Nafasi ya urais ni ya juu zaidi katika nchi; inaambatana na wajibu mkubwa wa kuusimamia ili kukidhi matarajio ya wananchi katika kuwaletea maendeleo na kujenga hatima yao njema, hasa kuwafanya wawe na furaha.
Baadhi ya watu wamejitosa kuwania nafasi hiyo mara kadhaa licha ya kwamba ni wachache waliofanikiwa kushinda uchaguzi na kubeba jukumu hilo. Hata hivyo, kwa wengine, dhamira hiyo bado haijafa.
Aliyekuwa mgombea wa urais wa Tanzania kupitia chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Wilson Elias, anasema ndoto yake ya kuutaka wadhifa huo ili kuwatumikia wananchi bado haijaisha; anajipanga kwa awamu ijayo.
Elias alikuwa mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, akiwa sambamba na wagombea wengine 16 walioteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kushiriki uchaguzi huo.
Katika uchaguzi huo, mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, alitangazwa mshindi baada ya kupata asilimia 98 ya kura zilizopigwa. Elias alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 12,898, sawa na asilimia 0.04 ya kura zote zilizopigwa.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na Salum Mwalimu Salum wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), aliyepata kura 213,414, sawa na asilimia 0.65. Katika kinyang’anyiro hicho, vyama viwili vikubwa havikusimamisha wagombea wao.
Vyama hivyo, vilivyotarajiwa kuongeza ushindani na kupunguza kura za Rais Samia, havikushiriki kwa sababu tofauti. Mgombea wa ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, aliondolewa na INEC katika kinyang’anyiro hicho kwa kukosa sifa.
Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilijitenga na mchakato wa uchaguzi na badala yake kikaelekeza nguvu zake katika kudai mabadiliko ya mfumo wa INEC ili kuhakikisha chombo hicho kinatenda haki na kwa uwazi.
Mbio za urais kwa Elias hazikuanzia ADC, bali alianzia katika chama cha Tanzania Labour Party (TLP). Baada ya kukosa nafasi hiyo, alijiunga na ADC na kuomba nafasi ya kuwania urais kupitia chama hicho, jambo ambalo alifanikiwa.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Elias amesema ndoto yake ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho ni kuwa Rais wa Tanzania ili kuboresha maisha ya wananchi.
“Nilishiriki uchaguzi mkuu nikiwa na ndoto ya muda mrefu ya kuwa Rais wa Tanzania. Ndoto hiyo haikutimia, lakini nashukuru Mungu kwa kuwa umri wangu bado unaruhusu. Nina uwezo, nina sababu, na nina nia. Naendelea kujipanga na nitaingia tena,” anasema.
Anasema matokeo aliyoyapata ni makubwa kwake, hasa ikizingatiwa kuwa hakuwa na uzoefu wa awali wa kuwania nafasi hiyo. Anaongeza kuwa anajipanga kuja na sera mpya baada ya kuzunguka nchi nzima na kuelewa mahitaji ya wananchi.
“Nitakuja na sera mpya ambazo naamini nitazifafanua vizuri kwa wananchi ili wazielewe. Njozi ya kuutaka urais bado ipo palepale. Sina nia ya kugombea nafasi nyingine hata ndani ya chama; waliopo wanafanya kazi nzuri,” anasema.
Elias anasema mipango yake ya kuingia Ikulu ni kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo, ambayo inaajiri wananchi wengi lakini bado uwekezaji wake umekuwa mdogo.
“Katika eneo hili, nashauri hata chama kilichoshinda kuongoza dola kuzingatia hilo. Ni matarajio yangu kuona ardhi ya Tanzania inatumika vizuri, hasa kwa kuwekeza kwenye zao la mpunga aina ya Basmati, ambao una mahitaji makubwa katika soko la dunia,” anasema.
Anasema ametembelea Kenya na kuona kuwa wameanza uwekezaji wa zao hilo katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo, wakiwa na lengo la kuliteka soko la kimataifa.
“Mchele wa Basmati unapendwa sana duniani kwa sasa. Misri na nchi nyingine pia zinawekeza kwenye zao hilo. Ni muhimu kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kila zao, hasa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini,” anasema.
Elias anasema mpango huo unaweza kutekelezwa iwapo kutakuwa na utashi wa kisiasa wa kutoa ruzuku kwa mbegu, pamoja na kuwezesha usafirishaji wa mbegu za Basmati kutoka India ili zisambazwe bure kwa wakulima.
“Wananchi wapewe mbegu bure na kwa mwaka wa kwanza wasiruhusiwe kuuza mazao hayo bila usimamizi maalumu. Wakulima wasaidiwe kitaalamu na ikiwa mpango huu utatekelezwa, ndani ya miaka mitatu nchi inaweza kupiga hatua kubwa na kuongeza mapato ya fedha za kigeni,” anasema.
Machi 31, 2026, Rais Samia alifanya mazungumzo na wagombea wa nafasi ya urais na wagombea wenza kutoka vyama vya siasa 16 vilivyoshiriki uchaguzi mkuu, yaliyoanza Ikulu jijini Dar es Salaam. Elias, mmoja wa washiriki wa mazungumzo hayo, anasema ajenda kuu iliyojadiliwa ni kufanya maridhiano ya kitaifa na njia zinazopaswa kutumika.
“Ikiwa muda wote unapinga kwenye majukwaa, lakini haupati muda wa kwenda kumshauri faragha au kukaa na kujadiliana naye kuhusu makosa yake na hatua zinazopaswa kuchukuliwa, ndipo ambapo kuna shida katika taifa letu,” anasema.
Anasema umoja na mshikamano ni muhimu katika mataifa ya Afrika. Elias anasema kwamba, kwa bahati nzuri, amezunguka mataifa mengi, hasa ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kwa mfano Zimbabwe, ambayo inapitia vikwazo vinavyoathiri taifa hilo.
“Matokeo yake, kila mwaka wanafanya maombi ya kuliombea taifa kwa siku 10. Ni muhimu hata kwa vyama vya upinzani kuwa kitu kimoja linapofika suala la maslahi ya taifa kwa ustawi wa jamii,” anasema.
Elias anafafanua kuwa walishiriki mazungumzo hayo na Rais Samia kwa ajili ya maslahi ya taifa, huku wakiwanufaisha pia vyama vya upinzani. Ushauri waliotoa hauwezi kuuweka wazi kwa sasa kwa sababu wanasubiri utekelezaji.
Kuhusu ukimya baada ya uchaguzi
Kuhusu wagombea urais kutokuwapo baada ya uchaguzi, Elias anasema wanakaa kimya kwa sababu ni muda wa chama kilichoshinda kuunda serikali na kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.
“Tulioshindwa tunaendelea na shughuli zetu za kiuchumi; binafsi mimi ni mkulima wa zao la mkonge Tanga, kwa hivyo narudi kwenye shughuli zangu kujipanga upya,” anasema.
Anasema hali hiyo si ya kipekee Tanzania pekee, bali hata katika mataifa makubwa kama Marekani, hakuna mshindani anayetoka hadharani kuzungumza au kufanya mikutano mara kwa mara.
“Shughuli zetu za kisiasa ni tofauti na mchezo wa soka. Labda utaona wasemaji muda wote wakiendelea kuzungumza, lakini wanasiasa, mchezo wetu unafanyika mwaka mmoja kila baada ya miaka mitano,” anasema.
Elias anasema kujitokeza mara kwa mara wakati mwingine kunachangia kupoteza mvuto wa kisiasa.
Kuhusu rasilimali za umma ambazo hazinufaishi wananchi, Elias anasema tatizo ni uadilifu. Anasema uwajibikaji lazima uhimizwe kwa watumishi wa umma na wananchi wote. Serikali imechukua hatua, lakini ni lazima kutekeleza mkakati maalumu.
“Mali za umma lazima zilindwe. Kuna Mahakama ya mafisadi iliyoundwa, lakini utekelezaji wake unazua wasiwasi. Tunaiomba serikali ichukue hatua kali dhidi ya wabadhirifu wa mali za umma ili iwe fundisho kwa jamii,” anasema.
Anasema watumishi na wasimamizi lazima wawe wazalendo na wakali katika kulinda rasilimali za umma, wakiwa na wivu wa kimaadili, kwa kutambua kuwa nafasi hizo ni dhamana.
“Nyuma yao kuna wananchi wengi wanaotarajia kuona manufaa na maisha bora. Haitakuwa na maana ikiwa rasilimali zipo lakini tija yake haionekani,” anasema.
