KABLA ya kuondoka KMC Desemba 2025, Kocha Mbrazili, Marcio Maximo amesema kupitia usajili wa dirisha dogo la Januari 2026, lazima kikosi hicho kifanye maboresho ya kusajili wachezaji watakaoipambania timu kukaa nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Hata hivyo, hakufika Januari, akasitishiwa mkataba wake kwa makubaliano ya pande mbili, huku nafasi yake ikichukuliwa na Abdallah Mohamed ‘Bares’ ambaye naye amefikia makubaliano ya kuchana na kikosi hicho, Aprili 4, 2026.
Sasa baada ya Bares naye kuondoka, Maximo ameibuka na kusema haitakuwa rahisi kwa mwalimu yeyote kuinusuru KMC kutokana na ubora walionao wachezaji kwani yalifanyika makosa ya msingi wakati wa maandalizi mwanzoni mwa msimu kipindi yeye ndiye kocha mkuu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maximo amesema, changamoto kubwa inayoikumba KMC ni ubora wa wachezaji waliopo kikosini, kwani baadhi wanashindwa kuhimili presha ya ushindani wa Ligi Kuu.
“Hali hiyo imekuwa ikiathiri matokeo ya timu uwanjani na kuifanya kushindwa kupata ushindi, ningependa kuona msimu unaanza upya ili kikosi hicho kiandaliwe kwa umakini zaidi na kwa mtazamo tofauti.
“Hata hivyo, hilo haliwezekani kwa sasa jambo linaloifanya timu kuendelea kubeba matatizo yaleyale, hali hiyo itaendelea kuiweka KMC kwenye wakati mgumu huku ikiwa ni changamoto kubwa kwa makocha wanaoiongoza kurekebisha makosa yaliyofanyika awali,” amesema Maximo.
Kwa sasa KMC inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi nane baada ya kucheza mechi 18, imeruhusu mabao 33 na yenyewe ikifunga matano.
Maximo ilianza msimu na kikosi hicho ambaye alidumu kwa siku 131, akiwa ameongoza mechi tisa za Ligi Kuu Bara, huku akiambulia ushindi mara moja pekee na vipigo saba, sare ikiwa moja.
Baada ya kuondoka Maximo, Desemba 30, 2025 alitambulishwa Bares kuchukua nafasi yake ambapo aliiongoza KMC kwenye mechi nane za ligi, akishinda moja, sare moja na kupoteza sita, akaondoka Aprili 4, 2026 baada ya kudumu kwa siku 94. Juzi wakati inafungwa na Singida Black Stars, KMC iliongozwa na Imani Mwalupetelo akikaimu nafasi ya kocha mkuu.
