Nairobi. Tanzania imewaita wawekezaji wa ndani na kimataifa kuchangamkia fursa zilizopo nchini huku ikieleza mafanikio yake katika maendeleo ya miji na sekta ya makazi.
Akizungumza wakati wa kongamano la pili la miji Afrika (2nd African Urban Forum), lililofanyika leo Aprili 9, 2026 jijini Nairobi, Kenya, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo amesema Tanzania imepiga hatua katika utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika.
Amebainisha maeneo mahsusi iliyopiga hatua kuwa ni pamoja na miundombinu, upatikanaji wa nishati, utoaji wa huduma za kijamii na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
“Juhudi hizo zinaendana na mkakati wa bara la Afrika wa kuimarisha muunganiko, biashara na maendeleo jumuishi,” amesema.
Aidha, Dk Akwilapo ameeleza mikakati ya Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto za ukuaji wa kasi wa miji pamoja na upungufu wa makazi ambapo kwa sasa makazi yasiyo rasmi yanakadiriwa kufikia asilimia 67.3.
Amesema katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza mageuzi ya sera, kuanzisha mifumo bunifu ya fedha, kuboresha umiliki wa ardhi pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika makazi nafuu kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.
Aidha, amesema katika kuboresha upatikanaji mikopo ya nyumba, Serikali imeanzisha Taasisi ya Tanzania Mortgage Refinance (TMRC), inayosaidia kupunguza gharama za mikopo, kuongeza muda wa marejesho na kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kupata huduma za kifedha kupitia mikopo midogomidogo.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutumia rasilimali zake za asili pamoja na kudumisha amani na usalama ili kuharakisha utekelezaji wa Ajenda 2063.
Hivyo, ametoa wito kwa washirika wa maendeleo na sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kuwekeza kwenye sekta ya makazi aliyoieleza kuwa ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Kongamano hilo limezinduliwa rasmi Aprili 9, 2026 na Rais wa Kenya, William Ruto na linaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Makazi Bora kwa Wote: Kukuza Mabadiliko ya Kijamii, Kiuchumi na Kimazingira kuelekea Kufanikisha Ajenda 2063”.
Ajenda hiyo inalenga kuhamasisha mijadala inayotoa fursa kwa washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika kubadilishana uzoefu na suluhisho bunifu katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya miji na makazi.
