Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amependekeza Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya balozi na ofisi za uwakilishi ili kuziwezesha kutimiza shughuli za diplomasia ya uchumi na majukumu ya kimkakati.
CAG Kichere amebainisha hayo kwenye Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Serikali Kuu ya mwaka 2024/25, iliyowasilishwa bungeni Dodoma leo Aprili 10, 2026, zikiwa zimepita siku chache tangu alipoiwasilisha kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika ripoti hiyo, CAG amebainisha kwamba ukaguzi wake ulibaini kuwa jumla ya Sh188.73 bilioni zilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za balozi na ofisi za uwakilishi 44 za Tanzania, ambapo Sh14.12 bilioni, sawa na asilimia 7, zilitengwa mahsusi kwa ajili ya shughuli muhimu, zikiwemo kukuza biashara, uwekezaji, masoko ya utalii, na ushirikiano wa nchi mbili.
Amebainisha kwamba kiasi kilichobaki cha Sh174.61 bilioni, sawa na asilimia 93, kiligharamia matumizi ya uendeshaji wa ofisi ikiwa pamoja na kodi ya pango, umeme, maji, ada za shule, na posho za huduma nje ya nchi.
CAG ameongeza kuwa fedha zilizowasilishwa katika balozi na ofisi za uwakilishi, jumla ya Sh199.05 bilioni zilizidi bajeti iliyopangwa. Kati ya hizo, Sh14.09 bilioni, sawa na asilimia 7, zilitumika kwa shughuli muhimu katika balozi na ofisi za uwakilishi, wakati Sh184.96 bilioni sawa na asilimia 93 ziligharamia matumizi ya uendeshaji wa ofisi.
Amesisitiza kwamba kiasi kikubwa cha fedha kilichotumika kwa matumizi mengine ya ofisi kilizuia balozi na ofisi za uwakilishi kutekeleza ipasavyo shughuli za kimkakati za diplomasia ya uchumi.
“Ninapendekeza Serikali ihakikishe kunakuwepo na upatikanaji wa fedha za kutosha na kuongeza mgao wa bajeti kwa shughuli za diplomasia ya uchumi katika balozi na ofisi za uwakilishi ili kutimiza majukumu yao ya kimkakati,” amesema CAG Kichere katika ripoti yake.
Wakati huohuo, ukaguzi huo wa CAG ulibaini kwamba Sh199.05 bilioni kilichotumwa katika balozi na ofisi za uwakilishi 44 kwa mwaka wa Fedha 2024/25 kilichelewa kutumwa, uchelewaji ukiwa kuanzia siku 30 hadi 75 kwa kila mwezi kwa mwaka mzima,
Amesema jambo hilo liliathiri uwezo wa kifedha wa balozi na ofisi za uwakilishi za Tanzania katika kutimiza majukumu kwa wakati, ikiwa pamoja na malipo ya kodi, ada za shule, gharama za uendeshaji ofisi na posho za wafanyakazi.
“Ninarudia pendekezo langu la mwaka uliopita kwamba Serikali itenge bajeti toshelezi kwa ajili ya balozi na ofisi za uwakilishi na kuziwasilisha kwa wakati.
“Hatua hii itawezesha balozi na ofisi za uwakilishi kutekeleza majukumu yake muhimu kama vile kulipa kodi za pango, ada za masomo, gharama za uendeshaji, na posho za wafanyakazi bila kukwama hivyo kudumisha taswira njema ya nchi kimataifa,” amebainisha CAG.
Mbali na masuala ya kibajeti na uchelewaji wake, CAG amebainisha ucheleweshaji wa hati za utambulisho wa mabalozi katika baadhi ya vituo huku akipendekeza Wizara ya Mambo ya Nje itoe hati hizo kwa mabalozi husika.
Amebainisha kwamba Ubalozi wa Tanzania, Washington D.C umeidhinishwa kuiwakilisha Tanzania nchini Marekani, Mexico pamoja na mashirika kadhaa ya kimataifa. Hata hivyo, balozi bado hajapokea hati za utambulisho kwa ajili ya Mexico, licha ya kukumbushia mara kwa mara na kuwasilisha hati ya utambulisho Februari 2023.
Aidha, amesema Ubalozi wa Tanzania, Muscat umeidhinishwa kuiwakilisha Tanzania nchini Oman, Iran, na Yemeni. Hata hivyo, balozi bado hajapokea hati ya utambulisho kwa nchi za Iran na Yemen kutoka Wizara ya Mambo ya Nje tangu alipoteuliwa Oktoba 2023.
“Ninapendekeza Serikali ianzishe mazungumzo ya kidiplomasia na Serikali ya Mexico ili kushughulikia hati za utambulisho zilizowasilishwa kwao.
“Pia, ihakikishe Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inatoa hati za utambulisho zinazohitajika kwa mabalozi walioko Muscat na Moscow,” amependekeza CAG katika ripoti hiyo.
Akiangazia ripoti ya CAG katika eneo hilo, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo amesema diplomasia ya uchumi siyo kauli tu, bali ni shughuli zinazohitaji rasilimali halisi: tafiti za masoko, uwekezaji wa uhusiano (networking), matukio ya kibiashara, na ufuatiliaji wa fursa.
Amesema Sh14 bilioni kuzigawanya kwa balozi 44 maana yake ni wastani wa chini sana kwa kila kituo. Amesema hiyo inaleta changamoto ya kushindwa kutafuta wawekezaji na masoko, kukosa wataalamu na kutoutoonekana kirahisi kwenye nchi husika.
“Ni muhimu kuweka malengo ya kupimika kwa kila balozi, kuajiri au kupeleka wataalamu wa biashara na uwekezaji, kuunganisha diplomasia na sekta binafsi na kufanya performance audit (ukaguzi wa ufanisi) ya mara kwa mara.
“Ndiyobajeti kubwa inaweza kusaidia sana. Lakini kama mfumo haujaboreshwa, inaweza kuwa tu ‘gharama kubwa bila matokeo makubwa’,” amesema Shoo wakati akichambua ripoti ya CAG katika eneo hilo.
