LIGI Kuu Bara Alhamisi hii, Aprili 9, 2026, inaendelea na kama utafuatilia basi tambua kwamba macho yote yatakuwa kule Kaskazini katika mikoa ya Arusha na Manyara ambapo kutakuwa na dakika 180 ngumu kutoka kwa timu nne tofauti zikiwa na hesabu ngumu zikiwahusisha Azam na Simba.
Tuanzie pale Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ambapo Simba itakuwa mgeni wa TRA United, mchezo wa kiporo uliosogezwa mbele kutokana na mvua kubwa kunyesha wiki chache zilizopita, ikiwa ni kama mechi ya kisasi.
Baada ya kuangusha pointi mbili mbele ya Azam, Simba inakutana na TRA ambayo haijawahi kuwazuia wekundu hao tangu ilipopanda Ligi Kuu.
Rekodi zinaonyesha kwamba, kabla ya mchezo huu, timu hizo zimekutana mara tano na Simba ikishinda zote tena kwa mabao kuanzia mawili ambapo ushindi mkubwa umekuwa wa 4-0 kwenye mchezo wa kwanza zilipokutana wakati huo ikiitwa Tabora United.
Simba imevuna jumla ya mabao 15 katika mechi tano wakati TRA United ikiwa haijawahi kuzitikisa nyavu za wekundu hao mpaka zinakutana kwenye mchezo huu wa sita.
Hofu pekee kwa Simba msimu huu ni juu ya rekodi yao ikiwa ugenini ambapo kwenye mechi tano zilizopita, imeshinda mbili ilipozichapa Tanzania Prisons (2-0) na Singida Black Stars (2-1), zingine tatu ni sare dhidi ya Dodoma Jiji (1-1), Pamba Jiji (1-1) na Azam (0-0).
Habari njema kwa Simba ni kurejea kwa winga Elie Mpanzu aliyekosa mechi mbili zilizopita kwa kuumwa ambaye ana asilimia 50 ya kucheza mchezo huo ambapo msimu huu mpaka sasa ndiye kinara wa kutengeneza mabao akiwa na asisti tano sawa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC.
Timu hizo mbili zinacheza soka la kasi lakini wekundu hao wanatakiwa kujipanga kwa namna TRA inavyotumia nguvu kubwa kwenye kuzuia na kufunga njia za wapinzani kukamilisha mashambulizi yao.
Kocha wa Simba, Steve Barker akizungumzia mechi hiyo, alisema wanatambua ugumu wake wakienda kukutana na timu nzuri inayocheza soka la kushambulia na kwamba wamejipanga kurudi njia ya ushindi.
“Utakuwa mchezo mgumu, tunakutana na TRA United inayocheza mpira mzuri, ina wachezaji wenye nguvu na kutokana na mchezo wa kwanza kuahirishwa na tulipowafunga nyumbani itaufanya mchezo huu kuwa na presha yake lakini tunataka kushinda turudi kwenye njia ya ushindi,” alisema Barker.
TRA United iliyo chini ya kocha Mrundi, Ettiene Ndayiragije, ikiwa nyumbani ndio imekuwa na matokeo mazuri ambapo kwenye mechi tano zake za nyumbani imeshinda tatu, ikitoa sare moja na kupoteza moja.
Habari mbaya kwa TRA United ni kwamba itawakosa wachezaji wake wawili, beki Chamou Karaboue na kiungo Mzamiru Yassin ambao kanuni zinawazuia kutokana na aina ya mkataba wao wa mkopo wakitokea kwa wekundu hao.
Kocha Ndayiragije akizungumzia mchezo huo alisema anaiheshimu Simba kwamba ni timu nzuri ikwia na wachezaji wakubwa lakini wataingia na falsafa yao kuzuia ubora huo na kutumia makosa yao ili waweze kushinda.
“Simba ni moja kati ya timu kubwa hapa Tanzania,ina wachezaji wenye uzoefu mkubwa lazima uwe na hesabu nzuri, tutajaribu kuzuia yale ambayo yanawapa ubora lakini pia tutumie makosa yao kuweza kutengeeneza ushindi wetu,” alisema Ndayiragije.
ISHU YA TIKETI ZA MASHABIKI
Jana asubuhi taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) iliwakumbuka mashabiki ambao walikata tiketi za mchezo ulioahirishwa Machi 14 mwaka huu ikisema mashabiki hao wataingia bila kununua tiketi mpya za mchezo huu wa leo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mashabiki hao wanatakiwa kuja na kadi ambazo zilitumika kununulia tiketi za kwanza kwa wauzaji, huku wale ambao hawakununua kwenye mchezo wa kwanza wakitakiwa kununua mpya.
Mchezo mwingine utapigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara ambapo Mbeya City inayojitafuta itakapokuwa mwenyeji wa Azam FC.
Rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana mara 18 ambapo Azam imeshinda mechi 13 wakati City ikishinda moja, huku sare nne.
Azam imefunga jumla ya mabao 29 mbele ya City wakati wagonga nyundo hao wakifunga mabao tisa kwenye michezo yote baina ya timu hizo mbili.
Azam FC chini ya kocha Mkongomani, Florent Ibenge, haijafungwa na timu yoyote msimu huu ikiringia kwamba iliifunga City 2-0 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huu.
Hata hivyo, Azam haina rekodi nzuri ikiwa ugenini ambapo kwenye mechi zake tano zilizopita imeshinda mbili dhidi ya Singida Black Stars (2-1) na Dodoma Jiji (3-0) kisha ikapata sare tatu dhidi ya Mashujaa (0-0), Tanzania Prisons (0-0) na Pamba Jiji (2-2).
Mbeya City ilishusha presha kwenye mchezo uliopita baada ya kushinda mbele ya KMC kwa mabao 3-2 ambapo matokeo hayo yataimarisha morali kwa wachezaji na kocha Mecky Maxime.