Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimesma kimewasilisha mambo manne kwa Mjumbe Maalumu wa Jumuiya ya Madola, Lazarus Chakwera ikiwemo madai ya Uchaguzi wa Tanzania Oktoba 29 mwaka jana kutokuwa huru na haki.
ACT imedai kuwa uchaguzi huo ulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi, na kulikuwepo na matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Madai mengine ya ACT Wazalendo, ni ukiukwaji wa haki za binadamu kabla na baada ya uchaguzi, kuminywa kwa uhuru na haki ya kiraia na kijamii, pamoja na mageuzi ya kisiasa na uwajibikaji unaohitajika.
Katika taarifa yake kwa umma iliyotolewa na Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu, ACT Wazalendo imedai uchaguzi huo “uligeuzwa kuwa mchakato wa kupanga matokeo” na kwamba matukio yaliyofuata yalileta mgogoro wa uhalali wa kisiasa wa Serikali inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan.
Chama hicho kimesema tathmini yake inategemea ushahidi uliokusanywa kabla, wakati na baada ya uchaguzi, ikiwemo hatua za uteuzi wa wagombea, upigaji kura, uhesabuji na utangazaji wa matokeo.
“Kwa mujibu wa tathmini yetu, Tanzania kwa sasa inakabiliwa na hali mbaya ya kisiasa inayoashiria kuporomoka kwa demokrasia ya vyama vingi na kuimarika kwa utawala unaotegemea vyombo vya usalama,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu akiwa na Mjumbe Maalumu wa Jumuiya ya Madola, Lazarus Chakwera leo Ijumaa, Aprili 10, 2026 jijini Dar es Salaam.
ACT Wazalendo pia imedai kuwa wagombea wake wa urais na ubunge waliondolewa katika mazingira yasiyo ya haki, huku zaidi ya asilimia 30 ya wagombea wa ubunge na asilimia 22 ya udiwani wakikosa nafasi ya kushiriki.
Aidha, chama hicho kimesema katika uchaguzi huo kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa wanachama wao kupigwa, kukamatwa kiholela, kubambikiwa kesi na wengine kuuawa kikatili.
Pia, chama hicho kimeeleza, mamia ya wananchi wamejeruhiwa kufuatia uchaguzi huo,watu kupotea na wengine kushikiliwa bila taarifa.
“Tathmini ya ACT Wazalendo inaonesha kudhoofika kwa mazingira ya uhuru wa kiraia na kijamii nchini Tanzania, ambapo haki za msingi za raia zimeendelea kubanwa na kupungua nafasi ya wananchi kushiriki kikamilifu katika maisha ya umma.
“Hali hii imejidhihirisha kupitia vikwazo katika uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kushirikiana, pamoja na ongezeko la hofu katika jamii,” taarifa hiyo imeeleza.
Kuhusu uminywaji wa uhuru na haki ya kijamii, taarifa hiyo imeeleza hali hiyo imejidhihirisha kupitia vikwazo katika uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kushirikiana, sambamba na ongezeko la hofu miongoni mwa jamii, hali inayoathiri ushiriki wa wananchi katika masuala ya kijamii na kisiasa.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa vikihusishwa na matukio ya tuhuma za utekaji, wakati vyombo vya habari navyo vikikabiliwa na vikwazo vya kiutendaji ikiwemo udhibiti wa vipindi, kusimamishwa kwa baadhi ya vituo na kuondolewa hewani kwa vipindi vya uchunguzi,” ACT Wazalendo kwenye taarifa yake imeeleza.
Kwenye mageuzi ya kisiasa na uwajibikaji unaohitajika,ACT Wazalendo imesema, hali ya sasa inaashiria kudhoofika kwa demokrasia na kupungua kwa uhuru wa kiraia na kijamii.
Hali hiyo inayotokana na kile ACT Wazalendo wanachodai ni athari za mchakato wa Uchaguzi Mkuu na matumizi ya nguvu katika siasa, jambo linalohitaji hatua za haraka za kitaifa kurekebisha mwelekeo wa kisiasa na kisheria nchini.
“ACT Wazalendo inaona kuna mgogoro wa uhalali wa kisiasa nchini Tanzania, unaohitaji mageuzi ya haraka ya kikatiba, uchunguzi huru wa matukio ya Oktoba 29, 2025, pamoja na kuachiliwa huru kwa wafungwa wa kisiasa ili kurejesha imani ya wananchi kwa demokrasia na utawala bora.” Amesema.
Chakwera amewasili nchini Aprili 08, 2026 na kupokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe na alianza ratiba yake kwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo Aprili 9, 2026 Dar es Salaam.
Wakati wa ziara hiyo ambayo itahimishwa Aprili 16, 2026, Chakwera amepangiwa miadi ya kukutana na viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia na viongozi wastaafu.
