KOCHA Mkuu wa Hausung FC ya Njombe, Selemani Kitunda Simota ‘Guardiola’, amesema amekuwa na kipindi kirefu cha kukaa na kuzungumza na wachezaji wa timu hiyo, huku malengo makubwa yakiwa ni ya kuweka mikakati ya kufanya vizuri Ligi ikirejea.
Guardiola, amejiunga na kikosi hicho ambacho kinacheza Ligi ya Champioship msimu huu wa 2025-2026, baada ya kuondoka kwa aliyekuwa Kocha Mkuu, Zulkifri Iddi ‘Mahdi’, aliyejiunga na IAA SC ya jijini, Arusha inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Guardiola, amesema baada ya kukabidhiwa majukumu hayo alianza mapema kufanyia kazi changamoto zilizokuwepo awali, ikiwemo kutengeneza balansi nzuri ya kikosi hicho, kuanzia eneo la kujilinda hadi la ushambuliaji.
“Tumekuwa na wakati mzuri kwa maana ya kukaa na kuzungumza na wachezaji kwa ajili ya kuhakikisha tunarejea katika nafasi nzuri ya kiushindani, jambo la kufurahisha tumekuwa na kipindi cha mwezi mmoja tangu Ligi imesimama,” amesema Guardiola.
Kitunda anayefananishwa na Kocha wa Manchester City ya England, Pep Guardiola, katika karia yake ya soka amecheza timu mbalimbali za Kikwajuni FC, Polisi Pemba na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo maarufu KMKM FC zote za visiwani, Zanzibar.
Licha ya kucheza Kikwajuni FC, Polisi Pemba na KMKM FC, ila, Kitunda amewahi pia kuzifundisha timu mbalimbali, zikiwemo, Tunduru Korosho, Stand United ‘Chama la Wana’, Cosmopolitan na mabingwa wa Ligi Kuu mwaka 1982, kikosi cha Pan Africans.
Hausung imepanda daraja msimu huu na kushiriki Ligi ya Championship baada ya kuongoza kundi A na pointi 25, ikiungana na mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2024-2025, Gunners FC ya Dodoma, iliyoongoza pia kutoka kundi B na pointi 35.
Timu hiyo inayotumia Uwanja wa Amani uliopo Mkoa wa Njombe, katika mechi 21, ilizocheza msimu huu imeshinda tatu, sare mbili na kupoteza 16, ikishika nafasi ya 14 na pointi 11, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 14 na kuruhusu 37.
