nyaraka na kuwapa watoto wake tu.”
“Mimi ndiye mke wa kwanza tangu 1959, yeye Juliana aliolewa 1991, amefoji hati ya jengo la kibiashara pale Uyole anafaidika tu, watoto wengine wanahangaika, Serikali itusaidie tumalize mgogoro huu” amesema Josepha.
Kwa upande wake mtoto wa Josepha, Eliam Sanga amesema enzi za uhai wa baba yake alikuwa akishirikiana naye kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na baada ya kifo chake, alikabidhiwa kuwa msimamizi wa mirathi kupitia kiapo cha mama yake mahakamani.
“Kwa sasa mzigo unaegemea kwangu napata taabu kwa nini watoto wote wanateseka ilihali kuna mali za baba yetu, ndio maana napambania familia yote wakiwamo wa Juliana wapate ila ile nyumba igawanywe kwa kuwa ina milango 40.”
Juliana Luvanda mmoja wa wajane wa marehemu Ordinary Sanga akionesha baadhi ya nyaraka juu ya uhalali wa umiliki wa moja ya nyumba ya biashara iliyopo Uyole jijini Mbeya.
“Kama siyo kugawanywa zile fremu, basi tuuze ili kila mmoja apate japo kidogo kwa kila mmoja, taarifa tumeipeleka ofisi ya Mkuu wa Mkoa na tunajipanga kwenda Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), naumia kuona watoto wengine wanateseka huku wachache ndio wananufaika” amesema Eliam.
Kwa upande wake Elias Sanga, mtoto wa mke wa tatu, amesema mahakama ilielekeza familia kukaa na kumaliza changamoto hiyo kwa kila mmoja kunufaika na mali zilizoachwa, lakini Juliana (mke wa mwisho) amegomea nyumba hiyo.
“Mahakama ilielekeza mgogoro tuumalize kifamilia, kesi zikafutwa tukasainiana makubaliano, lakini imekuwa tofauti na uamuzi wa huyu Mama, tuliviamini vyombo vya sheria imekuwa tofauti, kwa nini sisi tuteseke wengine wanufaike” amehoji Elias.
Akizungumzia suala hilo, Juliana amesema yeye ndiye mwathirika mkubwa wa mali za marehemu mume wake, akieleza kuwa kwa sasa anaiomba Serikali iingilie kati ili kila mmoja apate haki yake.
Amesema enzi za uhai wa mume wake, alikuwa na mali nyingi zaidi ya 40 zinazohamishika, lakini mtu mmoja tu ndiye ameonekana kunufaika zaidi kwa kuwa ameuza kinyemela kila kitu na sasa wanageukia nyumba yake na watoto.
Muonekano wa jengo lenye vyumba vya biashara lililopo Uyole jijini Mbeya linalodaiwa kuleta mgogoro wa kifamilia juu ya mirathi ya Ordinary Sanga ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Barua zote za wosia ninazo, kila mali alielekeza usimamizi na muhusika wake, mume wangu alikuwa tajiri mwenye magari, silaha, viwanja, mashine, nyumba, misitu na vitu vingine kibao.”
“Lakini mwaka 2005, hii nyumba wanayoisemea waliiuza kwa mtu (jina tunalo), nikaingia kazini kulipa hiyo gharama nikaikomboa Sh17 milioni, nikapewa hati kwa mujibu wa makubaliano, nyaraka na risiti za malipo ninazo,” amesema na kuongeza:
“Kwanza tuliolewa wake wanne, wawili wakaondoka wakaacha watoto mmojammoja, tukabaki wawili wakitaka tugawane hii nyumba, naomba mali zote zilizoachwa na marehemu ziwepo tugawe vyote wote tupate,” amesema huku akiangua kilio.
Kwa upande wake mtoto wa Juliana, Furaha Sanga amesema familia hiyo imefanyiwa hujuma na baadhi ya ndugu zao, akieleza kuwa wosia wa baba yao alioacha hakuna chochote walichoambulia na nyumba wanayotolea macho alijenga mama yake.
“Ukiachana na hii nyumba wanayoitolea macho, hakuna kingine tulichoambulia, mali zote Eliam ameuza sasa wamebaki bila kitu wanaanza kutusumbua, kwa muda huu tunaanza kuwa na hofu na usalama wetu, Serikali itusaidie,” amesema Furaha.