SERA NA MIFUMO YA FEDHA KUBORESHWA KUIMARISHA UCHUMI

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Serikali imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha sekta ya fedha nchini ili iwe chachu ya maendeleo ya haraka ya kiuchumi, huku ikisisitiza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wote kwa urahisi na gharama nafuu.

Kauli hiyo ilitolewa leo Aprili 9, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa jukwaa la wadau wa sekta ya fedha la mwaka 2026, lenye kauli mbiu isemayo “Sekta ya fedha bunifu na yenye uwajibikaji kwa maendeleo endelevu na jumuishi ya jamii na uchumi.”

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omari, aliwataka wadau wa sekta hiyo kutumia jukwaa hilo kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sera, sheria na mifumo ya kifedha, ili kufikia lengo la kuwa na uchumi imara unaotegemea sekta ya fedha ifikapo mwaka 2050.

“Sekta ya fedha ni mhimili muhimu wa maendeleo ya taifa. Tunahitaji kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wote kwa urahisi na kwa gharama nafuu,” alisema Waziri Omari.

Ameeleza kuwa jukwaa hilo lina lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kujadili utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa miaka kumi (2021–2029), huku akibainisha kuwa sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kumekuwa na mafanikio makubwa katika sekta hiyo, ikiwemo kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za fedha, ongezeko la matawi na mawakala wa benki pamoja na ukuaji wa huduma za fedha kidijitali.

Amebainisha kuwa asilimia 76 ya Watanzania sasa wanapata huduma rasmi za kifedha, hatua inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya simu za mkononi na huduma za fedha mtandao.

Naye Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Munde, amesisitiza umuhimu wa kudhibiti hatari za kifedha ikiwemo biashara haramu na matumizi mabaya ya mifumo ya fedha, huku akihimiza usimamizi madhubuti wa teknolojia mpya za kifedha.

Washiriki wa jukwaa hilo walipata fursa ya kujadili changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya fedha, hususan katika maeneo ya ubunifu wa teknolojia, ujumuishwaji wa kifedha na uwekezaji.

Jukwaa hilo linatarajiwa kutoa maazimio yatakayosaidia kuimarisha sekta ya fedha na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Wadau waliohudhuria ni pamoja na wawakilishi wa mabenki, taasisi za bima, vyama vya ushirika pamoja na sekta binafsi.