Mtazamo kuhusu fedha unavyoathiri maisha

Katika maisha ya kila siku, watu hupata mafundisho tofauti kuhusu fedha kulingana na mazingira wanayokulia. Wengine hufundishwa kusoma kwa bidii, kupata ajira nzuri na kutegemea mshahara na wengine hufundishwa kutafuta fursa za biashara na uwekezaji.

Mitazamo hii miwili inaweza kuathiri sana maisha ya kifedha ya mtu, hata katika mazingira ya Tanzania, tunaweza kuona tofauti hii wazi katika namna watu wanavyotafuta mafanikio ya kifedha.

Mtazamo wa kwanza unaweza kuitwa mtazamo wa uoga, huu ni mtazamo unaoamini kwamba njia bora ya maisha ni kupata elimu nzuri na ajira yenye mshahara wa uhakika.

Wazazi wengi nchini Tanzania huwafundisha watoto wao kusoma kwa bidii ili wapate kazi nzuri serikalini au katika makampuni kwani ajira inaweza kusaidia kupata kipato cha kila mwezi na kukidhi mahitaji ya familia kama chakula, kodi ya nyumba na ada za watoto.

 Hata hivyo, changamoto ya mshahara ni kwamba kipato chake huwa na mipaka na mara nyingi mtu hupata fedha kulingana na muda anaofanya kazi.

Kwa upande mwingine kuna mtazamo wa mafanikio, huu ni mtazamo unaowahimiza watu kutafuta fursa za biashara na uwekezaji.

Badala ya kutegemea mshahara pekee, mtu anajifunza kujenga mali ambazo zinaweza kuingiza fedha. Katika Tanzania, tunaona watu wengi wamefanikiwa kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo kama maduka, usafirishaji, kilimo au miradi ya huduma mbalimbali.

Biashara hizi zinapokua zinaweza kuleta kipato kikubwa zaidi na hapa somo muhimu katika mtazamo huu ni kuelewa tofauti kati ya mali na vitu vinavyotumia fedha.

Mali ni vitu vinavyoingiza fedha au vinavyoongeza thamani kwa muda, mfano ni nyumba za kupangisha, mashamba ya kilimo, biashara au uwekezaji mwingine.

Lakini kuna vitu ambavyo vinachukua fedha bila kurudisha faida, kama matumizi makubwa ya anasa. Watu wengi hununua vitu vya gharama kubwa wakidhani ni mafanikio, lakini wakati mwingine vituhivyo vinaweza kuwa mzigo wa kifedha.

Katika mazingira ya Tanzania, changamoto nyingine ni kwamba elimu ya fedha haifundishwi sana shuleni hivyo wanafunzi wengi wanamaliza shule wakiwa na elimu ya darasani lakini hawajui jinsi ya kusimamia fedha au kuanzisha biashara.

Ndiyo maana ni muhimu watu kujifunza kuhusu fedha kupitia vitabu, semina, au uzoefu wa maisha. Somo lingine muhimu ni kuwa na vyanzo zaidi ya kimoja vya kipato. Kutegemea mshahara pekee kunaweza kuwa hatari. Ikiwa mtu atapoteza ajira, maisha yanaweza kuwa magumu.

Watu wengi wanaofanikiwa huwa na biashara ndogo, uwekezaji au miradi mingine inayowaongezea kipato. Pia ni muhimu kuwa na ujasiri wa kujaribu na kujifunza kutokana na makosa.

Watu wengi wanaogopa kuanza biashara kwa sababu wanaogopa kushindwa. Lakini ukweli ni kwamba makosa ni sehemu ya kujifunza. Watu wengi waliofanikiwa walipitia changamoto nyingi kabla ya kufikia mafanikio. Usisubiri mpaka kila kitu kiwe sawasawa ndio uanze kufanya biashara.

Ni muhimu kuanza, kisha utaendelea kurekebisha mambo taratibu kadiri unavyoendelea kwani watu wengi hushindwa kuanza kwa sababu wanataka kila kitu kiwe kamili tangu mwanzo.

Ukweli ni kwamba mafanikio huanza kwa hatua ya kwanza, ukichelewa kuchukua hatua, utakuta wengine tayari wameanza na hivyo kukuletea ushindani mkubwa hivyo ni bora kuanza mapema na kuboresha kadiri unavyoendelea.

Kwa ujumla, somo kubwa ni kwamba mafanikio ya kifedha hayategemei tu mshahara au elimu,bali pia mtazamo wa mtu kuhusu fedha na fursa. Kwa Mtanzania wa leo, ni muhimu kuthamini elimu na ajira, lakini pia kujifunza kuhusu biashara, uwekezaji na matumizi sahihi ya fedha.

Kwa kuwa na fikra sahihi, kufanya kazi kwa bidii na kutumia fursa zilizopo, inawezekana kabisa kujenga maisha bora na ustawi wa kifedha kwa muda mrefu.