KUNA mechi mbili za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) zinachezwa leo Ijumaa huku ile ya KMKM dhidi ya Mafunzo kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, imekaa kimtego ikisubiri kutoa hukumu kutokana na msimamo wa ligi hiyo ulivyo.
Wakati KMKM ikicheza na Mafunzo, Kipanga yenye alama 35 ikishika nafasi ya sita, itaikaribisha New King iliyopo ya 10 na 11 na alama 28, itachezwa kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja.
Kwa sasa KMKM ipo nafasi ya tisa na alama 29, wakati Mafunzo ni ya 12 ikikusanya alama 27, hivyo zimetofautishwa kwa alama mbili pekee hali inayofanya mechi kutarajiwa kuwa ngumu zaidi.
Kocha Msaidizi wa Mafunzo, Haji Ramadhan, amesema makosa waliyofanya huko nyuma, wameyafanyia kazi na kujiweka imara zaidi.
Amesema, yaliyojitokeza kwenye mchezo wao dhidi ya KVZ, hawatamani kuona yanajirudia, hivyo wanaamini leo mbele ya KMKM watavuna alama tatu.
“Timu zote mbili hazipo kwenye nafasi nzuri ya msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar, hivyo tunaamini mechi hiyo itakuwa na ushindani mkubwa ndani yake,” amesema.
Alifafanua timu hiyo imejitayarisha vizuri kuhakikisha inavuna pointi tatu ambazo zitaiondoa kwenye nafasi yenye presha ya kushuka daraja.
Amesema, katika kikosi hicho, mchezaji Jaku Joma ana majeraha ambayo yamesababisha kutokuwa sehemu ya mchezo, lakini wengine wanaendelea vizuri.
Alisisitiza mchezo huo hautakuwa rahisi kwa pande zote mbili kwani kila mmoja anahitaji kujinasua kwenye nafasi aliyopo na kusonga mbele.
Kocha huyo amesema mchezo uliopita dhidi ya KVZ umekuwa kipimo kizuri cha kurekebisha makosa ambayo yaliigharimu timu hiyo na wapo tayari kuivaa KMKM.
Kiungo mkabaji wa Mafunzo, Ibrahim Ramadhani Juma amesema mchezo huo utakuwa mgumu lakini watapambana kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika nafasi nzuri.
Timu zote mbili zinaingia katika mchezo wa leo zikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mechi zilizopita na Mafunzo ilifungwa mabao 3-1 dhidi ya KVZ, huku KMKM ikichapwa bao 1-0 na New King.
Kwa upande wa kiungo mshambuliaji wa KMKM, Imran Mohammed Abdallah “Jaba” amesema hawapo tayari kurudia makosa ya mchezo uliopita na kupelekea kupoteza, hivyo watacheza kwa umakini.
Jaba amesema mchezo huo hautokuwa mwepesi kwa sababu Mafunzo ni timu nzuri na ukizingatia kila timu ina uhitaji ili kujiweka katika nafasi nzuri kwa hiyo watakuwa makini.
