KCMC yaanza ujenzi kituo cha kisasa tiba za moyo, ugonjwa ukishamiri Kaskazini

Dar es Salaam. Magonjwa ya moyo yanaendelea kuwa tishio kubwa kwa maisha ya Watanzania, huku takwimu zikionyesha kuwa asilimia 18 ya vifo vinavyotokea katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC vinahusishwa na magonjwa hayo.

Aidha, asilimia 14 ya wagonjwa wanaopokelewa hospitalini wanakabiliwa na matatizo ya moyo, hali inayoakisi ukubwa wa changamoto hii katika jamii. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita pekee, jumla ya wagonjwa zaidi ya 24,000 waliripotiwa kuwa na matatizo ya moyo katika hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa Daktari Bingwa Mbobezi wa watoto wenye matatizo ya moyo KCMC, Ronald Mbwasi, hali hiyo ni kubwa zaidi inapochunguzwa kwa upana nchini na barani Afrika, ambako magonjwa ya moyo yanachangia sehemu kubwa ya vifo.

Amesema barani Afrika, kati ya vifo 100 vinavyotokea, watu 13 hufariki kutokana na magonjwa ya moyo huku wastani wa umri wa kuishi kwa wagonjwa wa moyo ukiwa ni miaka 28 pekee.

Mbwasi ameongeza kuwa nchini Tanzania, hali ni ya kutia wasiwasi zaidi, hasa kwa watoto. Takribani watoto 70,000 huzaliwa kila mwaka wakiwa na matatizo ya moyo, lakini ni asilimia 10 tu wanaogundulika mapema.

Katika kanda ya Kaskazini yenye zaidi ya wakazi milioni 15, takribani watoto 4,000 huzaliwa kila mwaka na matatizo hayo lakini chini ya 1,000 hugundulika na hata hao si wote wanapata matibabu kwa wakati.

Daktari Mbwasi ameonya kuwa changamoto kubwa ni wagonjwa wengi kufika hospitalini katika hatua za mwisho za ugonjwa, hali inayopunguza uwezekano wa mafanikio ya matibabu.

Ameeleza mifano ya watoto wanaokumbwa na tatizo hilo, akiwemo mtoto mchanga aliyezaliwa Arusha ambaye alianza kuonyesha dalili baada ya mwezi mmoja, ikiwemo kushindwa kunyonya, kikohozi kisichoisha na kushindwa kuongezeka uzito.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya KCMC, Gileard Masenga wakati akizungumzia mradi wa hospitali ya kisasa itakayojengwa mkoani Kilimanjaro  yenye thamani ya zaidi ya Sh25 bilioni itakayohudumia magonjwa wa moyo.

“Kuna mtoto mmoja mchanga alizaliwa Arusha, wazazi wakawa na furaha wakamchukua na kurudi naye nyumbani pasipokujua kuwa huyu mtoto amezaliwa na shida ya moyo, wiki zinapita mtoto anakua vizuri, baada ya mwezi anaanza kupata changamoto katika kunyonya, anapata kikohozi kisichoisha na uzito unaacha kuongezeka,” amesema.

Amesema pia kuna mtoto mwingine mwenye miaka 13 kutoka Moshi aliyelazimika kuacha michezo na hata kushindwa kulala vizuri kutokana na matatizo ya kupumua, kabla ya kubainika kuwa na tatizo la moyo.

Kwa mujibu wa daktari huyo, magonjwa ya moyo yapo katika makundi matatu makuu: ya kuzaliwa nayo, yanayopatikana baada ya kuzaliwa, na yale yanayohusiana na mtindo wa maisha.

Ameonya kuwa baadhi ya magonjwa hayo yanaweza kuzuilika au kutibika mapema endapo yatagundulika kwa wakati, lakini wengi huchelewa kufika hospitalini.

“Inatia uchungu kuona wagonjwa wanakuja katika hatua mbaya wakati ugonjwa ungeweza kutibika mapema,” amesema.

Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Gileard Masenga amesema hospitali hiyo imeanzisha mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha matibabu ya moyo na mishipa ya damu. Amesema KCMC, ambayo ni hospitali ya rufaa ya kanda ya Kaskazini inayohudumia zaidi ya wakazi milioni 11, imekuwa ikitoa huduma za kibingwa bobezi kwa zaidi ya miaka 55.

Hospitali hiyo inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kufanya kazi kwa ubia na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo imekuwa ikichangia mishahara na kusimamia miongozo ya utoaji huduma.

Masenga amesema jitihada hizo zimewezesha hospitali kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi, huku ikiendelea kuboresha huduma, ikiwemo kuanza kutoa tiba ya saratani kwa mionzi mwaka huu.

Amesema mradi wa kituo cha moyo unalenga kuwa na huduma kamili, ikiwemo kinga, elimu kwa umma, uchunguzi wa mapema, tiba kupitia mishipa ya damu, na upasuaji mkubwa.

“Tunataka kuwa na taasisi itakayofanya kila kitu kinachohusu matibabu ya moyo ili kupunguza mzigo wa wagonjwa wanaokwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI),” amesema.

Kwa mujibu wa Masenga, jengo hilo litakuwa na ghorofa tatu, vitanda 114, vyumba viwili vya upasuaji mkubwa, vyumba viwili vya upasuaji wa mishipa, maabara, vyumba vya wagonjwa mahututi, na kliniki za wagonjwa wa nje kwa watoto na watu wazima.

Gharama za ujenzi zinakadiriwa kufikia Sh25 bilioni huku vifaa tiba vikitarajiwa kugharimu kiasi kama hicho. Amesema tayari asilimia 90 ya fedha za ujenzi zimepatikana kupitia ubia na taasisi kutoka Marekani, huku wataalamu wakipelekwa nje ya nchi, ikiwemo India kwa mafunzo maalum.

“Ni gharama kubwa, lakini maisha ya binadamu yana thamani kubwa zaidi,” amesema Masenga. Ametoa wito kwa Watanzania na wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia kukamilisha asilimia 10 ya fedha zilizobaki ili kufanikisha mradi huo, akisisitiza kuwa uwekezaji katika huduma za moyo utasaidia kuokoa maisha ya maelfu ya Watanzania na kupunguza mzigo wa rufaa katika hospitali chache zilizopo nchini.

“Niwaombe Watanzania kuungana nasi katika ujenzi wa jengo hili muhimu. Lengo letu ni kuuzindua mradi huu ifikapo mwaka 2027,” amesema.