Dodoma. Suala la uwajibikaji wa watumishi wa umma katika kushughulikia kero za wananchi na kusimamia utekelezaji wa maagizo ya viongozi wa kitaifa, leo limeelekezwa pia kwa mawaziri na naibu mawaziri, wakitakiwa kutoa majibu yenye utekelezaji wanapojibu hoja za wabunge bungeni.
Hatua hiyo imekuja kufuatia baadhi ya wabunge kueleza kutoridhishwa na majibu wanayopewa na mawaziri, wakidai kuwa mara nyingi hayatekelezeki na hivyo kuwawia vigumu kuyasimamia mbele ya wananchi wao.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo, amesema Serikali ina mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa maamuzi na maagizo yake, akiwahakikishia wabunge kuwa hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.
Amesema kila kauli au agizo linalotolewa na Serikali hupitia katika mfumo wa ufuatiliaji ili kuhakikisha linatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Hata hivyo, Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga, ameeleza kutoridhishwa na hali ilivyo sasa, akitaka kuwepo kwa uwajibikaji wa wazi kwa mawaziri wanaotoa majibu yasiyo na mwelekeo wa utekelezaji.
Sanga amesema baadhi ya majibu yanayotolewa bungeni ni ya bora liende, hali inayowalazimu wabunge kukumbana na changamoto wanaporejea kwa wananchi wao, ambao wanatarajia majibu yenye suluhisho la vitendo.
“Tunapozungumzia tathimini na upimaji wa matokeo ya utendaji serikalini, ni muhimu pia kuangalia upande wa mawaziri, kwani baadhi yao wanatoa majibu ambayo hayatoi suluhisho la moja kwa moja,” amesema Sanga.
Hoja hiyo ya uwajibikaji serikalini imetokana na swali lililoulizwa kwa Waziri Mkuu na Mbunge wa Monduli, Isack Capriano, kuhusu utaratibu wa ufuatiliaji wa ahadi na maagizo ya viongozi wanapofanya ziara.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Serikali tayari ina kitengo cha ufuatiliaji, lakini imejipanga kuanzisha mfumo mpya utakaoshuka hadi ngazi ya chini ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi.
Amefafanua kuwa mfumo huo utahusisha watumishi wa umma kujaza taarifa za wananchi wanaowahudumia, ikiwemo majina, namba za simu na namna walivyotatuliwa changamoto zao, badala ya kusubiri ziara za viongozi wakuu.
“Tunaanzisha mfumo wa ufuatiliaji kuanzia ngazi ya vijiji. Tutahitaji kujua kila kiongozi kwa mwezi amehudumia wananchi wangapi, kwa majina na mawasiliano yao, pamoja na hatua zilizochukuliwa. Hatutaki wananchi wawafuate viongozi wa juu, huduma zinapaswa kuwafikia walipo,” amesema Dk Nchemba.
Ameongeza kuwa mfumo huo utaambatana na tathmini ya utendaji kazi wa watumishi, ambapo vyeo vitatolewa kulingana na uwezo wa kuhudumia wananchi badala ya muda wa kukaa kazini.
Wakati huohuo, wabunge wameibana Serikali kuhusu hali ya miundombinu iliyoharibiwa na mvua kubwa pamoja na tabia ya kuanzisha miradi mipya huku ile ya zamani ikitelekezwa.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Tarimba Abbas, amesema hali ya barabara katika jimbo lake ni mbaya, akieleza kuwa mvua za mwaka huu zimeharibu sehemu kubwa ya mtandao wa barabara.
Amesema kati ya kilomita 198.34 za barabara zilizopo, ni kilomita 58 pekee zilizojengwa kwa kiwango cha lami na zege, sawa na asilimia 29 tangu uhuru, hali aliyoitaja kuwa hairidhishi kwa eneo lenye mchango mkubwa wa kiuchumi.
“Kwa zaidi ya miaka 60 tangu uhuru, tumekuwa tukijenga chini ya kilomita moja kwa mwaka. Hii siyo sawa kwa eneo linalochangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Taifa. Serikali iangalie uwezekano wa kukopa au kutumia mapato ya ndani kuboresha miundombinu,” amesema Tarimba.
Kwa upande wake, Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, amesema si kosa kwa Serikali kukopa mikopo yenye masharti nafuu ili kujenga miundombinu, mradi kuwe na usimamizi madhubuti ili kuepusha ubadhirifu.
Pia, amekosoa kile alichokiita utelekezaji wa miradi iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi, akitoa mfano wa Bandari Kavu ya Kwala ambayo, licha ya uwekezaji mkubwa, bado haijaendelezwa ipasavyo.
“Hatuwezi kuanzisha miradi mipya kila kukicha wakati ile tuliyoianzisha haijakamilika. Tunapaswa kuweka mkazo katika kukamilisha miradi iliyopo kabla ya kuanza mingine,” amesema Shabiby.
Wabunge wengine waliounga mkono hoja hiyo ni pamoja na Hawa Mwaifunga, Husna Sekiboko, Sara Msafiri, Ritha Kabati na Patali Shida, ambao walilalamikia kutelekezwa kwa miradi ya maendeleo katika majimbo yao.
