Kibubu cha akiba ya wafanyakazi, ambacho kimemtunzia akiba yake kwa miaka 40 ya ajira, huyu mstaafu, kimefanya kile kinachoamini kuwa ni bonge la kuboresha maisha ya huyu mstaafu, ili aweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha, hususan tangu alipostaafu na kuambiwa sasa matibabu ya dezo kwa wazee ni maneno ya kanga tu!
Kibubu kinajifagilia kwamba kinamboreshea maisha mstaafu kwa ‘kumpa’ Sh5.5 milioni, akishakuwa rasmi mkazi wa Kinondoni na si akiwa hai, ili aweze kurudi mavumbini alikokuwa kwa amani!
Kibubu kinamfanya mstaafu kujiuliza sana kwamba kimeingiwa na huruma gani ghafla ya kumpa mstaafu Sh5.5 milioni pale Mungu anapochukua pumzi yake ya uhai aliyompa, lakini hakikuwa na huruma hiyo wakati akipokea pensheni ya shilingi laki moja na elfu tano kwa miaka 21 aliyoipitisha akiomba nyongeza ya pensheni hiyo na kibubu kikawa bize kujenga ‘vikwangua anga’ tu nchini!
Mstaafu wetu angependa kukiambia kibubu chake kwamba baada ya kustaafu na miaka 60, yeye sasa amebakisha miaka miwili au mitatu kufikisha ule umri anaotuambia Mungu mwenyewe kuwa amempa binadamu uwezo wa kufanya ‘vitu vyake’ atakavyotaka, lakini akiishafika miaka 70, safari yake ya kuwa mkazi wa kudumu wa Kinondoni itamhusu wakati wowote ule, anachostahili sasa ni heshima tu akiwa hai!
Kweli mstaafu wa miaka 70 apate Sh5.5 milioni zake achanyikiwe mpaka apoteze hesabu yake ya mwisho wa maisha? Hiyo si ni hela yake aliyoitolea jasho na damu yake wakati akiijenga nchi hii, na sasa wanataka kumpa akiwa tayari anaitwa kwa ‘past tense’ (‘kisambaa’ kwa msisitizo!)? Hapo kweli kibubu kinaweza kujinasibu kuwa kimempa mstaafu Sh5.5 milioni za jasho lake ajipongeze huku kibubu kikimpa hela hiyo akiwa amerudi mavumbini?
Waheshimiwa, acheni ‘mijiroho mibaya’. Chambilecho ndugu zangu wa nyumbani Tanga, mbona wale wanaolipwa Sh14 milioni na ushee kwa mwezi wakiwa hai hamuwawekei mikwara kuwa wanaweza kuzitapanya zote kwa kuchanganyikiwa, lakini sisi tunaolipwa pensheni ya shilingi laki mbili na elfu hamsini tu kwa mwezi ndiyo tutazitapanya, na ndiyo maana mtatupa hela hiyo tukiwa marehemu na si tukiwa hai? Acheni hizo!
Wastaafu wanaomba kumhimiza kiongozi wa nchi afanye ‘uteuzi’ wa dharura ili Sh5.5 milioni ‘ziteuliwe’ haraka kwenda kwenye mifuko ya wastaafu wa kima cha chini wakiwa hai na si wakiwa wakazi wa kudumu wa Kinondoni, kama kibubu chao kinavyotaka kutoa fedha hizo kwa mstaafu akishakufa na si akiwa hai! Yaani kuna watu na madigrii yao kibubuni wanauwaza utani huu mbaya sana kwa maisha ya wastaafu? Utenguzi uwahusu!
Wastaafu tunamuomba mheshimiwa kiongozi wa nchi auharakishe ‘uteuzi’ huu wa Sh5.5 milioni fasta ili uingie mifukoni mwa wastaafu walio hai na si mpaka wakiwa maiti, ili uteuzi usije ukasitishwa ghafla kwa gharama ya mafuta kupanda juu, maana mstaafu hana hata uhakika vinahusiana vipi!
Ndiyo, gharama za maisha zinazoletwa na gharama za mafuta kupanda juu fasta, lakini mstaafu ataamini kuwa kweli gharama za mafuta zimepanda pale atakapoona siri kali ikilazimika kupunguza mishahara ya wale binadamu tunaoaminishwa kuwa, licha ya sisi wote kuwa sawa, lakini wao wako ‘sawa’ zaidi kuliko sisi wengine kiasi cha kulipwa Sh14 milioni na ushee kwa mwezi, wakati sisi tukipambana na pensheni ya shilingi laki mbili na nusu kwa mwezi, huku tukisubiri kupata Sh5.5 milioni eti tukiwa mavumbini tulikotoka na si tukiwa hai!
Mama, ‘uteuzi’ wa Sh5.5 milioni uwahusu fasta wastaafu wa kima cha chini wakiwa hai, ambao hata idadi yetu sasa ni chini mno. Tunaamini kuwa Taifa halitaingia hasara yoyote kwa kutupongeza kwa kuijenga nchi ‘dakika za mwisho mwisho’ za uhai wetu! Tusingoje tuwe wakazi wa kudumu wa Kinondoni ndipo mtupe Sh5.5 milioni. Kumbukeni sisi ndiyo tumeijenga nchi hii!
0754 340606 / 0784 340606
