Dar es Salaam. Mgogoro wa nyumba ya urithi unaohusisha mjane Florentina Francis, mkazi wa mtaa wa Majimatitu A, Kata ya Mianzini Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, umechukua sura mpya baada ya kuibuka mvutano baina yake na ndugu wa marehemu mumewe.
Kutokana na mvutano uliopo, Florentina amewaangukia Watanzania akiomba wamsaidie Sh12 milioni ili awape ndugu wanaotaka kuuza nyumba anayoishi na watoto watatu, akiwamo mwenye ulemavu ili aweze kuishi kwa amani.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake, Florentina (40) amesema nyumba hiyo inatakiwa kuuzwa Sh20 milioni, kati ya hizo ndugu wa mume watachukua Sh10 milioni, mtoto wake wa kufikia Sh2 milioni naye kupewa Sh8 milioni.
Hata hivyo, amesema haoni kama fedha hizo hizo zitamtosha kujenga nyumba nyingine na kuishi na watoto wake, akiwamo mlemavu anayehitaji huduma za karibu.
“Kwa hiyo natamani ningepata kiasi hicho cha fedha nikawapa ili waniachie nyumba, sijajua naweza kuzipata wapi, naomba msaada kwa msamaria yeyote, biashara yangu ni kuuza mandazi,” amesema.
Akieleza sakata lilipoanzia hadi ndugu kuamua kuuza nyumba hiyo, Florentina amesema ni baada ya mume wake kufariki dunia mwaka 2024 na ndugu hao kumnyang’anya hati.
“Kabla ya mume wangu kufariki tuliishi kwa amani na sikuwahi kusikia kesi yoyote ya ndugu kumdai mumewe wauze nyumba wagawane, siku mbili tu baada ya kifo chake walinitaka niwape hati nikawapa bila kujua nia yao,” amesema.
Kwa mujibu wa mama huyo, wakati anaolewa alimkuta mume wake akiwa amejenga vyumba vitatu, lakini walipaendeleza kwa kuongeza nyumba nyingine yenye vyumba vitatu, ambayo walikuwa wameweka wapangaji.
Wakati wanafanya hayo, hati ya kiwanja ilikuwa imeandikwa jina la baba mkwe wake, lakini yeye alijua ipo siku mume wake ataibadilisha lakini akakutwa na umauti kabla hajafanya hivyo.
“Ndio maana ndugu wa mume wangu wamepata nguvu ya kutaka kupauza na hiyo hela ya mgawo haiwezi kutosha kununua uwanja na kujenga nyingine,” amesema.
Florentina Francis, akiwa nje ya nyumba inayotakiwa kuuzwa na ndugu wa mume
Kauli ya ndugu wa marehemu
Wakati Florentina akileza hayo, ndugu wa marehemu, Bahati Rwambow (dada wa mume), amekiri kutaka kuuza nyumba hiyo kwa kile alichoeleza ni baada ya ndugu zake wawili waliorithishwa na baba yao kufariki.
“Hii nyumba baba yetu kabla hajafariki aliturithisha mimi, kaka yangu (mume wa Frorentina) na mdogo wangu mwingine wa kike ambaye pia kwa sasa ameshafariki na nimebaki mwenyewe nikiwa naishi Tanga,” amesema.
Kuhusu uamuzi wa kupauza amesema anataka fedha zitakazopatikana zigawanywe kwa watoto wa ndugu zake pamoja na hao wa wifi yake (Florentina) na nyingine achukue yeye ili kila mtu akafanyie mambo yake.
Amesema walishakubalina jambo hilo kwa kuandiskishana katika ofisi ya Serikali ya Mtaa ya Majimatitu A na ameeleza kushangaa kwa nini wifi yake huyo anataka kuwarudhisha nyuma.
“Nashangaa huyu wifi yangu leo kuja kulalamika kusema nyumba ni ya mume wake wakati nyaraka zote zipo, alitaka sisi wengine tukose haki na nyumba ya baba yetu, we uliona wapi,” amehoji Bahati.
Alipoulizwa kama atakuwa tayari kupewa fedha zikipatikana ili wamwachie mama huyo nyumba kama anavyotaka, alikataa na kusema anachotaka nyumba iuzwe kila mtu achukue chake.
Hata hivyo, Farida Rwambow ambaye ni wifi wa Florentina na aliyeteuliwa kusimamia mauziano hayo, amekuwa na msimamo tofauti na kueleza kama hizo Sh12 milioni zitapatikana ndani ya siku mbili hizi, wapo tayari kumwachia nyumba mama huyo.
“Kwa kuwa hapa tunataka kila mtu apate haki yake kwenye urithi wa nyumba, hivyo hela zikipatikana tutamwachia, lakini sio tena ndio ije ipatikane baada ya mwezi au mwaka, hapana, kwani ndugu zangu wana shida na hizo hela,” amesema Farida.
Kuhusu umiliki, Farida amesema wifi yao huyo anajua kila kitu kuwa hiyo nyumba ni ya ndugu, haelewe maneno ya kuwa ilikuwa ni ya mume wake yanatokea wapi na isitoshe alifuatilia hadi mahakamani akaelewesha kuhusu hilo na nyaraka zote zipo.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mianzini, Richard Butiku amekiri kumfahamu mama huyo na anachojua ni mjane na ameachwa katika nyumba ambayo ni mali ya ndugu watatu.
Amesema wawili kati yao tayari wamefiriki na mmoja aliyebaki ni dada yake ambaye anaishi Tanga, ambao wanataka nyumba hiyo iuzwe kwa kuwa ni mali ya baba yao na si ya huyo mjane.
“Ukisoma nyaraka, kwa kweli nyumba hiyo si mali halali ya huyo Florentine (mjane) bali kairithi kwa mume wake lakini familia ilikaa kwa pamoja kwa busara na kuamua nini kifanyike ili pande zote ziliridhike kusiwe na mgogoro katika eneo hilo.
‘Wakawa wamekubaliana eneo hilo waliuze na yeye (Florentina) akasaini hizo nyaraka kwamba waliuze Sh20 milioni na kwa kuwa mama huyo ana mtoto mwenye ulemavu iIikakubaliwa apewe shilingi milioni nane, mtoto wa kufikia Sh2 milioni na mawifi kila mmoja apewe Shilingi milioni tano, sasa sijajua malalamiko yake hapo ni yapi,” amesema.
Kuhusu kutaka abaki katika nyumba hiyo kwa kuwa fedha atakazopata hazitatizosha kujenga nyumba, Butiku amesema hilo bado hajalisikia kutoka kwake na kwa kuwa ni eneo la urithi ni jambo linalohitaji kushughulikiwa kwa busara.
“Katika hili ninachoona ni huyu mama ama kutumia busara kurudi mahakamani au kukaa na ndugu kuwaambia hizo hela anazotaka nyumba iuzwe hazitoshi, jambo ambalo alipaswa pia kunipa mrejesho,” amesema.
Maelezo ya mtendaji huyo yameungwa mkono na Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Said Mpeta:
“Ni kweli mgogoro huu naujua kwani wiki mbili zilizopita walikuja ofisini kwetu wakaandikishiana makubaliano kuwa wauze na kila mmoja akaweka saini yake akiwemo msimamizi wao wa mirathi.
“Tangu siku hiyo madalali kila siku wanakuja pale ofisini kwangu na mpaka leo ninavyozungumza na wewe, ndugu walikuja ofisini na kuniambia wameshampata mteja,” amesema.
Mpeta amesema: “Wanataka wakutane na huyo Frolentina ili wamalize shughuli ya mauzo lakini hakutokea wala simu zao alikuwa hapokei, lakini walishakubaliana mapema.”
Amesema katika pitapita zake alikutana na mama huyo na kumuuliza kwa nini hajatokea katika kikao hicho, akamjibu bado anajifikiria na maamuzi ya nyumba kuuzwa.
Vaileth Mpolo, amesema Florentina kwa muda mrefu anapitia changamoto na watoto wake baada ya kufiwa na mume wake, hivyo katika hili angeomba familia itumie busara kumuacha hapo.
“Kwa sasa anachoomba ni huruma kwa Watanzania kumsaidia kwa kuwa bado ana mahitaji mengi na anategemewa sana na familia yake ili kuihudumia kwa ukaribu na mazingira rafiki,” anasema Vaileth.
Naye Fatma Nohamed, amesema mbali ya kuachiwa nyumba wanaomba wasamaria wema wamsaidie kupata bajaji ili iweze kumsaidia kutoka na hali ya mtoto wake.
“Lakini pia kuifanya kama kitega uchumi cha kumuingizia kipato kwa kuwa katika kazi ya maandazi hela anayopata haikidhi mahitaji kutokana na familia aliyonayo,” amesema Fatma.
