Dk Mwinyi atengua, kuteua wakuu wa wilaya

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametengua na kuteua wakuu wa wilaya watano Zanzibar.

Kati ya hizo, tatu zilikuwa zinakaimiwa na mbili waliokuwa wakuu wa wilaya hizo uteuzi kutenguliwa.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Zena Said, Ali Abdalla Said Natepe ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharib B akichukua nafasi ya Amour Juma Mmanga ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Kabla ya uteuzi huo Natepe alikuwa Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mjini Magharibi. Riziki Daniel Yussuf ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A akichukua nafasi ya Rashid Simai Msaraka ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

“Kabla ya uteuzi huo, Riziki alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Sherehe na Maadhimisho ya kitaifa katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,” amesema

Wengine walioteuliwa ni Dk Said Haji Mrisho anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja. Kabla ya uteuzi huo alikuwa katibu Tawala wa wilaya hiyo.

Taarifa hiyo pia imesema Laila Burhan Ngozi ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi A. Laila aliwahi kuwa muuguzi na kwasasa alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Zuhura Mgeni Othman ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chakechake Pemba. Zuhura aliwahi kuwa ofisa mdhamini wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Pemba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huo unaanza leo Aprili 10 na waterless wote wataapishwa Aprili 13 saa 4:00 asubuhi Ikulu Zanzibar.