Simiyu. Baadhi ya wananchi mkoani Simiyu wametaka kuwepo kwa udhibiti mkali wa dawa na vifaatiba vilivyoisha muda wa matumizi ili kulinda afya za jamii.
Wakizungumza na Mwananchi leo Aprili 9, 2026, wananchi hao wamesema bado kuna hatari ya bidhaa hizo kuendelea kuonekana katika baadhi ya maduka ya dawa.
Mkazi wa Bariadi mjini, Silvester Lupembe amesema wananchi wengi hawaangalii muda wa matumizi ya dawa wanazonunua, hivyo ni jukumu la wauzaji kuhakikisha wanatoa dawa salama kwa watumiaji.
“Watu wengi wanaamini mfamasia ndiye mtaalamu, hivyo wanachopewa wanatumia bila kuangalia tarehe ya mwisho ya matumizi. Ni muhimu sana maduka ya dawa yahakikishe hayauzi dawa zilizopitwa na wakati,” amesema.
Kwa upande wake, mkazi wa Maswa, Maria Joseph amesema elimu kwa wananchi kuhusu kuangalia muda wa matumizi ya dawa, pia, inapaswa kutolewa mara kwa mara ili kuwasaidia kujilinda.
“Wakati mwingine tunanunua dawa kwa haraka bila kuangalia tarehe zake. Elimu zaidi itatusaidia wananchi kujilinda wenyewe pamoja na kusaidia kudhibiti wauzaji wasiokuwa waaminifu,” amesema.
Naye Paulo Jisinza, mkazi wa Meatu, amesema ukaguzi wa mara kwa mara kutoka kwa mamlaka husika ni muhimu ili kuondoa uwezekano wa dawa zisizo salama kuingia sokoni.
“Kama TMDA itafanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuchukua hatua kwa wanaokiuka sheria, itasaidia sana kulinda afya za wananchi hasa maeneo ya vijijini,” amesema.
Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Venance Burushi amesema mamlaka hiyo inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha dawa zote zinazouzwa nchini zinakuwa salama na zenye ubora unaokubalika.
Amesema TMDA imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya dawa, vituo vya afya na maghala ya kuhifadhi dawa ili kubaini bidhaa zilizoisha muda wa matumizi na kuchukua hatua kwa wahusika.
“Tunawasikiliza wananchi na tunawahakikishia kuwa TMDA ipo makini katika kuhakikisha dawa zote zinazofika kwa wananchi zinakuwa salama. Endapo tutabaini uwepo wa dawa zilizoisha muda wa matumizi, hatua za kisheria huchukuliwa mara moja dhidi ya wahusika,” amesema.
Ameongeza kuwa mamlaka hiyo pia inaendelea kutoa elimu kwa wafamasia na wamiliki wa maduka ya dawa kuhusu umuhimu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye stoo na rafu za dawa ili kubaini bidhaa zinazokaribia kuisha muda wake na kuchukua hatua mapema.
“Ni wajibu wa kila mfamasia kuhakikisha dawa zote zinazouzwa zinakuwa salama, zenye ubora na bado zipo ndani ya muda wake wa matumizi. Bidhaa zilizoisha muda wake hazipaswi kuendelea kuwepo kwenye rafu za maduka,” amesisitiza.
