Mwanza. Imezoeleka kwa wanaume wengi kuchagua nguo za ndani ama chupi maarufu hivi sasa kwa jina la ‘boxer’, kwa kuangalia mwonekano, bei au mtindo bila kufikiria athari zake kiafya.
Katika miaka ya karibuni, wataalamu wa afya ya uzazi wameanza kuonya juu ya ongezeko la matatizo ya ubora wa mbegu za kiume duniani, huku baadhi ya kazi za kitafiti zikionesha kuwa sababu si lishe au mtindo wa maisha pekee, bali hata mavazi ya ndani yanaweza kuwa na mchango.
Kazi hizo za kitafiti zinaibua mjadala mzito, je baadhi ya boxer hasa zile zinazobana na zilizotengenezwa kwa vitambaa vya polyester zinaweza kuwa hatari kwa afya ya uzazi wa mwanaume?
Utafiti wa mwaka 2018 uliofanywa na watafiti wa Chuo cha Afya cha Harvard nchini Marekani ulibaini kuwa wanaume wanaovaa chupi au boxer zisizobana walikuwa na kiwango kikubwa cha mbegu za kiume ikilinganishwa na wanaovaa zinazobana.
Katika utafiti huo uliohusisha zaidi ya wanaume 600 waliokuwa wakipatiwa matibabu ya uzazi kati ya mwaka 2000 na 2017, ilibainika kuwa waliovaa chupi zisizobana walikuwa na wastani wa asilimia 25 zaidi ya mkusanyiko wa mbegu za kiume. Watafiti walihusisha tofauti hiyo na joto la korodani.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyochapishwa kwenye jarida la Human Reproduction, korodani zimeumbwa nje ya mwili kwa sababu zinahitaji joto la chini kidogo kuliko joto la kawaida la mwili ili kuzalisha mbegu bora. Hivyo, boxer zinazobana huongeza joto na kuathiri mchakato huo unaoitwa ‘spermatogenesis’ yaani mchakato wa kutengeneza mbegu za kiume ndani ya korodani.
Mbali na suala la kubana, wataalamu wanaelekeza macho kwenye aina ya kitambaa kinachotumika.
Polyester ni moja ya vitambaa vinavyotumika sana kutengeneza boxer za kisasa kwa sababu ni nafuu, hudumu na hunyumbulika.
Hata hivyo, polyester hutengenezwa kutokana na kemikali za plastiki. Tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa kemikali kama phthalates na bisphenol A (BPA) zinaweza kuathiri mfumo wa homoni za binadamu.
Utafiti wa mwaka 2021 uliochapishwa katika jarida la Environmental International ulibaini kuwa wanaume wenye viwango vya juu vya phthalates mwilini walikuwa na viwango vya chini vya homoni ya testosterone.
Testosterone ni homoni muhimu katika uzalishaji wa mbegu za kiume na nguvu za kiume.
Ingawa tafiti hizo hazijasema moja kwa moja kuwa boxer za polyester ndizo chanzo kikuu cha kemikali hizo mwilini, wataalamu wanasema kuvaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa plastiki kunaweza kufanya mwili kukutana na kemikali hizi mara kwa mara kwa muda mrefu.
Dk Jaime Knopman, mtaalamu wa masuala ya uzazi, amewahi kueleza kuwa joto ni adui mkubwa wa uzalishaji wa mbegu za kiume.
“Iwapo ni boxer ya plastiki ambayo imeshika sana korodani, basi hupunguza ubora wa mbegu za kiume, kiwango cha mbegu hizo na kuathiri uzazi wa mwanaume,” amewahi kunukuliwa akisema katika mahojiano ya masuala ya afya.
Kwa upande wake, Dk Alex Robles wa Chuo Kikuu cha Columbia anasisitiza kuwa tafiti zaidi zinahitajika, lakini ushahidi wa awali, unaonesha kuwa joto la muda mrefu katika eneo la korodani linaweza kupunguza uzalishaji wa mbegu.
Anasema: “Kuvaa chupi inayokushika, kuketi kwa muda mrefu au kuendesha baiskeli, huongeza joto kwenye korodani. Tafiti za awali zimehusisha hali hiyo na kupungua kwa ubora wa mbegu za kiume.”
Maisha ya kisasa yameongeza hatari hiyo. Wanaume wengi hufanya kazi za ofisini zinazowalazimu kukaa kwa saa nyingi.
Utafiti wa mwaka 2015 uliofanywa Ufaransa ulibaini kuwa wanaume wanaokaa zaidi ya saa sita kwa siku walikuwa na viwango vya chini vya mbegu za kiume.
Hali hiyo ilihusishwa na ongezeko la joto katika eneo la nyonga. Iwapo mwanaume huyo atavaa boxer zinazobana au za polyester zisizoruhusu hewa kupita, joto huongezeka zaidi.
Wataalamu wanasema mchanganyiko wa kukaa muda mrefu, kuvaa boxer zinazobana na mazingira ya joto huweka korodani katika hali isiyofaa kwa uzalishaji wa mbegu.
Je, kutovaa boxer ni suluhisho?
Baadhi ya wanaume wameanza kuamini kuwa kutovaa boxer au kuvaa nguo huru nyumbani kunaweza kusaidia.
Tafiti ndogo zimeonesha kuwa wanaume wanaolala bila chupi hupata mzunguko mzuri wa hewa na udhibiti wa joto.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa hilo pekee halitoshi. Sababu nyingine kama lishe duni, uvutaji sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, msongo wa mawazo na magonjwa kama kisukari pia huchangia matatizo ya uzazi.
Utafiti wa mwaka 2020 uliochapishwa katika jarida la Andrology barani Ulaya ulibaini kuwa wanaume wanaovuta sigara, walikuwa na upungufu wa mbegu za kiume kwa zaidi ya asilimia 15 ikilinganishwa na wasiovuta.
Kutokana na ushahidi uliopo, wataalamu wanashauri wanaume kuchagua boxer au chupi za pamba au vitambaa vya asili vinavyoruhusu hewa kupita.
Dk Emmanuel Mjoli kutoka kituo cha Bright Future health Center mkoani Arusha, anasema ni muhimu wanaume kuepuka boxer zinazobana sana kwa muda mrefu.
“Kusimama au kutembea baada ya kukaa kwa muda mrefu lakini pia kuepuka joto kali kama sauna au kukaa na kompyuta mpakato mapajani kwa muda mrefu hii itasaidia mbegu bora kuzalishwa,”anasema.
Anashauri ili mbegu ziwe kwa kiwango kizuri ni vizuri kula vyakula vyenye madini kama zinki na vitamini C, kuacha sigara na kupunguza pombe.
Tafiti nyingi zimekubaliana kuwa joto kupita kiasi kwenye korodani, linaweza kupunguza ubora na wingi wa mbegu za kiume.
Boxer zinazobana na zilizotengenezwa kwa polyester zinaweza kuongeza joto na uwezekano wa mara kwa mara wa kemikali za plastiki. Ingawa utafiti zaidi bado unahitajika kubaini uhusiano wa moja kwa moja, wataalamu wanashauri tahadhari ichukuliwe mapema.
Kwa mwanaume anayejali afya yake ya uzazi, uchaguzi wa boxer si suala la mitindo tu, ni suala la afya.
Kubadili aina ya chupi, kupunguza joto kwenye korodani na kuboresha mtindo wa maisha, kunaweza kuwa hatua ndogo lakini yenye faida kubwa kwa mustakabali wa uzazi.