Kesi ya mauaji inayowakabili wanamgambo yapigwa kalenda

Mwanza. Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana Mkoa wa Mwanza imesema haina mamlaka ya kutoa uamuzi katika kesi ya mauaji inayowakabili wanamgambo wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji ya kijana mmoja, hivyo inatakiwa iende Mahakama ya Kuu ya Tanzania.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Amani Nelson Sumari, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, amesema hayo leo Aprili 4, 2026 katika mahakama hiyo na kupanga siku nyingine ya kurudi mahakamani kwa washtakiwa kupewa kibali cha kwenda Mahakama ya Kuu.

“Upelelezi utakapokamilika, Mahakama itakabidhi mwenendo (Committal) ili kupeleka kesi hiyo Mahakama Kuu ikasikilizwe. kosa linalowakabili halina dhamana, mtabaki rumande hadi siku ya Aprili 24, 2026,” amesema.

Kukabidhi mwenendo ni mchakato wa kisheria ambapo kesi inatolewa kutoka Mahakama ya Chini (kama Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu Mkazi) na kupelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa rasmi.

Hati ya mashtaka imesomwa na Sophia Warinda, mwanasheria wa Serikali, kuwa kosa wanaloshtakiwa nalo ni mauaji kwa mujibu wa kifungu namba 196 na 197 cha sheria ya adahabu, sura ya 16 marejeo ya mwaka 2023.

Washtakiwa hao ni Ibrahim Mwita (25), wa Bugando Mission, Zongori Makongoro (48), mkazi wa Bugarika, Genge Mwita (45), mkazi wa Igogo.

Tukio hilo la mauaji lilitokea Machi 20, 2026 kwa watuhumiwa hao kudaiwa kumuua Rashid Nyandonga (31), fundi simu na mkazi wa Bugando Jeshini, Wilaya ya nyamagana mkoani humo.

Mama wa kijana huyo, Anna Nyandonge (62) ameiomba Serikali imsaidie kupata haki katika kesi hii ya mauaji ya mtoto wake.

“Namuomba Mama Samia na Serikali yake anisaidie kupata haki ya mwanangu, yeye ndiye tegemezi kwenye maisha yangu na ameniacha na watoto wawili nikiwa sina hata tegemezi wala kitega uchumi chochote kile,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, Machi 22, 2026, tukio hilo lilitokea saa 12:45 jioni katika Mtaa wa Mission, eneo la Sahara, Kata ya Pamba.

Kesi hiyo itasikilizwa tena Aprili 24, 2026.