Wadau watia neno vyeti kudhamini mikopo

Dom/Dar. Wakati Serikali ikisema ipo mbioni kupeleka bungeni muswada wa sheria utakaoruhusu vyeti vya taaluma kutumika kama dhamana ya mikopo, wadau wa uchumi na vijana wanashauri hatua hiyo iende sambamba na mifumo madhubuti ya utekelezaji ili kuepusha hatari zinazoweza kujitokeza kwa wakopaji na wakopeshaji.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, leo Alhamisi, Aprili 9, 2026, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.

Alikuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Timida Fyandomo, aliyehoji Serikali ina mkakati gani kuwasaidia vijana kuwekeza na kuwaunganisha kwenye kampuni kubwa za ndani na nje ya nchi.

Hoja hiyo ya vyeti huenda ikawa ni mwarobaini wa kilio cha muda mrefu ambacho mara kadhaa kiliwasilishwa na aliyekuwa mbunge wa Kahama (CCM), Jumanne Kishimba.

Kishimba amekuwa akilalamikia utaratibu unaotumiwa na Serikali wa kukataa kuwapa mkopo vijana waliohitimu masomo yao wakiwa na vyeti, wakati wao walilipa fedha nyingi za ada na matokeo yake wakatunukiwa vyeti.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, mpango huo uko katika hatua nzuri na Serikali italeta muswada huo wakati wowote, ili vyeti vya taaluma vitambulike rasmi kama dhamana inayohamishika, hatua inayolenga kuwafungulia milango ya mikopo maelfu ya vijana wanaokosa dhamana za jadi.

Amesema changamoto ya ukosefu wa ajira imeendelea kuwa kubwa, huku idadi ya wahitimu ikiongezeka kila mwaka na kuwaacha wengi wao wakitegemea familia zilizowasomesha.

Hivyo, hatua hiyo inalenga kuwapa uwezo wa kuanzisha shughuli za kiuchumi badala ya kusubiri ajira rasmi.

Mbali na mpango huo, Serikali pia imetenga Sh200 bilioni kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya kuwawezesha vijana, sambamba na ahadi ya kuzalisha zaidi ya ajira milioni nane katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Wataalamu waonya hatari zilizopo

Mwananchi limezungumza na wadau mbalimbali juu ya uamuzi huo ambapo wachumi na wataalamu wa fedha wanaonya kuwa, licha ya nia njema ya Serikali, matumizi ya vyeti kama dhamana yanahitaji umakini mkubwa ili kuepuka athari zisizotarajiwa.

Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo, amesema ingawa hatua hiyo inalenga kutatua tatizo la dhamana, kibenki dhamana lazima iwe na uwezo wa kufidia mkopo pale mkopaji anaposhindwa kulipa.

“Dhamana ni kitu kinachoweza kuchukuliwa na kuuzwa ili kurejesha fedha. Sasa kwa vyeti, itakuwaje mtu akishindwa kulipa? Hapa ndipo changamoto ilipo,” amesema Profesa Kinyondo.

Ameshauri Serikali pia izingatie kurahisisha masharti ya mikopo kupitia mifumo ya kifedha ili kuwafanya vijana wengi zaidi kukopesheka bila kuweka mzigo mkubwa wa hatari kwa taasisi za fedha.

Kwa upande wake, mtaalamu wa usimamizi wa fedha, Tobias Swai, amesema ipo haja ya kuweka mfumo utakaovipa vyeti thamani ya fedha kulingana na kiwango cha elimu na ujuzi wa mhusika.

“Vyeti vina makundi mbalimbali, vipo vya PhD, digrii na ngazi nyingine. Lazima kuwe na vigezo vya kuweka thamani yake katika kiwango cha mikopo,” amesema.

Ameongeza kuwa dhamana yoyote lazima iwe na sifa ya kuuzika na kuwa na thamani halisi, hivyo utekelezaji wa mpango huo unapaswa kuwa wa kisayansi zaidi ili kulinda pande zote mbili, mkopaji na mkopeshaji.

Hoja ya Nida yaibuka upya

Wakati wataalamu wakijadili hatari zake, baadhi ya wawakilishi wa vijana wanaibua hoja ya ujumuishi, wakihofia kuwa matumizi ya vyeti yanaweza kuwaacha nje wale wasio na elimu ya juu.

Mkurugenzi wa tafiti na mafunzo wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf), Shukuru Zouma, amesema badala ya kutegemea vyeti pekee, Serikali ingeimarisha matumizi ya Kitambulisho cha Taifa (Nida) kama dhamana mbadala inayoweza kumfikia kila Mtanzania.

“Hili ni wazo zuri, lakini linaweza kuwa la kibaguzi. Sio wote wana vyeti. Nida inaweza kuwa suluhisho la jumla kwa sababu kila mtu anaweza kuipata,” anasema.

Hoja hiyo imeungwa mkono na Katibu Mwenezi wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Bakari Makame, anayesisitiza umuhimu wa kusogeza huduma za Nida karibu na wananchi, ili kuongeza upatikanaji wake na kuifanya iwe nyenzo kuu ya kiuchumi.

Kwa upande mwingine, baadhi ya vijana wamepokea kauli hiyo kwa tahadhari, wakitaka kuona utekelezaji wake badala ya kubaki kwenye ahadi za kisiasa.

Mratibu wa vijana wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Kivicha), Masoud Mambo, amesema historia ya ahadi nyingi zisizotekelezwa inawafanya vijana kuwa na mashaka na mipango mipya.

“Tunataka kuona hatua zikichukuliwa, sio maneno tu. Vijana wana matatizo ya kweli ya mitaji, na kama hili litatekelezwa litakuwa msaada mkubwa,” amesema.

Ametahadharisha kuwa kushindwa kutekeleza ahadi kama hizo kunaweza kugeuka kuwa mzigo wa kisiasa baadaye, kwani vijana wa sasa wanafuatilia na kuhifadhi kumbukumbu za ahadi zote zinazotolewa.

Mpango wa kutumia vyeti kama dhamana unaonekana kuwa na matumaini mapya kwa wadau na vijana, lakini wadau wamesisitiza kuwa mafanikio yake yatategemea zaidi ubora wa sera, uthabiti wa mifumo ya utekelezaji na dhamira ya kweli ya mamlaka.