Mbeya City mzuka umepanda | Mwanaspoti

MZUKA umeanza kupanda. Ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya Mbeya City kukusanya pointi nne katika michezo miwili, huku ikitoa matumaini kuwa kazi iliyobaki ni mchezo wa kesho dhidi ya Singida Black Stars katika Kombe la Shirikisho la CRDB ili kusaka heshima.

Timu hiyo ambayo kwa sasa inatumia uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mjini Babati, mkoani Manyara imeonekana kuamka baada ya kutokuwa na mwanzo mzuri baada ya matokeo waliyopata katika mechi mbili mfululizo.

City ilianza na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya KMC kisha suluhu ya bila kufungana mbele ya Azam FC na kubaki nafasi yake ya 12 kwa pointi 17 baada ya michezo 18 na kubakiza dakika 1080 kujua hatma yao msimu huu.

Hata hivyo, timu hiyo inatarajia kushuka tena uwanjani kuwakabili Singida Black Stars katika mchezo wa kombe la shirikisho hatua ya 16 bora kuisaka nafasi ya robo fainali ya michuano hiyo, mechi ikipigwa Aprili 12 mkoani Singida.

Nahodha wa timu hiyo, Eliud Ambokile ameliambia Mwanaspoti matokeo hayo yamerejesha nguvu, ari na morali mpya kikosini na kutoa mwelekeo mzuri katika vita ya kukwepa kushuka daraja.

Amesema kwa sasa timu imeonekana kuimarika na kubadilika kwa kuwa kwa katika mechi nne mfululizo licha ya matokeo mengine kutokuwa mazuri, lakini wamepata bao hali inayoonesha uimara eneo la ushambuliaji.

“Tunauona mwanga mpya kwa kuwa Azam ni timu kubwa ila tulipata pointi moja kwao, kwetu si matokeo mabaya na ni mwendelezo wetu katika kupata pointi kwenye mechi mbili mfululizo.

“Kwa mechi za karibuni tumekuwa na wastani wa kupata bao hili linatupa matumaini washambuliaji kwamba kuna kitu tumefanikisha, kimsingi tunaendelea kupambana kuhakikisha tunabaki salama,” amesema Ambokile.

Kuhusu hesabu za namna ya kuinusuru timu, nyota huyo mkongwe amesema kwa mechi 12 zilizobaki ni kufa au kupona kuhakikisha wanapata pointi tatu kila mchezo ili kufikia malengo.