MSHAMBULIAJI wa zamani wa Mbeya City, Habib Kyombo, amesaini mkataba wa mwaka mmoja na Klabu ya Napsa Stars ya Ligi Kuu Zambia.
Kyombo anakuwa mchezaji wa pili wa Kitanzania kujiunga na chama hilo ambapo awali Yusuph Athuman alitambulishwa msimu uliopita.
Mtanzania mwingine anayeitumikia ligi hiyo ni Alon Nyembe anayekipiga Zanaco FC.
Akizungumza na Mwanaspoti kuhusu dili hilo, wakala wa mchezaji huyo, Hon Simbeye, amesema Napsa walikuwa wakimfuatilia Kyombo tangu akiwa katika kikosi cha Simba kabla ya kujiunga na Mbeya City.
Ameongeza kuwa Napsa wameona kuna haja ya kumuongeza Kyombo kwenye eneo la ushambuliaji akasaidiane na Yusuph.
“Ni mchezaji mzuri na dili lake lilianzia tangu akiwa Simba, Napsa walimuona kupitia mechi za kimataifa hivyo wakaona ni mshambuliaji mzuri na anaweza kuongeza kitu kwenye kikosi hicho,” amesema Simbeye.
Kwa upande wake, Kyombo amesema: “Nashukuru kupata nafasi hii naamini kwa kushirikiana na wenzangu tunaweza kusaidia timu kutimiza malengo yake.”
Kihistoria, Napsa Stars ni moja ya klabu zinazoheshimika Zambia, huku mafanikio yake makubwa ni kutwaa taji la Kombe la Shirikisho la Zambia (ABSA Cup) 2022, ubingwa uliowapa nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuishia hatua za awali.
Kabla ya kujiunga na chama hilo, miaka michache iliyopita Kyombo alizitumikia Pamba Jiji, Mbeya City, Singida Black Stars na Simba.
