Wadau wapongeza, kutilia shaka ziara ya Chakwera nchini

Dar es Salaam. Jumuiya ya Madola imemtuma Rais mstaafu wa Malawi, Lazarus Chakwera, kuja nchini kujadili kuhusu matukio yaliyotokea Oktoba 29, mwaka jana, huku baadhi ya wadau wakisifu hatua hiyo na wengine wakionesha wasiwasi na kuhoji iwapo kweli ametumwa na jumuiya hiyo.

Hayo yanakuja wakati jana Chakwera amewasili nchini kwa ziara ya kikazi, takriban miezi sita imepita tangu ilipotangazwa angewasili kama kiongozi wa ujumbe wa Jumuiya ya Madola.

Leo, Aprili 9, 2026, Chakwera amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ulikuwa wa kumkaribisha rasmi nchini pamoja na kuashiria kuanza kwa ratiba yake ya kikazi, inayojumuisha mazungumzo na wadau mbalimbali.

Aidha, Chakwera anatarajiwa kukutana na ujumbe wa Serikali katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).

Kwa mujibu wa taarifa za awali, ziara ya Chakwera inatarajiwa kujumuisha mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Tanzania, na masuala ya kuimarisha demokrasia na haki za binadamu yatajadiliwa.

Aidha, anatarajiwa kukutana na wadau mbalimbali, wakiwemo wawakilishi wa asasi za kiraia, sekta binafsi na vyama vya siasa, kujenga msingi wa mshikamano na hatua za maridhiano.

Ziara hiyo inatazamwa kama sehemu ya jitihada za Jumuiya ya Madola katika kuimarisha uhusiano na nchi wanachama wa Afrika Mashariki, huku ukilenga kuongeza ushirikiano katika maeneo ya utawala bora.

Historia ya uteuzi na ziara iliyokwama

Novemba, 2025, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Botchwey, alimteua Chakwera kuwa mjumbe maalumu wa jumuiya hiyo, na ilitangazwa angefanya ziara ya siku nne nchini kuanzia Novemba 18 hadi 21, lakini hakuonekana kama ilivyotarajiwa.

Rais wa Zamani wa Malawi, Lazarus Chakwera na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Ayorkor Botchwey, amewasili nchini Aprili 8, 2026 kwa ziara ya kikazi. Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe.

Taarifa ya kuwasili kwa Chakwera nchini ilitolewa usiku wa kuamkia jana na alipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe.

Katika ziara hiyo ya awali, kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Jumuiya ya Madola, angefanya majadiliano na wadau mbalimbali kuhusu masuala yanayohusiana na uchaguzi na mustakabali wa maendeleo ya nchi.

Ilielezwa angekutana na viongozi wa Serikali, wanasiasa, mashirika ya kiraia, viongozi wa dini, mila na wadau wa kitaifa na kimataifa, ili kuanzisha mjadala jumuishi kuhusu maridhiano, haki za kisiasa na kuimarisha demokrasia.

Ziara hiyo ya awali ilitangazwa wiki chache baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, siku ambayo kuliibuka maandamano yaliyozaa vurugu, kusababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali za umma na zile za watu binafsi.

Hata hivyo, haikuwahi kuwekwa wazi kuhusu nini kilikwamisha ziara hiyo ya Chakwera. Hata Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati huo aliwahi kuiambia Mwananchi kuwa hakuwa na taarifa za ziara ya kiongozi huyo nchini.

Lakini Chakwera anakuja mwezi mmoja baada ya Tanzania kupokea ujumbe mwingine wa jumuiya ya kimataifa. Ilimpokea mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Parfait Onanga-Anyanga, aliyefanya ziara nchini kuanzia Machi 8 hadi 12.

Katika ziara hiyo, Onanga-Anyanga alizungumza na viongozi wa vyama vya ACT Wazalendo, Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na asasi za kiraia, kuhusu yaliyotokea Oktoba 29.

Hata hivyo, Chadema baadaye ilimwandikia barua Katibu Mkuu wa UN, António Guterres, ikimweleza wasiwasi wake kwa mjumbe huyo, kwa kile ilichodai anaweza kuwa na mgongano wa maslahi, kwani aliwahi kufanya kazi na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro.

Pia, ziara ya Chakwera inakuja siku kadhaa baada ya aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Palamagamba Kabudi, kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Ayorkor Botchwey, yaliyolenga kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya utawala bora, demokrasia na maendeleo ya pamoja miongoni mwa nchi wanachama.

Mazungumzo hayo yalifanyika Machi jijini London, Uingereza, sambamba na ushiriki wa Kabudi katika kikao cha 72 cha Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Madola (CMAG) kilichofanyika Machi 7, 2026, pamoja na Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola (CFAMM) uliofanyika Machi 8, 2026.

Kabudi, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), katika mazungumzo hayo alisema Jumuiya ya Madola ni jukwaa muhimu linalochochea mshikamano wa kimataifa na Tanzania itaendelea kushiriki katika programu na mikakati inayolenga kuimarisha demokrasia na maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Botchwey, aliipongeza Tanzania kwa mchango wake katika shughuli za Jumuiya ya Madola na nafasi yake katika kuendeleza ajenda za pamoja za maendeleo.

Pia, aliahidi kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Tanzania pamoja na nchi nyingine wanachama ili kuhakikisha malengo ya jumuiya hiyo yanafikiwa, hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Wanaoonesha wasiwasi wanasema kumekuwa na wimbi la watu wanaofanya ziara nchini kuisafisha mamlaka kwa jina la jumuiya ya kimataifa, hivyo wana mashaka iwapo Chakwera ametumwa kweli na jumuiya hiyo au ni mpango wa mamlaka kujisafisha.

Kwa upande wa wanaopongeza, wanasema uwakilishi huo ulisubiriwa kwa hamu kwa kuwa ni mamlaka huru na itasimamia mambo bila kuwa na upande. Zaidi, wanasema jumuiya hiyo ilionesha nia mapema ya kutafuta mwafaka wa jambo hilo.

Tayari baadhi ya vyama vya siasa vilivyozungumza na Mwananchi vimeonesha nia ya kushiriki mazungumzo na mwakilishi huyo iwapo kutakuwepo na vikao, vikisisitiza mamlaka hiyo haitakuwa na haya kuusema ukweli.

Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita, amesema chama hicho kipo tayari kutoa ushirikiano kwa mwakilishi huyo wa Jumuiya ya Madola.

Sababu za utayari wao wa kutoa ushirikiano ni kile alichoeleza, mambo yaliyotokea yalihitaji kuingiliwa na jumuiya ya kimataifa ili kutoa mwafaka wa namna ya kutoka.

Ilivyo bahati, amesema jumuiya ya madola ilionesha mapema nia ya kutafuta mwafaka wa changamoto iliyotokea nchini, hivyo anaiona ni mamlaka sahihi kufanya itakachokifanya.

“Tuko tayari kwa sababu tangu siku ya kwanza tulisema jambo hili linahitaji kuingiliwa na jumuiya ya kimataifa, kwa sababu ni mamlaka huru na itafanya kazi yake bila upendeleo,” amesema.

Amesema ni muhimu kushirikiana na jumuiya hiyo kwa sababu ni mamlaka inayoaminika, kwani haina upande, hivyo itasimamia mchakato kwa namna ya haki.

“Tunahitaji jumuiya ya kimataifa kwa kuwa naamini itatafuta mwafaka kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya kutatua migogoro na kuwezesha watu kuwajibika ipasavyo,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) Bara, Devotha Minja, amesema chama hicho hakikuwahi kujitenga na juhudi zozote za kujenga nchi.

Amesema iwapo watapata nafasi na mwaliko wa kushiriki mazungumzo hayo, watakwenda kutoa ushirikiano kwa kila namna.

“Kama tutahitajika tuko tayari kwa mazungumzo ya kila namna na lengo letu ni kujenga nchi na kuhakikisha maridhiano yanakuwepo nchini,” amesema.

Pamoja na hatua hiyo, amesema matamanio ya chama hicho ni kuona yaliyotokea Oktoba 29, mwaka jana hayajirudii nchini kwa kuwa ni matukio yasiyofaa.

Mwanaharakati wa haki za binadamu, Hellen Kijo Bissimba, amesema bado kuna wasiwasi wa ujio wa jumuiya ya kimataifa nchini kwa kuwa hakuna uhakika wa nani aliyeileta.

Rais wa Zamani wa Malawi, Lazarus Chakwera na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Ayorkor Botchwey, amewasili nchiniAprili 8, 2026 kwa ziara ya kikazi. Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe.

Ameeleza yapo makundi yanayoona wawakilishi hao wa jumuiya ya kimataifa wameletwa nchini na Serikali, hivyo watakachokifanya ni kuisafisha.

Lakini amesema wengine wanadhani wawakilishi hao wameletwa na jumuiya hiyo na kwamba wapo tayari kuwasikiliza na kuwapa ushirikiano kwa watakachohitaji.

Kwa mtazamo wake, amesema hata angekuja nani kutoka jumuiya ya kimataifa asingefaa na hatafanya lolote kama ndani ya nchi bado kuna watu wenye majeraha ambayo hayajatibiwa.

Ameeleza tiba ya majeraha na vidonda vya wengi ipo ndani ya nchi kwa watu wote, zikiwemo mamlaka, kuukubali ukweli na kuamua kuchukua hatua za uwajibikaji au vinginevyo.

“Kwa hali ilivyo, hatuhitajiki watu wa nje kuja kusaidia, hasa kama watu wa ndani hawajakubali kusaidiana kupona. Bado, kama nchi hatujasaidiana kupona, pengine hata wa nje watasema, watapita na wataondoka,” amesema.

Hatua iliyofikiwa sasa, amesema ni muhimu kujiganga wenyewe ndani kwa kueleza ukweli, kuwajibishana, badala ya kufungua milango kwa jumuiya za kimataifa.